Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Florence George Samizi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Primary Question

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI aliuliza: - Je, lini Serikali itakarabati Kituo cha Afya cha Kifura – Muhambwe?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kituo cha Afya cha Kifura ambacho Serikali imekiri kwamba ni chakavu sana kinapokea wagonjwa wa nje 110 hadi 150 kwa siku lakini kinazalisha kinamama 120 mpaka 150 kwa mwezi. Je, kutokana na mzigo wa wagonjwa wengi ulioko katika Kituo hiki chakavu, Serikali haioni sasa iko sababu ya kuharakisha mchakato wa kuleta pesa za ukarabati wa Kituo hiki cha Afya cha Kifura? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; Serikali iliahidi kumalizia ujenzi wa Kituo cha Afya cha Nyaruyoba kupitia ziara ya Mheshimiwa Makamu wa Rais mwaka 2021. Kituo hiki cha Afya cha Nyaruyoba kinahudumia takribani kata tatu ikiwemo Mkabule, Rusohoko na Kigaga iliyoko Kata ya Rugongwe. Je, Serikali haioni iko sababu ya kuharakisha kuleta pesa za kumalizia Kituo hiki cha Afya ambacho kinahudumia takribani kata nne katika Jimbo la Muhambwe? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba nianze tu kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo amefuatilia ahadi hizi za Serikali kuhakikisha kwamba zinakarabati Kituo cha Afya cha Kifura na ni kweli kituo hiki ni chakavu, kina upungufu wa miundombinu na kinahudumia wananchi wengi. Nimhakikishie kwamba katika mpango wa Benki ya Dunia hivi karibuni, hiki ni miongoni mwa vituo ambavyo vimeingizwa na tunaamini fedha zitakwenda kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni kweli kwamba Kituo cha Afya cha Nyaruyoba ni ahadi ya Mheshimiwa Makamu wa Rais nimhakikishie kwamba tayari Serikali inaendelea kutafuta fedha na mapema iwezekanavyo fedha ikipatikana itapelekwa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Kituo hiki cha Afya, ahsante. (Makofi)

Name

Geoffrey Idelphonce Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Masasi Mjini

Primary Question

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI aliuliza: - Je, lini Serikali itakarabati Kituo cha Afya cha Kifura – Muhambwe?

Supplementary Question 2

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwenye Jimbo la Ndanda tuna vituo kwenye Kata ya Ndanda, Kijiji cha Chiroro, Lukuledi, Ngalole, Chikundi pamoja na Namajani. Vituo hivi vimeshakamilika ujenzi wake zaidi ya miaka miwili sasa hivi lakini hata hivyo havijafunguliwa na kuanza kutoa huduma kwa wananchi kwa sababu ya mapungufu madogo madogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba; je, yuko tayari kutoa maelekezo kwa Halmashauri yetu ya Masasi DC ili vituo hivi vikamilishwe na kuanza kutoa huduma kwa wananchi kwani zile shilingi milioni 50 zilizoletwa na Serikali hivi sasa majengo haya yameanza kuchakaa?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecil Mwambe, Mbunge wa Jimbo la Ndanda kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuwapongeza Wananchi wa Jimbo la Ndanda kwa kujenga kutumia nguvu zao lakini Serikali iliwaunga mkono kuwapelekea shilingi milioni 50 kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati hizi na vituo hivi na vimekamilika vitoe huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nitumie fursa hii ya Bunge lako tukufu kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuwaelekeza Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuzingatia maelekezo ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwamba vituo vikikamilika vinabaki hatua ndogo ndogo za ukamilishaji, vifaatiba kwa ajili ya kuanza kutoa huduma. Ni lazima watoe kipaumbele kuhakikisha vinakamilika mapema na vinaanza kuwahudumia wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa Wakurugenzi wote nchi nzima, lakini mahususi nitoe maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi kuhakikisha vituo hivi ambavyo vimetajwa na Mheshimiwa Mbunge wa Ndanda mapema iwezekanavyo ndani ya miezi mitatu tuhakikishe vituo hivi vimekamilishwa na vinaanza kutoa huduma kwa wananchi, ahsante.