Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Vedasto Edgar Ngombale Mwiru
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Kilwa Kaskazini
Primary Question
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE aliuliza:- Serikali ya Awamu ya Tano inakusudia kuifanya Tanzania kuwa ni nchi yenye uchumi wa viwanda, hivyo inahitaji kuwa na uzalishaji wa umeme wa uhakika. Hata hivyo, umeme unaozalishwa kwa kutumia gesi asilia pale Somanga Fungu unakatika mara kwa mara na kusababisha adha kubwa kwa watumiaji:- Je, Serikali inaweza kutuambia wananchi kiini hasa cha ukatikaji huo wa kila siku wa umeme unaozalishwa kutokana na gesi ya Songosongo?
Supplementary Question 1
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Katika jibu lake la msingi Mheshimiwa Waziri anasema kwamba, ndiyo kwanza wameanza ukarabati wa mitambo ile, nilifanya ziara mwezi wa Saba na nikakutana na Meneja na akanieleza kwamba, ukarabati umefanyika, lakini bado kuna tatizo kila inapofika saa tano ya usiku mashine zile hujizima na baada ya saa nane ndiyo huweza kuwaka tena. Nahitaji kufahamu ukweli ni upi, maelezo ya Mheshimiwa Waziri au yale aliyonipa Meneja wa kile kituo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; bado kuna tatizo kubwa na hasa la kiufundi. Sasa Mheshimiwa Naibu Waziri anieleze kwamba, mkandarasi aliyetumika kufanya ukarabati ule ni yule aliyeelekezwa na mtengenezaji wa mashine au hawa wenzetu wa Magomeni? Mheshimiwa Naibu Waziri kama yuko tayari kufuatana nami kwenda kuangalia namna ya kutafuta suluhu ya tatizo lile? Ahsante.
Name
Dr. Medard Matogolo Kalemani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chato
Answer
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nitoe ufafanuzi mzuri wa matatizo ya umeme kule Kusini. Ukweli ni kwamba, umeme Mikoa ya Lindi na Mtwara una matatizo na matatizo ni ya kiufundi. Ilikuwa ni kampuni ya ARTMUS iliyopewa jukumu la kusambaza umeme huko, ilijenga miundombinu ya msongo mdogo wa kilovoti 33; ukizitoa Mtwara ziende mpaka Masasi, Nachingwea, ukweli ni kwamba umeme unakuwa na matatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kinachofanyika sasa hivi ambacho Mheshimiwa Naibu Waziri ameongea ni kweli kwamba, TANESCO inarekebisha hizo njia, zitajengwa sasa badala ya kilovoti 33 ni kilovoti 132 double circuit (njia mbili) za kuleta umeme mwingi zaidi. Kwa hiyo, hiyo kazi nadhani itakamilika mwisho wa mwaka huu, lakini nimemtuma mtu aende Mtwara kwa sababu, Mbunge wa Mtwara aliniuliza, nimemtuma Engineer aende alete jibu kabla ya Jumatano wiki ijayo. Kwa hiyo, jibu kamili mtalipata kama mradi unaendelea vizuri, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili kutatua hili tatizo, kama anavyosema Mheshimiwa, Somanga Fungu, lazima tukiri mitambo ya Somanga Fungu ina matatizo. Siyo Somanga Fungu tu ni kitu ambacho lazima tuwe wakweli tukifanyie kazi, kwa nini mitambo yetu inavyoanza kazi, ikifika miaka miwili tu inakuwa na hitilafu! Hicho kitu ni lazima tukifanyie kazi ni cha kitaalam; Somanga Fungu ilifungwa baada ya miaka miwili ikaleta matatizo. Ule wa Nyakato Mwanza umefungwa baada ya miaka miwili una matatizo! Mtambo wa Ubungo baada ya miaka miwili una matatizo, hivi ni vitu ambavyo lazima tuviongee kwa uwazi kuliko kuvificha, kuna tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Somanga Fungu ukweli ni kwamba, yule na nadhani Mbunge yuko makini sana alikuwa anauliza swali la kututega sisi; ukweli ni kwamba, aliyetengeneza ile mitambo na anayefanya repair sasa hivi ni watu tofauti, huo ukweli lazima tuukubali. Sasa tunachofanya ni kwamba, ukweli wamefanya rapair ya Somanga Fungu hatuna sababu ya kufunga safari kwenda kule kuthibitisha kwa sababu kazi yenyewe haijakamilika. Kwa hiyo, hakuna kujiridhisha, tunajua kazi haijakamilika, kwa hiyo tungoje ikamilike. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la Somanga Fungu kulitatua na Mikoa ya Kusini ni kuingizwa kwenye gridi ya Taifa. Kwa hiyo, fedha zimepatikana na TANESCO wameanza kujenga miundombinu ya msongo mkubwa kutoka Somanga Fungu, kuunganisha na Kinyerezi, tunataka iwe ya kilovoti 400, walikuwa 200 nikasema hapana, tumezowea tunafanya vitu kidogo baada ya muda tena matatizo! Kwa hiyo, watapeleka kilovoti 400 kusudi ule umeme wa Somanga Fungu na wa Mtwara ukiingia Somanga Fungu unaweza kwenda Kinyerezi na nyie mkipata matatizo mnaweza mkapata umeme kutoka kwenye gridi ya Taifa.
Waheshimiwa Wabunge, hili tatizo linatatuliwa tulieni tu, halitachukua muda mrefu. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved