Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Stella Ikupa Alex

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. STELLA I. ALEX aliuliza: - Je, ni Halmashauri na Manispaa ngapi nchini zinatekeleza ununuzi na ugawaji wa mafuta ya ngozi kwa watu wenye ulemavu wa ngozi?

Supplementary Question 1

MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 tuna idadi ya watu wenye ualbino wapatao 16,000 lakini kutokana na jibu la Serikali inaonesha kwamba watu wenye ualbino ambao wamenufaika na mafuta haya ni 3,389 kwa kipindi cha mwaka 2020 hadi 2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tukumbuke kwamba Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI alishatoa maelekezo kwa Halmashauri hizi kwamba zihakikishe zinanunua na kugawa mafuta haya ya watu wenye ualbino.

Nini kauli ya Serikali kwa Halmashauri ambazo hazitatekeleza takwa hili, na hasa ikizingatiwa kwamba maelekezo yameshatolewa mara nyingi, lakini pia miongozo ipo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili la nyongeza; kwa kuwa sasa hivi tunakwenda kuwa na zoezi hili la sensa, hivyo tunategemea kwamba tutapata idadi halisi ya watu wenye ulemavu, aina za ulemavu na mahali wanapopatikana ama mahali walipo.

Serikali inaonaje sasa ikianza kuyanunua mafuta haya ikawa inayashusha moja kwa moja kwenye vituo vya afya na zahanati, tofauti na utaratibu uliopo sasa ambapo mafuta haya kwa maeneo ambayo yalikuwa yakinunuliwa yalikuwa yakipatikana kwenye Hospitali za Mikoa na Wilaya? Ahsante.

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Stella Alex Ikupa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Stella Ikupa amekuwa mstari wa mbele sana kuhakikisha anawasemea watu wenye ulemavu wakiwemo wenye ulemavu wa ngozi na Serikali ya Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, inawajali na kuwathamini sana watu wote wenye ulemavu na ndiyo maana katika mipango yetu tumekubaliana kwamba kwanza ni maelekezo ya Serikali kwamba Halmashauri zetu zote zinapotenga fedha kwa ajili ya dawa lazima zitenge fedha kwa ajili ya mafuta haya kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa ngozi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba kurudia tena kauli hiyo ya Serikali ambayo ilikwishatolewa kwamba Halmashauri zote zihakikishe zinatenga fedha, miongoni mwa bajeti ya dawa lazima mafuta haya ya watu wenye ualbino yaweze kuwepo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari kwenye bajeti ya mwaka 2022/2023 Halmashauri zote zimefanya utambuzi na kufanya maoteo ya mahitaji ya mafuta hayo na katika mwaka huu tutakuwa na mafuta hayo kwa kiasi kikubwa zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kuhusiana na kusogeza huduma hizi karibu zaidi na watu wenye ulemavu, ni kweli tutakuwa na Sensa ya Watu na Makazi tarehe 23 Agosti, 2022. Niwaombe watu wote wenye ulemavu, pamoja na Watanzania wote, tujitokeze wote ili tuhesabiwe, na hii itasaidia sana Serikali kuwatambua watu wenye ulemavu na kujua mahali walipo na mafuta haya sasa yatasogezwa kwenye vituo vile kwa idadi kulingana na watu wenye ulemavu walipo katika maeneo hayo, ahsante.

Name

Dr. Christina Christopher Mnzava

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. STELLA I. ALEX aliuliza: - Je, ni Halmashauri na Manispaa ngapi nchini zinatekeleza ununuzi na ugawaji wa mafuta ya ngozi kwa watu wenye ulemavu wa ngozi?

Supplementary Question 2

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante; kwa kuwa watu wengi wenye ulemavu wa ngozi hawako kwenye vituo, wengine wako vijijini; je, nini kauli ya Serikali kuhakikisha kwamba hata wale ambao hawko kwenye vituo vya Watoto walio na albinism.

Je, nini mkakati wa Serikali kuwafikia kule waliko kuwapa mafuta?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Christine Mnzava, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba siyo wote wenye ulemavu wa ngozi (ualbino) wapo kwenye vituo vya huduma, kwa maana ya watoto, lakini hapa tunaongelea watoto na watu wazima kupata huduma hii. Sasa utaratibu ambao tutauweka, kwanza tukisogeza huduma hizi za mafuta karibu na zahanati na vituo maana yake wale watu wenye ualbino watajua kwamba mafuta yakiisha watakwenda kwenye zahanati ya karibu zaidi au kwenye kituo cha afya au hospitali ya karibu zaidi. Kwa hiyo, mpango wa Serikali ni kusogeza zaidi upatikanaji wa huduma hii kwenye vituo katika jamii zetu, ahsante.