Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Maimuna Ahmad Pathan
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MAIMUNA A. PATHAN aliuliza:- Je, ni lini wananchi wa Nachingwea ambao mashamba yao yalitwaliwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege watalipwa fidia?
Supplementary Question 1
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je, Serikali kwa kuchelewa kulipa pesa ya wananchi zaidi ya miaka mitano sasa, haioni kwamba imerudisha nyuma maendeleo ya wananchi hao kwa kukosa sehemu za kulima? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, naomba kauli thabiti ya Serikali, je, ni lini wananchi hawa wa Nachingwea wataipata pesa yao?
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba tuna viwanja takribani 15 nchi nzima ambavyo tunafanya uhakiki na hatua mbalimbali za utwaaji wa ardhi ili kuweza kufanya maendelezo makubwa ya viwanja vya ndege. Hilo moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ningependa kujibu maswali yake kwa umoja wake. Tunafahamu umuhimu mkubwa wa Uwanja wa Ndege wa Nachingwea, siyo tu kwa ajili ya korosho, madini ambayo yamegundulika na LNG, lakini pia kwa ajili ya mazao kama ufuta na kadhalika. Hivyo basi, Serikali kwa maana ya kutoa kauli thabiti, inaliarifu Bunge lako Tukufu kwamba tunao mpango wa kujenga uwanja huu na ndiyo maana sasa tulifanya uhakiki kwa wale wananchi 116. Awali ilikuwa tuwalipe shilingi bilioni 3.5, lakini baada ya kufanya uhakiki na ongezeko la gharama ya mazao, tukapata ni shilingi bilioni 3.4 – 3.5. Hii yote ni dhamira ya Serikali katika kuona kwamba wananchi hao wanakamilishiwa mradi wao. Hivyo basi, tunaendelea na taratibu mbalimbali za Serikalini, tukikamilisha tutaweza kuanza ujenzi huo. Ahsante.
Name
Vedastus Mathayo Manyinyi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Musoma Mjini
Primary Question
MHE. MAIMUNA A. PATHAN aliuliza:- Je, ni lini wananchi wa Nachingwea ambao mashamba yao yalitwaliwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege watalipwa fidia?
Supplementary Question 2
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Uwanja wa Ndege wa Musoma, watu wanadai fidia sasa ni zaidi ya miaka mitatu ambayo ni fedha isiyopungua bilioni 3.9. Hakuna biashara inayoendelea kwa kuwa wanategemea wapate fidia ili waendelee na maisha yao. Je, ni lini sasa hawa watu watalipwa fidia ili waweze kuendelea kuondoka pale? (Makofi)
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu madai mbalimbali ya Uwanja wa Ndege wa Musoma na hivi juzi Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuwa hapo na alitoa maelekezo kwa sisi wasaidizi wake Serikalini tukamilishe haraka iwezekanavyo. Tupo kwenye hatua mbalimbali hususan za mwisho kwa wenzetu Wizara ya Fedha. Mara watakapokamilisha tutakwenda kulipa mara moja, kwa sababu tunafahamu umuhimu wa Uwanja wa Ndege wa Musoma kwa maana ya madini pamoja na vitu mbalimbali ambavyo viko pale. Ahsante.
Name
Saashisha Elinikyo Mafuwe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Primary Question
MHE. MAIMUNA A. PATHAN aliuliza:- Je, ni lini wananchi wa Nachingwea ambao mashamba yao yalitwaliwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege watalipwa fidia?
Supplementary Question 3
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naishukuru Serikali kwa kutupa shilingi bilioni 11 kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi wale waliokuwa Uwanja wa Ndege wa KIA ili waweze kuondoka. Hata hivyo, kumejitokeza changamoto ndogondogo, baadhi ya wananchi kufanyiwa tathmini ndogo tofauti na hali halisi na baadhi yao kusahaulika. Changamoto hiyo Mheshimiwa Makamu wa Rais aliiagiza Wizara ya Uchukuzi iifanyie kazi. Je, ni lini sasa Serikali itamaliza changamoto hii ikiwa ni pamoja na kurudia tathmini kwa wale ambao walifanyiwa tathmini ambayo siyo sahihi? Ahsante.
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, tulifanya uhakiki kwa baadhi ya waliolalamika kwamba walipunjwa malipo yao katika Uwanja wa KIA, lakini kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge ameleta hoja hiyo, tuko tayari kama kuna malalamiko mengine, kuyapitia upya ili waweze kupata stahiki zao. (Makofi)
Name
Anatropia Lwehikila Theonest
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MAIMUNA A. PATHAN aliuliza:- Je, ni lini wananchi wa Nachingwea ambao mashamba yao yalitwaliwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege watalipwa fidia?
Supplementary Question 4
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Wananchi wa Wilaya ya Kyerwa na Karagwe ambao kwa muda mrefu waliambiwa wasiendeleze maeneo ambayo yako karibu na barabara ambazo ni Barabara kutokea Omugakorongo kwenda mpaka Murongo zikiathiri Kata za Kibale, Bugara na maeneo mengine. Je, ni lini sasa fidia hizo zitatoka ili wapishe hayo maeneo ya uendelezaji wa barabara kwa sababu wameshindwa kuendelea na maendeleo au kufanya chochote kwa sababu ni issue ya muda mrefu? (Makofi)
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye maelezo wakati namjibu mwenye swali la msingi, tupo kwenye hatua mbalimbali za utwaaji wa ardhi, tuna viwanja 15 nchini kote. Pamoja na hoja aliyoisema Mheshimiwa Mbunge, tunaichukua tuifanyie tathmini na tutaona namna bora ya kuonana naye ili kuweza kuzifanyia kazi hoja za wananchi hao.
Name
Cecilia Daniel Paresso
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MAIMUNA A. PATHAN aliuliza:- Je, ni lini wananchi wa Nachingwea ambao mashamba yao yalitwaliwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege watalipwa fidia?
Supplementary Question 5
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini wananchi wanaopisha upanuzi wa Uwanja wa Manyara watalipwa fidia?
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa hatua tuliyopo ni uandaaji wa taarifa ya uthamini, mara tutakapokamilisha, tutawalipa fidia.
Name
Mussa Azzan Zungu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ilala
Primary Question
MHE. MAIMUNA A. PATHAN aliuliza:- Je, ni lini wananchi wa Nachingwea ambao mashamba yao yalitwaliwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege watalipwa fidia?
Supplementary Question 6
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri, kuna fidia ambayo inadaiwa Kipunguni, walipisha Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam. Hawa wananchi wanalalamika sana na tulishawahi kwenda pale kwa Waziri wa Fedha, lakini bado fidia yao haijalipwa. Je, ni lini sasa watalipwa?
Name
Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Magharibi
Answer
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa. Ni kweli kama ulivyosema kuna fidia inadaiwa na wananchi walishapewa mwongozo huo na Serikali na ni kweli nilishafika pale. Kitu kilichofanyika ni kwamba…
NAIBU SPIKA: Tulikwenda wote mimi, wewe na Mheshimiwa Mbunge Bonnah pale.
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Naibu Spika, tulifika na Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Segerea, Mheshimiwa Bonnah amekuwa akifuatilia ofisini mara kwa mara kuhusu jambo hili. Kilichotokea ni kwamba ilikuja kugundulika kuna baadhi ya maeneo ambayo wananchi walikuwa wamepewa maeneo mbadala, yalikuwemo kwenye sehemu ya madai na kuna baadhi ambao walikuwa wamehitaji fidia zaidi. Kwa hiyo kilichofanyika, tulipeleka timu iweze kuwianisha, iweze ku-align zile numbers na jambo hilo lilishafanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunachofanya, tunatafuta fedha ndani ya kipindi hiki cha mwaka wa fedha unaoendelea ili tuweze kuanza kufanya malipo. Tutaanza na wale ambao madai yao yamehakikiwa na hayana vikwazo vyovyote…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri, ahsante…
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kulifuatilia kwa karibu sana jambo hili na sisi Serikali tutafanya hilo kwa ajili ya kuienzi kazi yake. (Makofi)