Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Conchesta Leonce Rwamlaza
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza:- Je, lini Serikali itaanzisha Maabara ya kupima Sampuli za Magonjwa ya Mifugo Mkoani Kagera?
Supplementary Question 1
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Mkoa wa Kagera umewahi kuwa na maabara kubwa na nzuri chini ya Mradi wa KALIDEP na baadaye KADADET. Miradi hii ilipokufa na maabara hiyo ikafa. Ni kwa nini Serikali haikuendeleza maabara hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mkoa wa kagera licha ya ukubwa wake lakini kuna mifugo mingi na kuna ugumu katika kupeleka sampuli kwa sababu ya umbali pia ukosefu wa wataalam, wakati mwingine wa dharura hulazimika madkatari kutoka Mwanza kuja kuchukua sampuli kutoka Mkoa wa Kagera. Je, ni lini Serikali itakuwa na mpango wa kuhakikisha kwamba hii Wizara ya Mifugo inakuwa na wataalam wa kutosha?
Name
Alexander Pastory Mnyeti
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Misungwi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na hili la kwanza ambalo Mheshimiwa Mbunge anataka kujua kwa nini Serikali haikuendeleza hizi maabara? Ni kweli maabara hizi zilikuwepo katika maeneo mbalimbali ndani ya nchi yetu, hususan Mkoa wa kagera kulikuwa na maabara, na hii ni kwa sababu ya wingi wa mifugo iliyoko katika Mkoa wetu wa Kagera. Tunatambua na kuwapongeza sana wananchi wa Mkoa wa Kagera kuwa wafugaji wazuri na maabara ilikuwepo na kama nilivyosema katika jibu la msingi kwamba, Serikali inayo mkakati wa kufufua maabara zote zilizokuwa zimekufa katika maeneo yetu mbalimbali ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa, kwa sababu maabara hizo zimekufa, wananchi na wafugaji wanashauriwa kupeleka sampuli zao katika Mkoa wa Mwanza ambako ndiyo kuna maabara kubwa katika kanda ya ziwa. Maabara hiyo imekuwa ikifanya vizuri na ina wataalam wa kutosha na kwa bahati nzuri sana wataalam wetu wako tayari kusafiri kuwafuata wafugaji kokote wanakopatikana, lakini hii haiondoi mpango wa Serikali wa kufufua maabara zetu zilizokuwepo katika mikoa yetu ikiwemo pamoja na Mkoa wa Kagera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, mpango wa kuwa na wataalam wengi ni mpango madhubuti wa Serikali chini ya Mheshimiwa Rais, na ameshatoa maelekezo tuendelee kutengeneza wataalam wa mifugo ambao watatusaidia kutoa elimu kwa wafugaji wetu katika maeneo mbalimbali ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali kupitia vyuo mbalimbali ambavyo viko ndani ya nchi yetu ikiwemo Chuo Kikuu cha Sokoine na vyuo vingine vidogo vidogo ambavyo vinatoa kwa level ya certificate, diploma na advance diploma tunaendelea kutengeneza wataalam wa mifugo ambao watasaidia kutoa elimu kwa wafugaji wetu ili mfugaji anapofanya shughuli za ufugaji aweze kupata tija katika shughuli hiyo aliyoifanya, ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved