Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Constantine John Kanyasu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita Mjini
Primary Question
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza: - Je, lini Wananchi wa Nyambalembo, Magema, Katoma, Mizingamo, Katumai na Nyakabale wanaoishi eneo la leseni ya GGM watalipwa fidia?
Supplementary Question 1
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Natumia fursa hii kwanza kumshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, Mheshimiwa Waziri wa Madini na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya kwa ushirikiano mkubwa ambao tumeufanya hadi kufikia hatua hii.
Mheshimiwa Spika, mwekezaji anatumia upungufu uliomo kwenye Sheria yetu ya Madini na Sheria ya Ardhi kuendelea kuchelewesha au kukwamisha mazungumzo yanayoendelea; na kwa sababu hiyo kuendelea kuwatesa wananchi ambao wamekaa kwenye mgogoro huu kwa zaidi ya miaka 22.
Mheshimiwa Spika, sasa, kwa nini wakati tunaendelea kubishana, Serikali isichukue jukumu la kulipa fidia yenyewe, halafu ikaendelea kujadiliana upungufu wa kisheria unaoendelea kuwepo eneo hilo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; naipongeza sana Serikali kwa tathmini ya awali inayoendelea kule Samina. Eneo linalofanyiwa tathmini linafanana kabisa na maeneo nane yaliyobaki. Kwa nini sheria ile ile ambayo imetumika kufanya tathmini kwa wananchi wa Samina isitumike kwenye maeneo mengine ambayo sasa hivi Serikali inasema bado inafanya mazungumzo? (Makofi)
Name
Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Longido
Answer
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Kanyasu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Serikali kulipa fidia, napenda kumjulisha kwamba, Serikali inapotoa leseni kwa mwekezaji, yule mwenye leseni ndiye anakuwa na Haki Madini pale na ndiye mmiliki wa madini. Hivyo, siyo tena Serikali yenye wajibu wa kulipa fidia ya aina yoyote. Kwa hiyo, kwa maridhiano kati ya mwenye leseni na wananchi na viongozi wa eneo lile, akikubali kuwalipa fidia kama anavyoomba kwamba fidia ilipwe hata kabla hajaweza kuhamishwa, hilo tunawaachia wao kupitia mfumo ulioko wa maridhiano na mahusiano mema na jamii.
Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la pili, kwamba kwa nini Serikali isilipe? Majibu ni kama hayo tu kama nilivyotangulia kusema, kwamba Serikali siyo mmiliki tena wa yale madini. Amepewa Haki ya madini yule aliyepewa leseni na ndiye mwenye dhamana ya kufanya kazi na wananchi ili waweze kulipa.
Mheshimiwa Spika, pia nitumie fursa hii kumjulisha Mheshimiwa Mbunge na nampongeza kwa namna anavyofuatilia swali hili kwamba, tulishaunda Kamati kati ya Wizara, Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya ya Geita ambayo inaendelea na mazungumzo ya kutafuta namna bora ya kuwafidia wale watu ambao ni lazima wahame, kama hao wa Samina ambao karibu hatua za mwisho zinafikiwa na hawa wengine ambao walisema hawatayahitaji maeneno yao lakini itafutwe namna bora ya kuwashika mkono au kwa ajili ya usumbufu ili waweze kuendelea na maisha yao.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved