Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2020-2025 | Session 11 | Sitting 42 | Water and Irrigation | Wizara ya Maji | 557 | 2023-06-07 |
Name
Dr. Charles Stephen Kimei
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vunjo
Primary Question
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Mabwawa katika Mito Ghona, Rau na Deu ili kupunguza athari za mafuriko?
Name
Maryprisca Winfred Mahundi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Vunjo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mito ya Ghona, Rau na Deu inapitisha maji kiasi cha lita 103,310 kwa sekunde (sawa na mita za ujazo 267,940.21 kwa siku) ambapo Mto Rau ni lita 98,000 kwa sekunde, Mto Dehu Lita 3,100 sekunde na Mto Ghona ni lita 2,210 kwa sekunde. Mito hiyo hupeleka maji yake katika Mto Ruvu na hatimaye kufika katika Bwawa la Nyumba ya Mungu. Serikali kupitia Bodi ya Maji Bonde la Pangani imeshafanya upembuzi wa awali na kubaini kuwa sehemu ya maji ya mito hiyo haifiki kwa wakati kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu na badala yake husambaa na kuacha mkondo wake na kuathiri wananchi kandokando ya mito hiyo ikiwemo Vijiji vya Chekereni na Kileo kupitia Mto Ghona; maeneo ya Majengo, Msaranga, Mabogini, Oria, Ngasini, Mandakamnono yanayoathiriwa na Mto Rau; na Vijiji vya Mongalia, Soko, Ngaseni na Kiterini huathiriwa pia kupitia Mto Deu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu kubwa ya maji ya mito hiyo kusambaa ni kutokana na kuharibika kwa kingo za mito husika katika maeneo ya tambarare kunakosabisha maji kutoka katika mikondo yake na kusambaa katika maeneo wanayoishi wananchi. Serikali imeanza kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na ufukuaji wa mikondo ya mito katika baadhi ya maeneo korofi ya mito hiyo na kazi ya ufukuaji itaendelea katika Mwaka wa Fedha 2023/2024 mpaka itakapokamilika. Aidha Bonde la Pangani litafanya tathimini kwenye maeneo yanapitiwa na mito hiyo ili kubaini kama kuna uwezekano wa kujenga mabwawa bila kuathiri upatikanaji wa maji katika Bwawa la Nyumba ya Mungu ambalo linatumika katika shughuli nyingi za kijamii na kiuchumi.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved