Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Fatma Hassan Toufiq
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza:- Je, ni Wanawake wangapi wanaomiliki Migodi ya Madini nchini?
Supplementary Question 1
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa majibu ya Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, idadi ya wanawake milioni tatu ni ndogo sana. Je, ni nini mkakati wa Serikali wa kuhamasisha wanawake wengi zaidi waweze kushiriki katika sekta hii?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; Mkoa wa Dodoma ni miongoni mwa mikoa ambayo ina madini mengi ya kimkakati. Je, ni nini mkakati wa Serikali wa kuifanya Dodoma kuwa ni miongoni mwa vivutio vya wawekezaji wa madini ili kusudi wananchi wake waweze kufaidika? Ahsante.
Name
Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Longido
Answer
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Fatma Toufiq kwa maswali yake mazuri sana ambayo yanalenga kuwahamasisha wanawake waingie katika sekta hii ya madini yenye kuleta tija kwa Taifa. Kwanza, kwa swali lake hili la kwanza, sisi Wizara ya Madini kupitia Taasisi ya STAMICO na Tume ya Madini tumekuwa na mkakati mahususi wa kuhamasisha jamii nzima ya Watanzania wakiwemo wanawake kwa kutoa elimu na kuendelea kutenga maeneo mahsusi, kwa ajili ya vikundi vya wachimbaji wakiwemo wanawake nchini. Kwa hiyo, naendelea kumwomba awahamasishe wanawake wa Mkoa wa Dodoma nao wajiunge katika vikundi na waje Wizarani kwa sababu, tunaendelea kutenga maeneo kwa ajili yao.
Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la pili, mkakati tulionao sisi kama Wizara kwa sasa hivi, kwanza ni Mheshimiwa Rais ameendelea kututuma nje katika makongamano ya kimataifa kwenda kutangaza fursa za uwekezaji katika sekta hii ya madini mkakati. Tumeendelea kuongezewa fedha, kwa ajili ya kufanya utafiti katika maeneo mbalimbali nchini kubaini madini haya kwa kutumia sayansi na tekenolojia ya kisasa kama jiofizikia kupitia ule mfumo wa ndege zisizo na rubani na helikopta.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi tuna mpango mkakati wa kuanza high resolution airborne survey katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Mkoa wa Dodoma ili kubaini madini hayo. Tayari Mkoa wa Dodoma unajulikana kwamba una lithium na shaba kwa wingi na tafiti hizi zinavyoendelea kufanyika ndivyo tutakavyozidi kubaini maeneo ili Watanzania wote wajihusishe na biashara hii yenye tija.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved