Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2020-2025 | Session 11 | Sitting 50 | Finance and Planning | Wizara ya Fedha na Mipango | 654 | 2023-06-19 |
Name
Agnesta Lambert Kaiza
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. AIDA J. KHENANI K.n.y MHE. AGNESTA L. KAIZA aliuliza:-
Je, kwa nini Serikali isisamehe kodi na kuondoa baadhi ya tozo katika Sekta ya Elimu na Afya ili kuvutia taasisi binafsi?
Name
Hamad Hassan Chande
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kojani
Answer
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitoa misamaha ya kodi katika Sekta ya Elimu na Afya kwa kuzingatia sheria na miongozo mbalimbali kama ifuatavyo: -
(a) Kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332:-
(i) Wafanyabiashara wanaojihusisha na utoaji wa huduma za afya na elimu wanasamehewa kulipa kodi ya makampuni yanayotangaza kupata hasara kwa mfululizo wa miaka zaidi ya mitatu;
(ii) Mchango wowote anaofanya mfanyabiashara kwa ajili ya kuchangia Mfuko wa Elimu anajirejeshea kama gharama wakati wa kutengeneza faida;
(iii) Taasisi yoyote iliyoanzishwa kwa ajili ya kujishughulisha na uendelezaji wa elimu na afya au kutoa huduma za umma kwenye Sekta za Afya na Elimu imepewa hadhi ya charitable organization na kupata unafuu wa kodi.
(b)Kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura 148:-
(i) Msamaha wa kodi umetolewa katika ujenzi wa majengo kwa ajili ya kutoa huduma za afya na elimu kwa jamii;
(ii) Bidhaa na huduma zinazoingizwa nchini na Serikali au kununuliwa katika soko la ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi katika Sekta ya Afya na Elimu zimesamehewa Kodi ya VAT; na
(iii) Madawa na vifaa vya utabibu na huduma za afya zilizoorodheshwa katika para 7 la jedwali la kwanza la misamaha zimesamehewa Kodi ya VAT.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha miongozo na taratibu za usimamizi wa kodi ili kuimarisha biashara na kuvutia wawekezaji, ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved