Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Bernadeta Kasabago Mushashu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. BERNADETA K. MUSHASHU aliuliza:- Je, lini Serikali italipa madeni ya Wazabuni wanaotoa huduma za vyakula kwenye shule mbalimbali tangu Mwaka 2023 hadi 2024? (Makofi)
Supplementary Question 1
MHE. BERNADETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; fedha inayotengwa kumlisha mwanafunzi kwa siku ambayo ni shilingi 1,500 na zaidi kidogo haitoshi kuweza kumpa milo mitatu, kwa maana ya mlo kamili (balanced diet). Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza hicho kiasi ili kusudi kiweze kulingana na hali halisi ya maisha? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na kiasi ambacho kilishalipwa, lakini madeni ya wazabuni wa vyakula mashuleni bado ni makubwa na mengine bado yako kwenye halmashauri, hayajafika hata Wizarani. Je, Serikali mna mpango gani wa kuhakikisha kwamba, sasa wanaweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba, hayo madeni yanalipwa kila mwezi ili yasiendelee kurundikana kule? (Makofi)
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kumpa taarifa Mheshimiwa Mbunge ambaye ameuliza maswali mazuri kabisa haya kwamba, kiwango cha fedha, kwa ajili ya kununua chakula cha wanafunzi katika shule kimepandishwa, kimeboreshwa kutoka shilingi 1,500 kwa mwanafunzi mmoja mpaka shilingi 2,000. Kwa hiyo, Serikali itakuwa inahakikisha inafanya mapitio ya gharama hii ili kuweza kuiboresha zaidi kwa kadri muda unavyozidi kwenda na kwa kadri bajeti inavyoruhusu.
Mheshimiwa Spika, pia, Ofisi ya Rais, TAMISEMI ikishirikiana na Wizara ya Fedha itaendelea kuhakikisha kwamba, fedha zote zile ambazo zinakuwa zimetengwa zinatolewa zote kulingana na idadi ya wanafunzi wa bweni walioko katika shule zetu hizi. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali imefanya mapitio ya gharama hizo na itaendelea kufanya mapitio zaidi, ili kuendelea kuboresha kiwango.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, Serikali imeendelea kuhakikisha kwamba, inalipa wazabuni. Kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya msingi kwamba, katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 mpaka 2022/2023, Serikali tayari imelipa wazabuni wa chakula shuleni kiasi cha shilingi bilioni 26.3. Kwa muktadha wa swali la Mheshimiwa Mbunge, naomba nichukue nafasi hii, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kutoa maagizo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zote ambazo zina shule za bweni wafanye uhakiki wa madeni yote ya wazabuni wa chakula na waweze kuyawasilisha Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ili na sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI tuweze kuyawasilisha Wizara ya Fedha, kwa ajili ya taratibu za malipo.
Name
Mwanaisha Ng'anzi Ulenge
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. BERNADETA K. MUSHASHU aliuliza:- Je, lini Serikali italipa madeni ya Wazabuni wanaotoa huduma za vyakula kwenye shule mbalimbali tangu Mwaka 2023 hadi 2024? (Makofi)
Supplementary Question 2
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Shule nyingi za Sekondari Mkoani Tanga zina maeneo makubwa yanayofaa kwa kilimo ambayo yangesaidia kupata chakula cha mchana kwa wanafunzi. Je, ni lini Serikali itatoa waraka maalum kwa walimu wa Mkoani Tanga, ili maeneo hayo yatumike vizuri, kwa ajili ya chakula cha mchana kwa wanafunzi? (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Mwanaisha Ulenge, nani anayepaswa kulima kati ya wanafunzi na walimu ili niwe nimeelewa swali lako vizuri?
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, swali la msingi la kwenye hili swali Namba 43 linazungumzia chakula ambacho...
SPIKA: Hilo limeeleweka, yaani muktadha wa swali lako, umesema walimu waelekezwe ili yale maeneo yatumike vizuri; kwa maana ya kutafuta wakulima wa kulima? Ama yale maeneo walime walimu ama walime wanafunzi?
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, vyovyote iwavyo, lakini maeneo yatumike vizuri. Yanakuwa ni kama vile sehemu ya elimu ya kujitegemea, lakini pia, shule ziwe na miradi ili kuepusha huu mzigo wa Serikali kuwalipa wazabuni. (Makofi)
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa lishe na hasa katika ustawi wa wanafunzi wetu. Kwa hiyo, kwa muktadha wa swali la Mheshimiwa Mbunge, naomba nichukue nafasi hii kuendelea kuwahamasisha Wakuu wa Shule waweze kuwa wabunifu, kuanzisha vibustani vidogo vya matunda, mbogamboga na mazao madogo ili waweze kuchangia katika lishe za wanafunzi wetu.
Mheshimiwa Spika, nadhani Mheshimiwa Mbunge dhamira yake ilikuwa ni kuhakikisha kwamba, shule zetu hizi na zenyewe kwenye maeneo yao wanaweza kuwa wabunifu na kuanzisha vimiradi vidogo ambavyo vitasaidia katika lishe za watoto ambazo ni muhimu sana katika makuzi yao katika kupata afya ambayo itawawezesha kupokea masomo vizuri.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved