Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Stella Ikupa Alex

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. STELLA I. ALEX aliuliza:- Je, nini mkakati wa Serikali kuajiri wasaidizi kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wenye ulemavu uliozidi?

Supplementary Question 1

MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Spika, naomba muda wako kidogo; tarehe 6 Februari, 2024 Mwananchi Digital ilimwonesha mama ambaye amehamia shuleni, ameacha majukumu yake ya kiuchumi na kijamii ili kuweza kumsaidia mtoto wake awapo shuleni.

Swali la kwanza, je, hakuna kada inayofanana na kada hii ambayo nimeiulizia ambayo kwa sasa Serikali wakati inajiandaa kuipata kada husika inaweza ikaitumia ili kuwasaidia watoto hawa wawapo shuleni?

Swali la pili, je, ni nini mkakati wa Serikali kuipata sasa hii kada husika? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ni kweli miongoni mwa wanafunzi wenye ulemavu wapo wanafunzi wenye ulemavu ambao umewaathiri kwa kiasi kikubwa na kushindwa kufanya baadhi ya majukumu ambayo kimsingi wanahitaji usaidizi wa karibu zaidi. Ndiyo maana Serikali imeweka utaratibu kuwa na vyuo vya Walimu, mafunzo maalum kwa wanafunzi wenye ulemavu, ambao kwa sasa wanatumika kuwasaidia wanafunzi hao katika mazingira hayo.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tunahitaji kuwa na kada maalum ambayo inaweza ikawasaidia kwa ukaribu zaidi wanafunzi wenye mahitaji makubwa ya usaidizi katika mazingira ya shule. Kwa hivyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inalifanyia kazi hilo, inatambua umuhimu wao, lakini tuna mkakati wa kuhakikisha kwamba tunaendelea kuwatumia pia Maafisa Ustawi wa Jamii katika maeneo hayo pamoja na Walimu wenye mafunzo maalum ili wanafunzi wenye ulemavu waweze kupata huduma bora zaidi.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, nikiongezea hapo ni kwamba, kwa kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulika na masuala ya watu wenye ulemavu sambamba na Wizara ya Elimu tumekwishaanza kufanyia kazi suala hilo la kuwa na kada maalum kwa ajili ya kutoa msaada kwa watu wenye ulemavu kwenye shule.

Mheshimiwa Spika, pia ukiangalia kwa upande wa vyuo vikuu University of Dar es Salaam wamekwishaanza. Kwa sasa tuko mbioni na tumeshapata bajeti maalum ya Mfuko wa Watu wenye Ulemavu ambao utasaidia katika kutekeleza jukumu hili. Kwa hiyo Serikali ipo katika hatua nzuri.