Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Ally Anyigulile Jumbe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyela
Primary Question
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE aliuliza:- Je, mchakato wa kuwalipa waliokuwa Wafanyakazi wa Kiwira Coal Mine umefikia hatua gani?
Supplementary Question 1
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ni miaka 15 sasa tangu mchakato huu umeanza na katika mchakato huu kuna wananchi wengine mpaka sasa hivi wameshapoteza maisha. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuharakisha hili zoezi ili hawa wananchi walipwe fedha yao? Wananchi hawa wanatia huruma sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Naishukuru sana Serikali kwa kuanzisha kiwanda bora kabisa pale STAMICO ambacho kwa sasa kitatoa makaa ya kupikia kwa kutumia makaa ya mawe.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuuliza swali. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha makaa ya mawe na makaa haya ya kupikia ambayo ni bora zaidi yanawafikia wananchi wa Rungwe, Kyela na Ileje? (Makofi)
Name
Anthony Peter Mavunde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Dodoma mjini
Answer
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Ally kwa maswali yake mazuri. Ninakiri kwamba, kweli deni hili la wafanyakazi hawa limechukua muda mrefu. Pia sisi kama Wizara, hata kupitia ziara ya Kamati ambayo ilitutembelea miezi michache iliyopita, tulipewa jukumu la kulifuatilia Hazina. Namwahidi kwamba, baada ya kujibu maswali hapa niko tayari kuungana naye tuendelee kufuatilia deni hili ili liweze kulipwa haraka iwezekanavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la pili, kuhusu makaa ya mawe ambayo yanachakatwa Kiwira kwa mtambo ambao uliwekwa na Serikali, namjulisha kwamba, kwanza mtambo huo umekamilika na tunavyoongea mzabuni yuko site kwa ajili ya commissioning na uzalishaji wa majaribio umeanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango uliowekwa na Serikali ili kusambaza makaa haya kupitia Shirika letu la STAMICO ni kwamba, wazabuni, wasambazaji (distributers), walikuwa wanatafutwa nchi nzima na mpaka sasa hivi wamepatikana wasambazaji 52. Pia nitumie fursa hii kuwaasa wananchi wa Kyela waunde vikundi, wapeleke maombi ya kuwa mawakala wa kusambaza makaa hayo ambayo yanaitwa Rafiki Briquettes ili waweze kutumia makaa hayo ambayo ni safi na salama na itanusuru misitu yetu na mazingira kuharibiwa na wakata mkaa. Maana yake ni kwamba haya makaa sasa ni mbadala wa kuharibu mazingira. Ahsante sana. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved