Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Prof. Patrick Alois Ndakidemi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Vijijini
Primary Question
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa msaada wa kitaalamu kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu ili kuongeza idadi ya samaki?
Supplementary Question 1
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na nina maswali mawili ya nyongeza. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwapatia Wavuvi wa Bwawa la Nyumba ya Mungu zana na nyenzo za uvuvi kama vile nyavu, boti na vizimba, kama ilivyofanya hivi karibuni kwa wenzao wa Lake Victoria?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; uvuvi haramu ni chanzo kikubwa cha kuzorotesha uchumi wa Samaki; na Maafisa Uvuvi wa hapa nchini na hata kule Nyumba ya Mungu, wameweka mkazo kwenye kuwakamata wavuvi na kuwapiga faini badala ya kutoa elimu endelevu ya namna bora ya kufanya uvuvi: Je, Serikali haioni umuhimu wa kuchukua hatua kupambana na hali hii? (Makofi)
Name
Alexander Pastory Mnyeti
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Misungwi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nianze na hili la kwanza. Kwanza ugawaji wa nyenzo za uvuvi kama boti, nyavu na kadhalika, kama ambavyo Mheshimiwa Rais alifanya juzi kule Mwanza, Ziwa Victoria, hii ni fursa kwa Watanzania wote kwenye maziwa na mabwawa mbalimbali, wanaruhusiwa kuchukua nyenzo hizi kwa njia ya kukopa kupitia TADB, benki yetu ya kilimo ambapo ukiwasilisha andiko lako vizuri kwa kupitia wataalamu wetu, unaweza kupata ushauri na baadaye ukakopeshwa nyenzo hizo ukafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hii ni fursa kwa Watanzania wote ikiwemo wavuvi wa Bwawa la Nyumba ya Mungu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, kwanza nikupongeze sana kwa ufuatiliaji na namna ambavyo unaendelea kufuatilia. Umekuwa msumbufu sana kwenye hili. Tunakupongeza kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri. Kwa kweli tupo tayari kukupa ushirikiano ili wavuvi wako waweze kupata nyenzo hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni kweli kwamba Maafisa Uvuvi kazi yao ni kuhakikisha wanasimamia shughuli za uvuvi kwenye maeneo yao pamoja na kutoa elimu kwa wavuvi wetu. Natoa wito na rai kwa Maafisa Uvuvi wote nchini kuhakikisha kwamba wanajikiza zaidi kwenye kutoa elimu na kusimamia shughuli za uvuvi na siyo kujigeuza kuwa Maafisa Masuuli na Maafisa wa Mapato, kukatisha ushuru na mambo mengine ambayo hayawahusu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunatoa wito kwa Maafisa wote kwamba sasa wajielekeze kwenye kazi yao ya msingi ambayo wanatakiwa kufanya kwenye maeneo yao huko wanakofanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved