Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Grace Victor Tendega

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:- Je, lini Serikali itamalizia ujenzi wa Kituo cha Afya cha Migoli katika Jimbo la Ismani?

Supplementary Question 1

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na jengo la OPD kukamilika, jengo la wazazi pamoja na upasuaji bado hayajakamilika. Akina mama pamoja na wananchi wanapata adha kubwa kwenda katika hospitali ya wilaya ama kwenda Hospitali ya Rufaa ya Iringa Mjini: Je, lini Serikali itakamilisha majengo haya ili wananchi hao wapate huduma?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, hadi sasa tumebakiza miezi mitano ili tukamilishe mwaka wa fedha na asilimia 100 aliyosema italetwa, bado haijaletwa: Ni lini sasa hiyo fedha asilimia 100 itapelekwa?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Grace Victor Tendega, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nimejibu katika majibu yangu ya msingi kwamba ni kweli jengo la OPD limekamilika, jengo la wazazi na upasuaji halijakamilika, na Serikali katika mwaka huu wa fedha imetenga shilingi milioni 100 kwa ajili ya kukamilisha majengo hayo.

Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia na vile vile nampongeza Mheshimiwa Lukuvi asubuhi ameniambia shilingi milioni 100 tayari imeshapokelewa katika halmashauri yake. Kwa hiyo, nawapongeza kwa ushirikiano huo mzuri wa kuwahudumia wananchi wa Wilaya ya Iringa.

Mheshimiwa Spika, pili, kuhusiana na shilingi milioni 100, ndiyo hiyo ambayo tumeambiwa imeshafika. Kwa hiyo, tutafuatilia utekelezaji ili jengo likamilike mapema wananchi waanze kupata huduma, ahsante.

Name

Jackson Gedion Kiswaga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Primary Question

MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:- Je, lini Serikali itamalizia ujenzi wa Kituo cha Afya cha Migoli katika Jimbo la Ismani?

Supplementary Question 2

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali hii ya Awamu ya Sita inatekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi na Katibu Mkuu Daniel Chongolo ambaye ni mstaafu, alivyopita Jimbo la Kalenga aliahidi kuleta shilingi milioni 500 kujenga Kituo cha Afya Kata ya Lyamgungwe ndani ya miezi mitatu: Je, Serikali itatekeleza lini agizo hili ambalo ni halali kabisa? Ahsante sana.

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jackson Kiswaga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali yetu inatekeleza kwa ufanisi mkubwa sana Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na maeneo yote ambayo Serikali imeahidi kujenga vituo vya afya baada ya kujiridhisha na vigezo, tutakwenda kupeleka fedha kwa awamu kwa ajili ya kujenga vituo hivyo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Kiswaga kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI, itakwenda kufanya tathmini eneo hilo kuona kama linakidhi vigezo na kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya, ahsante.

Name

Edwin Enosy Swalle

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Primary Question

MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:- Je, lini Serikali itamalizia ujenzi wa Kituo cha Afya cha Migoli katika Jimbo la Ismani?

Supplementary Question 3

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kata ya Mtwango tumejenga kituo cha afya kwa mapato ya ndani, pia tumejenga jengo kwa ajili ya mortuary, lakini hatuna jokofu. Kwa kuwa nimemsikia Mheshimiwa Waziri kwamba Kibaha Vijijini kuna jokofu na hawana jengo la mortuary; je, Serikali iko tayari kuchukua hili jokofu kwenda pale Mtwango? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Edwin Enosy Swalle, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza niwapongeze wananchi wa Jimbo la Lupembe na Mheshimiwa Mbunge kwa kujenga Kituo cha Afya cha Mtwango kwa mapato ya ndani. Pia nimhakikishie tu kwamba tunafahamu kwamba kuna jengo la kuhifadhia maiti halina mashine kwa maana ya jokofu la mortuary na tayari Serikali hii imeshapeleka fedha zaidi bilioni 150 kwenye halmashauri zote kote nchini ndani ya miezi mitatu, minne iliyopita kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vya kipaumbele yakiwemo majokofu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutatoa kipaumbele kupata jokofu katika Kituo cha Afya cha Mtwango, ahsante. (Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, swali lilikuwa, kuna jokofu mahali halina chumba, kwa hiyo, limehifadhiwa, halafu kuna mahali kuna chumba ambapo hakuna jokofu. Haliwezi kutolewa hili jokofu ambalo kwa sasa limehifadhiwa halihifadhi maiti likapelekwa kwenye chumba ambacho kipo tayari? (Makofi)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nakushukuru; jokofu hili lilipelekwa na Bohari ya Dawa kwa maana ya MSD na tulishapata taarifa na tayari taratibu za kulihamisha kupeleka sehemu ambayo tayari jengo limekamilika zinaendelea. Baada ya Kibaha kukamilisha jengo watapelekewa tena jokofu lao. Kwa hiyo, naomba nisilete commitment kwamba tunapeleka Lupembe, lakini tunapeleka sehemu ambayo tayari MSD wameshafanya tathmini na wameona uhitaji kwa sasa ili lisikae bila kufanya kazi, ahsante.

Name

Daniel Baran Sillo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Babati Vijijini

Primary Question

MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:- Je, lini Serikali itamalizia ujenzi wa Kituo cha Afya cha Migoli katika Jimbo la Ismani?

Supplementary Question 4

MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Serikali ilipeleka shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Gidas: Je, ni lini itamalizia awamu ya pili ya shilingi milioni 250 ili kukamilisha majengo yale?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Daniel Sillo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kweli Serikali ilishapeleka shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Gidas na inahitaji shilingi milioni 250 ya awamu ya pili kwa ajili ya ukamilishaji wa majengo yaliyobaki katika hicho kituo cha afya.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote ambao walipata fedha za awamu ya kwanza ya shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya, kwamba Serikali imeshaweka mkakati katika mwaka ujao wa fedha kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha majengo kwa awamu ya pili. Ahsante.

Name

Issa Ally Mchungahela

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lulindi

Primary Question

MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:- Je, lini Serikali itamalizia ujenzi wa Kituo cha Afya cha Migoli katika Jimbo la Ismani?

Supplementary Question 5

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Makamu wa Rais alipokuja Chiungutwa alitoa ahadi ya shilingi milioni 100 kwa ajili ya kumalizia Kituo cha Afya cha Chiungutwa na pia shilingi milioni 100 pia kwa Kituo cha Afya cha…

SPIKA: Mheshimiwa swali la nyongeza huwa ni moja.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, lini…

SPIKA: Subiri, subiri. Kwanza huwezi kwenda mbili; pili, kwa sababu ni swali la nyongeza huwezi kuweka maswali mawili katika swali moja. Chagua kimojawapo kati ya hivyo umwulize Mheshimiwa Naibu Waziri ili akujibu.

MHE. ISSA ALLY MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, ni lini pesa hizi shilingi milioni 100 zitakwenda kwenye Kituo cha Afya cha Chiungutwa?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Mchungahela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Mheshimiwa Makamu wa Rais aliahidi shilingi milioni 100 kwa ajili ya ukamilishaji wa Kituo cha Afya cha Chiungutwa na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba fedha hiyo imeshatengwa kwenye bajeti ya mwaka huu 2023/2024 na fedha zitakapopatikana zitapelekwa katika kituo hiki kwa ajili ya ujenzi, ahsante.

Name

Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Primary Question

MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:- Je, lini Serikali itamalizia ujenzi wa Kituo cha Afya cha Migoli katika Jimbo la Ismani?

Supplementary Question 6

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Pale kwenye kituo chetu cha Bweri pamoja na Makoko ni vituo ambavyo sasa vimekaa muda mrefu pasipo kumaliziwa; je, ni lini Serikali italeta fedha ili tuweze kumalizia hivyo vituo wananchi waweze kupata huduma bora?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vedastus Manyinyi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya cha Bweri na Makoko ambavyo havijakamilika, kwanza utaratibu ambao tumeweka Serikalini ni kwamba vituo vyote ambavyo havijakamilika tunafanya tathmini ya kujua havijakamilika kwa sababu gani; je, ni matumizi mabaya ya fedha? Kama ni matumizi mabaya ya fedha tunachukua hatua kwa watumishi waliohusika.

Mheshimiwa Spika, pili, kama ni inatokana na inflation, tumeelekeza halmashauri kutenga fedha kwa awamu, badala ya kusubiri fedha za Serikali kuu pekee kwenda kukamilisha majengo hayo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nitumie fursa hii kwanza nichukue hoja hii kwamba tutafanya tathmini kujiridhisha, na pili, nimwelekeze Mkurugenzi wa Halmashauri hii ya Manispaa ya Musoma kuhakikisha wanaanza kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha miundombinu iliyobaki ili vituo vianze kutoa huduma kwa wananchi, ahsante.

Name

Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Primary Question

MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:- Je, lini Serikali itamalizia ujenzi wa Kituo cha Afya cha Migoli katika Jimbo la Ismani?

Supplementary Question 7

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Kwa kuwa Serikali ilituahidi kutupatia fedha kwa ajili ya kujenga Kituo chetu cha Afya cha Choma; je, ni lini fedha hizo zitafika kwenye Kituo cha Afya cha Choma? Ahsante.

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Gulamali, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali ilishaahidi kupeleka fedha shilingi milioni 500 kwenye Kituo cha Afya cha Choma na tayari nimeshawasiliana na Mheshimiwa Mbunge mara kadhaa kwamba imeshaingizwa kwenye orodha ya fedha za Benki ya Dunia ambazo tunatarajia wakati wowote mwezi wa Pili au wa Tatu zitatoka kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha afya. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi hiyo imezingatiwa na Serikali itatekeleza, ahsante.