Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Maimuna Salum Mtanda
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Newala Vijijini
Primary Question
MHE. MAIMUNA S. MTANDA K.n.y MHE. TOUFIQ SALIM TURKY aliuliza:- Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha Watanzania wanashiriki Kongamano la Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Wafugaji mwaka 2027?
Supplementary Question 1
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapongeza Serikali kwa majibu mazuri ambayo wameyatoa lakini nataka kufahamu tu kwamba, yapo maeneo mengi katika nchi yetu ambayo yanafaa sana kwa ufugaji wa nyuki. Ninashukuru wamesema wanaanza mikakati ya kuelimisha Watanzania, lakini naomba niulize; swali la kwanza; ni upi sasa mkakati ambao Serikali imejiwekea ili wale wananchi ambao wanaishi kule vijijini wapate kwa uhakika elimu hii ili ilete manufaa kwa wafugaji wa nyuki wanaoishi vijijini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, Mheshimiwa Waziri anaweza kuongozana nami kwenda katika Jimbo la Newala Vijijini ili aone namna ambavyo mazingira yetu ni mazuri kwa ufugaji wa nyuki na kuleta hamasa kwa wananchi wa Newala Vijijini? Nakushukuru (Makofi)
Name
Dunstan Luka Kitandula
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maimuna, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tumekuwa na mipango mbalimbali ya kutoa elimu kwa wananchi na kama mnavyofahamu kwenye kila Halmashauri tunao Maafisa Nyuki. Kwa hiyo, tumekuwa tukiwajengea uwezo ili waweze kutoa elimu hiyo. Vilevile, kupitia makongamano ambayo tumekuwa tukiyaandaa tumekuwa tukitoa elimu kwa wananchi na pale ambapo kuna vikundi ambavyo vinahitaji kupatiwa elimu, tumeweza kuwasaidia Maafisa Nyuki waliopo kwenye Halmashauri zetu kuweza kutoa elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninatoa wito kwa wananchi kujiingiza kwa nguvu kubwa katika ufugaji wa nyuki, kwa sababu biashara ya asali na bidhaa zinazoambatana nazo ni kubwa na hivi karibuni Serikali imefanya jambo kubwa. Tumeweza kupata soko kubwa kule Nchini China ambalo kwa mwaka wanahitaji tani 38,000,000. Kwa hiyo, hii ni fursa kwetu sasa kuweza kuchangamkia soko hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali la pili, nipo tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge kwenda Newala kuona jinsi ambavyo tunaweza kushirikiana, kuhamasisha ufugaji wa nyuki na biashara hii katika eneo hilo.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved