Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Conchesta Leonce Rwamlaza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza: - Je, suala la vifo vitokanavyo na utoaji mimba usio salama lina ukubwa na madhara gani nchini?

Supplementary Question 1

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru; ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo TBC Radio ambacho ni chombo kikuu cha habari cha Tanzania, walikuwa wanaendesha mjadala kuhusu jambo hili. Wao wamesema ni asilimia 19, ninyi mnasema ni asilimia kumi. Naona mkasawazishe hapo kwa sababu nyote mnatoa taarifa kwa jamii.

Je, Serikali imejipangaje kupunguza hii asilimia kumi ya vifo vitokanavyo na kutoa mimba kusiko salama?

Swali la pili; Serikali iliridhia na kusaini Mkataba wa Maputo wa Nyongeza ambao mkataba huu ulikuwa unatetea haki za wanawake na afya pamoja na uzazi salama. Makubaliano hayo yalilenga kwamba mimba zitolewe zile ambazo zinapatikana kwa kubakwa, mimba ambazo zinatokana na mashambulio ya ngono na zile mimba maharimu yaani zile mimba ambazo zinatokana na ndugu. Je, Serikali sasa haioni ni wakati muafaka wakuweka makubaliano hayo katika sheria za nchi yetu ili kuwasaidia wamama ambao wanapata mimba za aina hii waweze kuzitoa kwa usalama bila kuhatarisha maisha yao? (Makofi)

Name

Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, kwamba eneo hilo ni muhimu lizungumziwe ili kuendelea kutoa hamasa kwamba kuna tatizo na kuna watu wanapoteza maisha kwa sababu ya mimba zisizo salama. Mheshimiwa Mbunge umesema hili la TBC inategemeana ni nani alikuwa anaongea na source yake ya data ni wapi, lakini sisi tuna source ambayo inakubalika kwa sababu tunajua duniani kwa mwaka wanawake milioni 42, mimba zisizo salama ni milioni 20 na kidunia ni asilimia 13 ambayo wanapata haya matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tutafuatilia TBC wametoa source wapi lakini data ambazo tunazo kwa kupitia mifumo ya hospitali zetu za Serikali na private inaonyesha hili ambalo tumelisema hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu tunashushaje sasa hiyo, tutaendelea kutoa hamasa kuhakikisha kwamba tunashirikiana na Wizara ya Elimu, tunashirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii na nyinyi wenyewe Wabunge kila mmoja awe balozi wa kuonyesha kwamba watoto wetu kuna wakati muafaka wa kupata mimba, kuna wakati muafaka wa kuanza hayo mambo ambayo yanasababisha hayo matokeo. Wote tukiboresha na tukahamasisha maadili katika jamii yetu ni mojawapo ya sehemu yakushusha mimba kama hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili unazungumzia kwamba mikataba ya kidunia lakini pia kuruhusu sasa ili watu waweze kwenda kutoa mimba, sheria zetu ziruhusu. Hii inahitaji mchakato mkubwa kwa sababu inagusa Wizara mbalimbali lakini inagusa imani mbalimbali za watu na mambo mengine. Ninakuomba tupeni muda tuendelee kuchakata ili tusije tukajaribu kuzuia tatizo kwa namna nyingine tukazalisha tatizo lingine. Mimi ninachokuomba Serikali ipo committed na elimu itaendelea kutolewa na wewe uwe balozi wetu kwenye eneo lako. (Makofi)