Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Sylivia Francis Sigula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. SYLVIA F. SIGULA aliuliza: - Je, Wizara ya Viwanda na Biashara imejipanga vipi kuendana na kasi ya uboreshaji Bandari ya Dar es Salaam?
Supplementary Question 1
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali na naishukuru kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, bado kuna changamoto kubwa ya ucheleweshwaji wa mizigo bandarini. Kuna wakati unakuta zaidi ya meli 20 ziko zinasubiri kushusha mzigo. Je, Wizara hii kwa kuwa inahusika na wafanyabiashara, haioni kama kuna haja ya kukaa na TPA na mwekezaji kuona namna nzuri ya kutatua hii changamoto ya ucheleweshaji wa mizigo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, tunaipongeza sana Serikali kwa uboreshaji wa Bandari. Ukanda wa Ziwa Tanganyika tunaona kuna Bandari ya Kalema, tunaishukuru sana Serikali, lakini Wizara hii haioni kuna haja ya kuwa na mpango maalumu wa kuwaandaa wafanyabiashara vijana, wakulima na wavuvi ili kuitumia Bandari hii ya Kalema kufanya biashara ili kuingiza pato kwa Taifa na pato la mtu mmoja mmoja? (Makofi)
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Answer
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la dada yangu Mheshimiwa Sylvia Francis, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli hivi karibuni baada ya kupata uteuzi, niliamua kukaa na wafanyabiashara kubaini changamoto zao. Miongoni mwa jambo ambalo walibainisha ni suala hilo kwamba mizigo sasa hivi inachelewa. Hata hivyo, Serikali hivi sasa ina mchakato mpana, hili ni jambo la mpito tu, siyo muda mrefu watu wataona kuna transformation kubwa sana inafanyika na shughuli za usafirishaji mtaona zimeboreka sana katika eneo hili.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, hata juzi nilipotembelea Bandari ya Tanga, wengine wanaanza kusema sasa hivi kuna mabadiliko makubwa yanapitia katika Bandari ya Tanga. Kwa hiyo, naomba kuwahakikishia Watanzania kwamba kazi kubwa inayofanywa na Wizara ya Uchukuzi na Serikali kwa ujumla, siyo muda mrefu mtaona mapinduzi makubwa katika suala zima la usafirishaji wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, lakini katika suala zima la Kalema kwamba ni jinsi gani tutahamasisha vijana kuletewa utaratibu mzuri, ni jukumu letu hili. Naomba niwaombe Watanzania kwamba, hivi karibuni tumeamua sasa kuja na mpango mkubwa sana na hasa mpango huu utahusisha makundi mbalimbali ikiwemo makundi ya vijana. Kwanza, suala zima la kuweka programu kwanza ya viwanda, lakini kuhakikisha kurahisisha mchakato wa kusafirisha mizigo maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, naomba niwahakikishie Watanzania, hili jambo tutalibeba kwa nguvu zote na muda siyo mrefu sana mtaona tunakuja na kazi kubwa sana ya kuwasaidia Watanzania. Lengo letu ni kwamba tufanye reform katika maeneo mbalimbali ambayo itawasaidia Watanzania katika viwanda na halikadhalika katika biashara na hasa katika hii milango yetu ya bandari tulizokuwanazo za baharini na katika maziwa yetu tuliyokuwanayo. Ahsante sana. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved