Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Justin Lazaro Nyamoga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilolo
Primary Question
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA K.n.y. MHE. KASALALI E. MAGENI aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga Shule ya Sekondari Kata ya Malya, Kitongoji cha Mwashilibwa ili kuongeza huduma Vijiji vya Mwitemba, Talaga na Kitunga?
Supplementary Question 1
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, swali la kwanza ni kwamba ni kweli kuna utaratibu wa shule za SEQUIP kujengwa na mojawapo ikiwa ni katika Jimbo la Mheshimiwa Kasalali, je, ni lini kwa mwaka huu wa fedha shule hizo zitaanza kujengwa kwenye jimbo hili na majimbo mengine? (Makofi)
Swali la pili, kuna shule za SEQUIP za awamu ya kwanza ambazo hazikuwa zimekamilika, je, ni lini Serikali itapeleka fedha ili kukamilisha shule hizo kwenye majimbo yote ikiwemo Jimbo la Sumve na Jimbo la Kilolo? (Makofi)
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitafuta fedha na akapata fedha jumla ya shilingi trilioni 1.2 katika mradi tunaouita Mradi wa SEQUIP ambao lengo lake ni kuongeza shule zetu za sekondari kwenye kata na kuhakikisha zinafika, tunaongeza idadi ya shule kwa ajili ya kupunguza kwanza umbali wa wanafunzi kusafiri ili kufika kwenye shule, lakini pia kupunguza msongamano katika baadhi ya maeneo ambayo kuna msongamano kwenye shule hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa lengo la Serikali na lengo la Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha anaboresha sekta ya elimu na hasa elimu hii ya shule za sekondari na shule za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Mbunge ameuliza kwamba ni lini awamu hii au mwaka huu fedha zitatolewa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa shule hizi katika mwaka huu wa fedha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali imeshafanya uhakiki wa maeneo yote yaliyoainishwa kwa ajili ya ujenzi wa shule hizi za kata katika mwaka huu na ninamhakikishia, wakati wowote fedha zitatolewa kwa ajili ya kuhakikisha tunatekeleza mradi huu kwa kadiri vile tulivyokuwa tumepanga kwa maana ya awamu ya mwaka wa fedha 2023/2024.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, Mheshimiwa Mbunge ametaka kufahamu kwamba zile shule za awamu ya nyuma ambazo hazikukamilika, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kuhakikisha inakamilisha shule hizo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali ilishaanza kutoa fedha na itahakikisha inapeleka fedha ili kukamilisha ujenzi wa miundombinu muhimu ya shule hizi za kata ili wanafunzi waweze kuanza kuzitumia. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved