Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Mrisho Mashaka Gambo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arusha Mjini
Primary Question
MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapandishia mishahara wafanyakazi?
Supplementary Question 1
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali hasa kwa kuzingatia kwamba wafanyakazi wamepata ahadi ya kupata neno la kuhusiana na mishahara yao wakati wowote Mheshimiwa Rais atakapoamua kuongea na umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimechanganyikiwa kidogo, ukiangalia wakati Serikali inaongeza mishahara ya watumishi wa umma kutoka shilingi 300,000 mpaka shilingi 370,000, kwenye sekta ya binafsi bado hali yao ni duni sana. Utaangalia kwa mfano tunaambiwa kwenye zile sekta 13, kwenye hoteli kubwa za kitalii, mishahara kima cha chini shilingi 300,000. Mheshimiwa Rais kafanya jitihada kubwa, Royal Tour imekuja, watalii wameongezeka lakini bado mishahara ipo chini.
MWENYEKITI: Swali Mheshimiwa Gambo.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka kujua je, Serikali kwa kupitia Wizara ya Utumishi na Utawala Bora, ina mpango gani wa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuhakikisha kwamba mishahara ya kima cha chini inakuwa angalau shilingi 370,000 pia na kwa sekta binafsi?
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Utumishi, kwa majibu yake mazuri ambayo ameyatoa kwenye swali lililoulizwa na Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, napenda kumpa taarifa Mheshimiwa Mbunge kupitia Bunge lako hili Tukufu kwamba, tayari Serikali Novemba, mwaka 2022 ilitoa mwongozo wa kima cha chini cha mshahara cha sekta binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mwongozo ule kutoka, Shirikisho la Vyama vya Waajiri (ATE), walitoa secular ya Disemba ambayo ilianza kutekelezwa Januari mwaka 2023, lakini mawazo yake tunayachukua na mchango wake tunauchukua na hivi sasa tayari kuna timu ambayo imeshaundwa na imeanza kazi mwezi Aprili kwa ajili ya kufanya mapitio tena ya kima cha chini cha mshahara katika sekta binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya timu hiyo kukamilisha mapitio hayo, basi tutaleta hapa Bungeni ili Waheshimiwa Wabunge wote waweze kufahamu. Timu hiyo inahusisha utatu kwa maana ya wataalam kutoka Serikalini, kutoka TUCTA vilevile kutoka ATE ambapo ikikamilisha kazi tutaleta majibu hayo. (Makofi)
Name
Jafari Chege Wambura
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rorya
Primary Question
MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapandishia mishahara wafanyakazi?
Supplementary Question 2
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Watumishi zaidi ya 850 wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya hawakulipwa mshahara wao wa mwezi wa tatu. Jambo hili limepelekea pia huduma ya Bima ya Afya kwa watumishi hao kufungwa, nataka kupata kauli ya Serikali juu ya watumishi hawa, nini tatizo?
Name
Ridhiwani Jakaya Kikwete
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chalinze
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na hiyo changamoto iliyotokea katika Halmashauri ya Rorya, ilitokana na ukweli kwamba Serikali katika kupitia mfumo mpya wa upimaji wa utendaji ndani ya watumishi wa umma, wako baadhi ya watu ambao walionekana kwamba taarifa zao za mwenendo wa utendaji kila siku hazikuletwa katika ofisi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara yako ilitoa maagizo kwa Halmashauri ya Rorya ili waweze kutupatia taarifa za watumishi wote hao. Nakiri mbele ya Bunge lako kwamba taarifa zilizotoka katika Ofisi ya Mkurugenzi Rorya, zilileta taarifa ya kwamba wako wafanyakazi zaidi ya 700 ambao walikuwa hawajajiorodhesha katika jedwali lile la utendaji (PEPMIS) kama ambavyo imeelekezwa na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwongozo wa Serikali ulieleza kwamba watumishi wote ambao hawakujiorodhesha wanatakiwa wafungiwe mishahara yao. Taratibu zilifanyika lakini baada ya kufanyia utaratibu tena kuangalia, tumegundua kwamba yako baadhi ya maeneo kulikuwa na changamoto ikiwemo taarifa ambazo zimeletwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi yako ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, imekwishalifanyia kazi jambo hilo na imeshapeleka ombi jipya kwa ajili ya utatuzi wa hiyo kero iliyoingia ya mishahara ambayo kupitia Wizara ya Fedha, tunategemea kwamba tutapata fedha hizo na ili jambo litakwisha ndani ya wiki hii. Kwa hiyo, nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba asiwe na wasiwasi, watumishi wake watarudishiwa payroll zao na mambo yataendelea vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, angalizo langu kwa Halmashauri zote, watumishi wote walio chini ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa, wajiorodheshe na wajiunge na mfumo huu ili tuendelee kupimana katika utekelezaji wa majukumu kama ambavyo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved