Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Anne Kilango Malecela

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Same Mashariki

Primary Question

MHE. ANNE K. MALECELA K.n.y. MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:- Je, nini mkakati wa Serikali wa kumaliza tatizo la matundu ya vyoo, viti, meza na madawati katika Halmashauri zote nchini?

Supplementary Question 1

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kupata majibu ya Serikali, sasa naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Halmashauri ya Tarime ina mapato makubwa ya ndani na chanzo cha mapato hayo ni wananchi wenyewe: Je, Serikali iko tayari kutoa maelekezo kwa Halmashauri ya Tarime iweze kuondoa changamoto za matundu ya vyoo, viti, meza na madawati?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Same inafahamu vema kwamba nimefanya jitihada kubwa kutengeneza madawati kwenye shule za msingi zaidi ya madawati 500: Je, Serikali hamwezi kuwaelekeza Halmashauri ya Wilaya ya Same ikachukua hatua nayo ya kutengeneza madawati sasa hasa katika shule za Kata za Lugulu, Mtii, Vuje na Bombo? (Makofi)

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la kwanza la Mheshimiwa Mbunge, ukweli ni kwamba shule ni mali ya Mamlaka za Serikali za Mitaa na shule zipo chini ya Mamlaka za Serikali za Mitaa. Pia wajibu wa kutunza na kusimamia shule hizi uko chini ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Kwa hiyo, tafsiri yake ni kwamba, ununuzi wa madawati, viti, ujenzi wa madarasa na miundombinu mingine ni wajibu wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia bajeti za maendeleo. Huo ndiyo msingi wa D by D.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya Serikali Kuu kimsingi ni miradi ya nyongeza kwa maana ni complimentary. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kukumbushia maelekezo ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kwamba, wahakikishe wanafanya tathmini ya miundombinu na samani na kutenga kwenye bajeti za maendeleo kwenye mapato ya ndani ya Halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, maelekezo hayo ya Mheshimiwa Waziri yanaenda pia kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa jitihada binafsi za kuhakikisha kwamba ananunua madawati haya kwa ajili ya kupeleka kwenye shule zake. Jitihada hizi ni nzuri na zinafaa kuigwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kukumbushia maelekezo ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote zilizopo nchini kuhakikisha kwamba wanatenga fedha kwenye mapato yao ya ndani, kwenye bajeti ya maendeleo kuhakikisha kwamba wanatumia fedha hizi kwenda kununua madawati haya na pia kuendeleza miundombinu mingine kama kujenga vyoo. Hilo ni jukumu lao kwa mujibu wa D by D. Kwa hiyo, naomba nikumbushie hilo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same Mashariki. (Makofi)