Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Mwantumu Mzamili Zodo
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MWANTUMU M. ZODO aliuliza: - Je, kuna mpango gani wa kuvisaidia vikundi vya uzalishaji mali vikiwemo vya ufugaji ambavyo wanawake wamehamasika ili wafuge kwa tija?
Supplementary Question 1
MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Swali la kwanza; kwa kuwa mchakato huu wa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 umesitishwa ni mrefu sasa, na kwa kuwa akina mama bado wanahangaika na mikopo ya kausha damu huko mitaani. Je, ni lini sasa Serikali itaanza tena zoezi hili la utoaji mikopo ili kuondoa adha kwa akina mama wa Mkoa wa Tanga na Watanzania kwa ujumla? (Makofi)
Swali la pili; kwa kuwa Halmashauri huwa zinatenga mikopo ya asilimia 10 kutoka kwenye mapato ya ndani kila robo ya mwaka, na kwa kuwa mchakato huu pia umesimama kwa muda mrefu. Je, Serikali inahakikisha Halmashauri zinaendelea kutenga fedha za asilimia 10 ili wakianza mchakato huu akina mama waweze kupatiwa mikopo? Ahsante.
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zodo. Swali lake la kwanza juu ya mchakato kusitishwa, ni kweli mchakato huu ulisitishwa baada ya Mheshimiwa Rais kupokea ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kuonesha kwamba kuna fedha nyingi ambazo zilikuwa hazijarejeshwa za mikopo hii, hivyo maelekezo ya Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassah yalikuwa, yafanyike mapitio sasa ya namna ya mikopo hii inavyotolewa.
Mheshimiwa Spika, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa aliunda timu, ambayo ilifanya mapitio ya namna ya mikopo inavyotolewa, timu ile ikawasilisha taarifa kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI na sasa mapendekezo yale yamewasilishwa kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hivi tunavyozungumza Waziri wa nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, amekumbushia kwa Mheshimiwa Rais ili jambo hili liweze kurudi sasa na kuanza utekelezaji wake. Kama kuna Sheria ya kubadilika iletwe mbele ya Bunge hapa ili sheria hizo ziweze kubadilika.
Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili la fedha hizi je bado hutengwa. Ndiyo, fedha hizi bado zinatengwa kwa sababu, kwa mujibu wa Sheria ile ya Fedha ya Serikali za Mitaa, fedha hii iko ring fenced na inaendelea kutengwa. Pale mikopo hii itakapoanza kutolewa tena basi fedha hii ipo, nawatoa mashaka hayo. Ahsante sana.
Name
Shally Josepha Raymond
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MWANTUMU M. ZODO aliuliza: - Je, kuna mpango gani wa kuvisaidia vikundi vya uzalishaji mali vikiwemo vya ufugaji ambavyo wanawake wamehamasika ili wafuge kwa tija?
Supplementary Question 2
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, kitu pekee cha kuwatoa wanawake wa Tanzania waendelee haraka, ni mifugo midogomidogo ikiwemo kuku, mbuzi na ng’ombe. Wanawake wa Kilimanjaro wanasubiri sana msaada huo kutoka Serikalini.
Je, ni lini sasa ile mitamba niliyoahidiwa hapa Bungeni itatolewa? (Makofi)
Name
Jenista Joackim Mhagama
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Peramiho
Answer
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika, wakati tunasoma Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2023/2024, Wizara ya Mifugo ilitoa maelezo ya namna gani tunakwenda kuboresha sekta ya mifugo kwa ujumla. Kwa hiyo, kwa sababu Mheshimiwa Shally ameuliza swali hili ambalo ni specific kwenye eneo hilo la mitamba, tunaomba tulichukue na Mheshimiwa Waziri wa Mifugo atapatiwa taarifa hii na atampatia majibu Mheshimiwa Shally Raymond. (makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, ahsante sana kwa majibu yako kwa maswali ya Waheshimiwa Wabunge. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Nchi, majibu yatatolewa kwa Mheshimiwa Shally bila kuwa swali la msingi kama nimekuelewa vizuri. Mtampelekea wenyewe majibu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika, ndiyo kwa sababu hapa limeletwa kama swali la nyongeza na siyo swali la msingi.
SPIKA: Ni sawa. Mimi naweza kuagiza mambo mawili, moja, ninyi mumpelekee ama lije kama swali la msingi. Kwa hiyo kwa maelezo yako kama nimekuelewa vizuri ni kwamba badala ya kuja kama swali la msingi, ninyi Serikali mtampelekea majibu Mheshimiwa Shally Raymond.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika, tuko tayari kupata Mwongozo wa Kiti chako.
SPIKA: Sawa. Mpelekeeni majibu, kama hakuyapata atauliza tena.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved