Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. Christine Gabriel Ishengoma
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza: - Je, lini Kata za Bwakila Juu, Singisa pamoja na Mkulazi, Morogoro Vijijini zitapatiwa mawasiliano ya uhakika?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, licha ya majibu mazuri nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya maswali mawili ya nyongeza ningependa kusisitiza katika Kata ya Bwakila Juu bado wana matatizo ya mawasiliano. Naomba sana muwasaidie kwa sababu hata barabara yao bado ni mbovu, mawasiliano ni mabovu na bado wanatumia milima kupata mitandao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza, katika Manispaa ya Morogoro, Kata ya Magado, Mtaa wa Fork Land ambao mimi mwenyewe naishi, bado kuna matatizo ya mawasiliano, tungeliomba Mheshimiwa Waziri mtuongezee mnara wa Vodacom angalau wananchi waweze kupata mawasiliano kwa sababu ni wananchi wengi, lakini hawana mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, katika Kata ya Bunduki na Mgeta pia wana matatizo ya mawasilino, naomba sana muwaongezee minara kusudi waweze kupata mawasiliano mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa maswali yangu hayo.
Name
Nape Moses Nnauye
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtama
Answer
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyiongeza ya Mheshimiwa Dkt. Ishengoma, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo aliyoyataja namna ya kushughulikia wakati mwingine siyo lazima kuongeza mnara, tunaweza tukaenda tukafanya ukaguzi na kama kutahitajika kuongeza mnara tutaongeza, lakini inawezekana tukahitajika kuongeza nguvu ya minara iliyopo.
Kwa hiyo, nachukua nafasi hii kuwaagiza TCRA Mkoa wa Morogoro waende leo kwenye eneo husika, wafanye tathmini na ndani ya siku tano walete matokeo ya tathmini hiyo, halafu tutafanya uamuzi wa nini cha kufanya ili kuboresha huduma kwenye maeneo aliyoyataja. (Makofi)
Name
Shamsia Aziz Mtamba
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Mtwara Vijijini
Primary Question
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza: - Je, lini Kata za Bwakila Juu, Singisa pamoja na Mkulazi, Morogoro Vijijini zitapatiwa mawasiliano ya uhakika?
Supplementary Question 2
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata za Tangazo na Naumbu, Kijiji cha Namgogori hakuna kabisa minara ya mawasiliano. Je, ni lini Serikali italeta minara ya mawasiliano katika Jimbo la Mtwara Vijijini kiujumla?
Name
Nape Moses Nnauye
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtama
Answer
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo aliyoyataja itabidi tukajiridhishe kama hayapo kwenye mradi wa minara unaoendelea sasa hivi wa rural coverage, tutafanya tathmini na tutaingiza kwenye mradi unaofuata ili wananchi wake wapate huduma za mawasiliano. (Makofi)
Name
Jackson Gedion Kiswaga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalenga
Primary Question
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza: - Je, lini Kata za Bwakila Juu, Singisa pamoja na Mkulazi, Morogoro Vijijini zitapatiwa mawasiliano ya uhakika?
Supplementary Question 3
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika minara zaidi ya 750 aliyoitoa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, mimi katika Jimbo la Kalenga nilipewa minara kumi. Sasa ni lini mtakwenda kujenga minara hiyo katika Kata ya Msaka ambapo napo nilipewa? (Makofi)
Name
Nape Moses Nnauye
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtama
Answer
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kiswaga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa minara 758 kwa ajili ya kupelekwa kwenye maeneo hasa ya vijijini na Jimbo la Mheshimiwa Kiswaga lilipata mgawo huo. Changamoto iliyotokea minara hii 758 haiwezi kuanza kujengwa yote kwa wakati mmoja, inajengwa kwa awamu na bila shaka Jimbo lake lipo katika mchakato huo wa ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, minara ambayo ilikuwa ijengwe na Vodacom kulikuwa na changamoto waliagiza vifaa vyote kwa wakati mmoja, kwa hiyo, vilichelewa kidogo kufika, lakini hivi tunavyoongea vifaa vyote vinavyotakiwa vipo nchini na ndani ya muda mfupi tutaona hiyo minara ikiinuka na wananchi wake watapata huduma wanazostahili kupata. (Makofi)
Name
Deodatus Philip Mwanyika
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Njombe Mjini
Primary Question
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza: - Je, lini Kata za Bwakila Juu, Singisa pamoja na Mkulazi, Morogoro Vijijini zitapatiwa mawasiliano ya uhakika?
Supplementary Question 4
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa namna ambavyo anafanya kazi na namna ambavyo Wizara inabadilisha nchi yetu kidigitali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikuliza swali kuhusiana na mnara mmoja tu, wengine wanaongelea minara 10 au 15 mimi ninara miwili tu ambao ni mnara wa Kijiji cha Uliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka juzi niliambiwa ungejengwa mwaka jana, mwaka jana nikaambiwa utaingizwa kwenye bajeti ya mwaka huu, lakini hata kwenye bajeti ya mwaka huu mimi sijaona, nimeona mnara mwingine wa kijiji kingine, lakini Uliwa ndipo kwenye tatizo hasa la mawasiliano na pana shule, sekondari, zahanati, kituo cha afya, lakini hawana mawasiliano, wapo chini. Mheshimiwa Waziri ni lini sasa Uliwa itaingizwa kwenye bajeti na itapata mnara huu? (Makofi)
Name
Nape Moses Nnauye
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtama
Answer
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Mwanyika, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru kwa pongezi zake kwa niaba za watumishi wa Wizara tunazipokea ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Deo amekuwa akilifuatilia jambo hili siyo mara moja au mbili, nataka nitoe ahadi ndani ya Bunge lako mimi na Mheshimiwa Deo tutakaa pamoja tulishughulikie hili jambo tuhakikishe tunalimaliza. Mheshimiwa Deo nikimaliza nitakuja tukae, nichukue taarifa zako, nione wapi tunakwama, lakini nikuhakikishie kwamba nia ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Samia ni kuhakikisha kila Mtanzania popote alipo anaunganiushwa na huduma za mawasiliano. (Makofi)
Name
Aida Joseph Khenani
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Nkasi Kaskazini
Primary Question
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza: - Je, lini Kata za Bwakila Juu, Singisa pamoja na Mkulazi, Morogoro Vijijini zitapatiwa mawasiliano ya uhakika?
Supplementary Question 5
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Mheshimiwa Waziri natambua mikakati inayoendelea ya kuunganisha Mkoa wa Rukwa na Katavi kwenye maeneo ambayo hayana mawasiliano na kwa sababu mawasiliano ni haki ya wananchi wote, ningependa kufahamu, kuna kata nne ambazo bado hazina mawasiliano. Kata za Mkinga, Kipili, Isale na Mkwamba, ni lini watu hao watapata mawasiliano?
Name
Nape Moses Nnauye
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtama
Answer
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba mikakati inayoendelea lengo lake ni kuhakikisha kila Mtanzania popote alipo anapata huduma za mawasiliano na hasa mikoa ya pembezoni. Mimi nimefanya ziara kwenye baadhi ya maeneo ya Rukwa, Sumbawanga, Katavi na kadhalika na ninajua changamoto iliyopo na hasa maeneo haya ya mipakani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kata alizozitaja nitakwenda kuangalia kwenye Mradi wa Tanzania ya Kidigitali kama hazimo jambo ambalo siamini, kama hazimo nitahakikisha zinaingia kwenye mradi unaofuata na kama zimo tutasukuma ili mradi huo uanze mapema tuwahudumie wananchi wako. (Makofi)