Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Bakar Hamad Bakar
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
House of Representatives
Primary Question
MHE. BAKAR HAMAD BAKAR aliuliza:- Je, fedha kiasi gani imepatikana Zanzibar kwa miaka mitatu iliyopita kupitia Mifuko ya Kimataifa ya Mazingira na mabadiliko ya tabianchi?
Supplementary Question 1
MHE. BAKAR HAMAD BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini nina maswali mawili. Swali la kwanza; kwa kuwa athari hizi za mazingira na mabadiliko ya tabianchi zinaendelea kuathiri maeneo mbalimbali ya nchi yetu na kwa kuwa upatikanaji wa fedha hizi kupitia mifuko ya nje ya Kikanda na ya Kimataifa bado ni mdogo. Je, ni mkakati upi wa Serikali kuhakikisha kwamba wanapanua wigo zaidi wa upatikanaji wa fedha hizi za mashirika haya ya nje?
Mheshimiwa Naibu Spika, pili nilitaka kujua; je, Serikali sasa haioni ipo haja ya kuweka utaratibu maalum kwa maana ya formula maalum sasa ya ugawaji wa fedha hizi zinazopatikana kwenye mashirika haya kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara kuwe kama formula maalum? Ninakushukuru sana. (Makofi)
Name
Khamis Hamza Khamis
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bakar kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru na kumpongeza sana kwa juhudi zake za kuona namna ambavyo mabadiliko ya tabianchi yanapata sura nyingine kwa maana kwamba tunatatua hizo changamoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo jitihada za Serikali ambazo zimefanywa na bado tunaendelea kuzifanya kuhakikisha kwamba tunaongeza fedha kwenye huu Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi. Kwanza kuna maandiko mbalimbali ambayo tayari tumeshaandika. Tuna jumla ya maandiko takribani 13 ambayo yote yanakwenda kuomba fedha kwa ajili ya kupambana dhidi ya athari kubwa ya mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, tumeshakaa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira pamoja na Sekretarieti za Mifuko inayoshughulika na kutoa fedha hii Mifuko ya Kimataifa kama ambavyo nimeitaja hapa ili lengo na madhumuni kuweza kupata fedha zitakazotusaidia. Tunapokaa nao mara nyingi huwa tunawaambia kwamba nchi zilizoendelea lazima zisaidie nchi zinazoendelea katika kukabiliana na hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine hivi ninavyoongea tayari Kamati ya Fedha ya Kudumu inayoshugulikia masuala ya mabadiliko ya tabianchi kuna kikao kinaendelea Arusha Mheshimiwa Makamu wa Rais alifungua jana. Yote hiyo ni namna bora na njia za kuomba fedha kwa ajili ya kupambana dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa swali la pili; fedha hizi zinapokuja kutoka kwa wahisani huwa zinakwenda pande zote mbili za Muungano na ndio maana tayari ipo miradi iliyofanywa Zanzibar na ipo miradi iliyofanywa kwa upande wa bara. Ipo miradi Kaskazini A na Kaskazini B, Unguja, ipo miradi Wete na Micheweni kwa pande wa Pemba, lakini ipo miradi ya kujenga kuta kwa upande wa Sipwese, Pemba na upande wa Mikindani Bara. Kwa hiyo miradi hii fedha zinapokuja zinanufaisha pande zote mbili za Muungano, nakushukuru.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved