Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Faida Mohammed Bakar
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR aliuliza:- Askari wa Wilaya ya Mkoani katika Mkoa wa Kusini Pemba wanakabiliwa na tatizo la uchache wa nyumba za kuishi na ubovu wa ofisi zao:- Je, ni lini Serikali itawajengea Askari nyumba za kuishi na ofisi za kisasa katika kituo cha Mkoani na Kengeja – Pemba?
Supplementary Question 1
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri Masauni huwa ana kawaida ya kutembelea mikoa mbalimbali ili kuona matatizo ama changamoto za askari na hata Pemba alifika na yeye mwenyewe alijionea tatizo sugu lililopo katika Mkoa wa Kusini Pemba, Wilaya ya Mkoani kituo cha Mkoani na kituo cha Kengeja, zile ofisi zinavuja. Je, Serikali itakubaliana nami kwamba hela hizi zilizopangwa na nyumba hizo zitakazojengwa zianzie katika ofisi za kule Mkoa wa Kusini Pemba Wilaya ya Mkoani na kule Kengeja ili kuwaondoshea askari hao usumbufu mkubwa wanaopata? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa kutokana na tatizo kubwa la ukosefu wa nyumba za askari hasa kule Pemba; askari wengi wanakaa katika nyumba za kupanga ambazo zipo mbali sana na vituo vyao vya kazi. Je, Serikali ipo tayari kuwaondoshea tatizo hili askari hao kwa kuwakopesha vifaa vya usafiri lakini vifaa hivyo viwe na riba nafuu ili kuwaondoshea tatizo hilo? Ahsante sana.
Name
William Tate Olenasha
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ngorongoro
Answer
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kama alivyosema kwamba Kusini Pemba kuna changamoto kubwa kama nilivyosema kwamba nchi nzima kuna changamoto ya nyumba za polisi kiasi kwamba kuna upungufu mkubwa. Katika kutimiza azma ile ya Serikali ya kuhakikisha kwamba askari wetu wanapata nyumba nchi nzima tutaanzia kwenye maeneo yale ambayo tunafikiri kuna tatizo zaidi na Kusini Pemba ni moja kati ya maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na kujenga nyumba mpya kama nilivyosema katika majibu ya swali la awali ni kwamba Serikali vilevile iko kwenye utaratibu wa kukarabati nyumba kwa kuanzia na yale maeneo ambayo yana shida zaidi. Kwa hiyo, nimwahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Kusini Pemba ni moja kati ya maeneo ambayo yameonekana yana changamoto kubwa na mpango huo wa kufanya ukarabati pamoja na ujenzi vilevile utahusisha kule.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kutoa mikopo ya riba nafuu kwa ajili ya kununulia vifaa naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni moja kati ya masuala ambayo yanafanyiwa kazi ili askari wetu hasa wale ambao hawana nyumba waweze kufika kazini bila matatizo yoyote.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved