Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Primary Question
MHE. MWITA M. WAITARA K.n.y. MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa nyumba za walimu wa Sekondari nchini na kukarabati zilizochakaa?
Supplementary Question 1
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi, naomba nitumie nafasi hii kutoa pole kwa kijana wangu aliyepata ajali katika Waitara Cup kule Sirari na namshukuru Mungu kwamba wahuni wote na shetani wameshindwa na Mungu ameshinda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili ya nyongeza kwa Serikali; swali la kwanza. Serikali ipo tayari kuleta takwimu za maboma ya nyumba za walimu msingi na sekondari nchi nzima kwenye majimbo yote ambayo wananchi wameweka nguvu zao kuyajenga na yameishia kwenye lenta na kuonyesha mkakati namna ambayo watakamilisha maboma hayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Halmashauri yangu ya Tarime DC ina mapato makubwa. Serikali ipo tayari kutoa maelekeza mahususi kukamilisha maboma yote ambayo wananchi wangu wamechangia nguvukazi ili wapate nguvu kuendelea kuchangia maboma mengine baada ya kukamilisha yale ambayo wameshiriki kuyajenga? Ahsante.
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake haya yenye tija. Kuhusiana na swali lake la kwanza, Serikali tayari imeshafanya tathmini ya kubaini ni maboma mangapi kwenye sekta ya elimu pamoja na sekta ya afya ambayo yamejengwa kwa nguvu za wananchi na tayari tathmini imekamilika na Serikali inafanya taratibu za kuhakikisha fedha inapatikana ili kuweza kuunga mkono jitihada zile za wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali la takwimu Mheshimiwa Mbunge tunaweza tukawasiliana nikakupatia lakini tayari Serikali ilishafanya tathmini kubaini idadi ya mabama na kiasi gani cha fedha kinahitajika kwa ajili ya kukamilisha maboma hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili; Halmashauri anayotoka yeye anasema ina mapato makubwa na kwamba tayari kuna maboma ambayo wananchi walianza kuyajenga. Nitumie nafasi hii kuendelea kusisitiza kwamba pale kunapokuwa na juhudi za wananchi Halmashauri na Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa zinakuwa na uwezo na ni lazima ziweze kutenga fedha na kuzingatia vipaumbele kuweza kuunga mkono jitihada za kuendeleza miundombinu na hasa hii muhimu ya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba nichukue nafasi hii kuendelea kumkumbusha Mkurugenzi wa Halmashauri kutoka anapotokea Mheshimiwa Mbunge ili waweze kutenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya kuendelea kuendeleza miundombinu hii muhimu katika sekta ya elimu.
Name
Dorothy George Kilave
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Temeke
Primary Question
MHE. MWITA M. WAITARA K.n.y. MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa nyumba za walimu wa Sekondari nchini na kukarabati zilizochakaa?
Supplementary Question 2
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Je ni lini sasa Serikali itajenga shule ya sekondari ndani ya Jimbo la Temeke kwenye Kata ya Makangarawe kwa sababu tulikuwa hatuna eneo lakini sasa hivi tumepata eneo?
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia programu ya SEQUIP imekuwa ikijenga miundombinu ya shule zetu hizi katika kata. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge bila shaka shule hii uliyoitaja ya sekondari itajengwa kupitia program hii ya SEQUIP. Kwa hiyo Serikali itaendelea kufanya tathmini na kuweka vipaumbele na shule shule hii Serikali itakuja kujenga. (Makofi)
Name
Maimuna Salum Mtanda
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Newala Vijijini
Primary Question
MHE. MWITA M. WAITARA K.n.y. MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa nyumba za walimu wa Sekondari nchini na kukarabati zilizochakaa?
Supplementary Question 3
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia fursa. Ni lini Serikali itajenga nyumba za walimu katika shule za Sekondari za Jimbo la Newala Vijijini ili kuwapunguzia umbali walimu ambao wanakaa mbali na shule? Ahsante.
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikijenga nyumba za walimu kupitia taratibu mbalimbali na kupitia utaratibu wa program. Kwa mfano programu ya GPE, TSP na kupitia mradi wa SEQUIP Serikali imekuwa ikihakikisha kwamba inatenga fedha mahususi kabisa kwa ajili ya kujenga nyumba za walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali inatambua kwamba jukumu lote la kujenga nyumba za walimu haliwezi kutekelezwa na Serikali kuu peke yake. Ndiyo maana tunasisitiza na Halmashauri zenyewe ziweze kutenga fedha kutoka kwenye mapato yake ya ndani na Wakurugenzi waweze kufanya tathmini sahihi ya kujua uhitaji wa nyumba hizi za walimu ili kwa pamoja kupitia miradi hii inayotoka Serikali Kuu na kupitia mapato ya ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa pamoja tuweze kushirikiana kuhakikisha kwamba walimu wanajengewa nyumba za kuishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa muktadha huo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kuhakikisha fedha zinapatikana kwa ajili ya kujenga nyumba za walimu Tanzania nzima lakini pia hususan katika Mkoa na Jimbo analotoka Mheshimiwa Mbunge.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved