Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Amina Saleh Athuman Mollel

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. AMINA S. MOLLEL aliuliza:- Masuala ya watu wenye ulemavu kwa kiasi kikubwa yanazungumzwa na kushughulikiwa katika maeneo ya mijini na kusahau maeneo ya pembezoni ambapo kuna watu wa jamii hiyo. Je, Serikali ina mpango gani kuhusu watu wenye ulemavu waishio vijijini ambapo matatizo yao ni mengi na makubwa kulingana na jamii inayowazunguka?

Supplementary Question 1

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na nashukuru pia kwa majibu mazuri kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri katika Wizara husika, nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kutokuwepo kwa takwimu sahihi hasa maeneo ya vijijini kumesababisha kutokuwepo na mipango mahsusi yenye kuleta maendeleo na tija kwa watu wenye ulemavu. Je, Serikali ina mpango gani wa kupata takwimu sahihi za watu wenye ulemavu zitakazosaidia kuwepo kwa mipango mahsusi itakayowasaidia watu wenye ulemavu hasa maeneo haya ya vijijini?
Swali la pili, uwepo wa Sera ya Taifa ya Huduma na Maendeleo kwa Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2004, pamoja na uwepo wa sheria ambayo Naibu Waziri ameitaja Sheria Namba 9 ya huduma kwa watu wenye ulemavu zimesaidiaje kutatua matatizo ya walemavu na Waziri haoni kwamba mfuko wa watu wenye ulemavu ambao ungesimamia Baraza la Watu Wenye Ulemavu kutokutengewa pesa kutasababisha jitihada na mafanikio kwa watu wenye ulemavu yasiwepo?

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake, lakini kwa namna ambavyo amekuwa akitetea na kutushauri hasa katika mambo yanayohusu watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lililoulizwa hapa ni Serikali ina mpango gani kupata takwimu halisi za watu wenye ulemavu. Serikali tayari imekwishaanza mchakato na wameshazindua utaratibu wa kuanzisha kanzidata ambayo itasaidia kupata takwimu sahihi ya watu wenye ulemavu katika maeneo yote ya mijini na vijijini. Lengo kubwa la kanzidata hii itatusaidia pia kuwatambua watu wenye mahitaji hasa watu wenye ulemavu katika maeneo ya vijijini na kushirikiana na Kamati zile ambazo zimeundwa kuanzia ngazi ya Kijiji, Mtaa mpaka Halmashauri ili iwe rahisi kuweza kuwatambua na pia iwe rahisi kuweza kuwasaidia katika kutatua changamoto zao mbalimbali ambazo zinawakabili.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili ameuliza Sera na Sheria Namba 9 ya mwaka 2010 imesaidiaje kutatua changamoto na kero ambazo zinawakabili watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nikiri kwamba uweo wa sheria hii kwanza kabisa imetengeneza msingi na imetengeneza haki za walemavu na sasa sheria hii imekuwa ndiyo sehemu nzuri na platform ya kuweza kusaidia Serikali katika kutimiza matakwa yake mbalimbali ya kusaidia watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma katika Sera ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2004 imezungumza moja ya jambo ambalo Serikali imeshaanza kulifanyia kazi hivi sasa, changamoto kubwa sana ya watu wenye ulemavu ilikuwa ni upatikanaji wa vifaa vyao ambavyo gharama imekuwa kubwa hasa kutokana na kodi ambayo imekuwa ikitozwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukifuatilia katika hotuba ya Waziri wa Fedha ambayo aliwasilisha hapa Bungeni Hotuba Kuu ya Serikali ukurasa wa 50, Mheshimiwa Waziri ameainisha bayana kabisa kwamba Serikali sasa inaandaa utaratibu wa kuondoa kodi na kuweka msamaha wa ushuru katika vifaa vyote ambavyo vinawahusu watu walemavu lengo lake kubwa ni kuhakikisha kwamba huduma hizi zinawafikia kiurahisi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia katika sheria yetu, Sheria Na. 9 ya mwaka 2010 ukiangalia kifungu namba 30 mpaka kifungu namba 34 kimezungumza wazi namna ambavyo watu wenye ulemavu na wenyewe wanapaswa kupata fursa za ajira katika taasisi za umma na taasisi binafsi. Kwa hiyo, naamini kabisa uwepo wa sheria na sera imechangia sana katika maendeleo ya watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Name

Kangi Alphaxard Lugola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwibara

Primary Question

MHE. AMINA S. MOLLEL aliuliza:- Masuala ya watu wenye ulemavu kwa kiasi kikubwa yanazungumzwa na kushughulikiwa katika maeneo ya mijini na kusahau maeneo ya pembezoni ambapo kuna watu wa jamii hiyo. Je, Serikali ina mpango gani kuhusu watu wenye ulemavu waishio vijijini ambapo matatizo yao ni mengi na makubwa kulingana na jamii inayowazunguka?

Supplementary Question 2

MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi kuuliza swali dogo la nyongeza.
Majibu ya Serikali kwa kweli yanawakatisha tamaa walemavu na hasa ambao wako vijijini. Kwa sababu Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba hii Sheria Namba 9 ni tangu mwaka 2010, lakini leo katika majibu yake ya msingi ndiyo anatamka mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba Serikali sasa inawaagiza watendaji waharakishe kuunda Kamati za Walemavu Vijijini.
Je, kama Mheshimiwa Amina Mollel asingeuliza swali hili leo ina maana Serikali haikuwa na mpango wa kuwaagiza watendaji kwa ajili ya uharakishaji wa uundaji wa hizi Kamati za Walemavu kule Vijijini?

Name

Jenista Joackim Mhagama

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Peramiho

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE WALEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwanza kabisa naomba nimshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa katika swali la msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo kweli kwamba Serikali haijaanza kutekeleza Sheria Namba 9 ya mwaka 2010 ambayo inasimamia huduma kwa watu wenye ulemavu. Naomba nikuhakikishie wewe binafsi na Bunge lako Tukufu kwamba haya yote ambayo mnaona yamekuwa yakiendelea, yanayowagusa watu wenye ulemavu katika nchi yetu ya Tanzania ikiwemo upunguzaji wa gharama ya vifaa vyao; ikiwemo namna tofauti ya kuhakikisha kwamba elimu inakuwa inclusive kwa watu wenye ulemavu katika nchi yetu ya Tanzania, ikiwemo namna ya kuunda Mabaraza hayo kwenye maeneo yetu ya Halmashauri zetu ndani ya Serikali za Mitaa. Ni utekelezaji wa sheria hiyo, ninaomba tu niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge mipango yote ipo na imeshaanza kutekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu cha msingi hapa wote kwa pamoja sasa na hasa tunapokaa katika vikao vyetu vya Mabaraza ni kuendelea kuona kwamba yale maagizo ambayo tumeshayaweka na kuyateremsha kwenye Serikali za Mitaa ni kuhakikisha kwamba yanatekelezeka na kama mnaona kuna tatizo mtupe taarifa ili tuweze kusimamia zaidi. Lakini naomba niwathibitishie kwamba sheria hiyo hiyo imeanza kufanya kazi na sisi kama Serikali tumekuwa tukiisimamia na siyo tu tumesubiri swali hili la Mheshimiwa Amina Mollel. Nakushukuru.