Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Ally Anyigulile Jumbe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyela
Primary Question
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE K.n.y. MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza: - Je, lini Serikali itapeleka watumishi wa Kada ya Afya na Elimu katika Wilaya ya Chunya?
Supplementary Question 1
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza tuishukuru Serikali kwa juhudi kubwa inayofanya kuajiri watumishi hasa wa kada ya afya na walimu.
Mheshimiwa Spika, shule nyingi za pembezoni katika Wilaya ya Chunya kwenye kata za Lualaje, Ifumbo, Mafyeko na Kambi Katoto zimekosa walimu pamoja na watumishi wa afya. Je, Serikali haioni sasa ni wakati sahihi wa kuhakikisha inafanya msawazisho ili walimu walioko mijini na walioko kule wafanane?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; ni lini Serikali itaandaa mpango maalum wa kufanya sensa ya kuhakikisha tunakuwa na takwimu za walimu na watumishi wa afya walio mijini na walio vijijini?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsate sana. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Ally Jumbe, Mbunge wa Kyela kwa kazi nzuri na kubwa anayowafanyia wananchi wa Jimbo la Kyela. Nianze kwa kumpa uhakika kwamba, kwanza tunatambua kuna baadhi ya shule zilizoko pembezoni mwa miji au halmashauri zina upungufu mkubwa sana wa watumishi zikiwemo hizo za maeneo ya Kambi Katoto, Mafyeko na maeneo mengine ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja.
Mheshimiwa Spika, tayari tumeshaweka mpango wa kuhakikisha maeneo yale ambayo yana upungufu mkubwa zaidi wa watumishi wanapelekwa na ndiyo maana kwenye mfumo wa ajira wa sasa, ni mfumo kwanza wa kieletroniki pia kila anayeomba ajira analazimika kuomba kwenye maeneo ambayo yameainishwa na ule mfumo automatically unaweka nafasi nyingi zaidi kwenye shule, halmashauri au mikoa ambayo ina upungufu mkubwa zaidi wa watumishi. Kwa hiyo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hilo tutalifanyia kazi ili tupunguze gap la watumishi katika shule hizo.
Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusiana na kufanya sensa ya walimu walioko mijini na vijijini. Tayari tulishafanya hivyo miaka miwili iliyopita na tunafahamu uwiano wa walimu vijijini na watumishi wa afya vijijini na mijini. Mpango uliopo sasa kwanza ni kuhakikisha kwamba kipaumbele cha ajira kinakwenda kwenye halmashauri za vijijini zaidi. Pili, tunazuia uhamisho kutoka vijijini kwenda mijini kwenye majiji, manispaa ili kuhakikisha kwamba tuna-balance uwepo wa watumishi katika vijiji na katika miji, ahsante.
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri ahsante sana kwa majibu yako kwa maswali ya Waheshimiwa Wabunge. Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji Mbunge wa Mwera sasa aulize swali lake.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved