Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza kujenga reli ya mwendokasi ya kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay?
Supplementary Question 1
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Je, Serikali inajua faida zitakazopatikana kutokana na ujenzi wa njia ya reli ya mwendokasi kutoka Mtwara kwenda Mbamba Bay Wilayani Nyasa? (Makofi)
(b) Je, ni kwa nini Serikali inachelewesha kuanza ujenzi wa njia ya reli ya mwendokasi kutoka Mtwara kwenda Mbamba Bay? (Makofi)
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kama nilivyosema kwenye swali la msingi, kwanza nianze kumshukuru Mheshimiwa Msongozi kwa sababu yeye pamoja na Wabunge wengi ambao nina uhakika watasimama tu kwa ajili ya kuhoji swali hili, wamekuwa wakihitaji kwa muda mrefu kuona SGR inajengwa kutoka upande wa Southern Corridor na Serikali inafahamu umuhimu wa jambo hili. Unapozungumza SGR ya Kusini lazima ufungamanishe Liganga na Mchuchuma pamoja na Bandari. Nini Serikali imefanya mpaka sasa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya kwanza tumekwishalipa fidia mwaka jana wananchi 1,142 takribani shilingi bilioni 15.4. Hii ni commitment ya juu kabisa ya kuona jinsi ambavyo tunataka jambo hili likamilike mapema iwezekanavyo. Hatua ya pili tumekwishaanza ujenzi wa bandari ya Mbamba Bay na hivi ninavyozungumza tupo hatua za mwishoni kuanza kujenga Bandari ya Kisiwa Mgao – Mtwara. Kwa sababu unapozungumza reli hiyo lazima uzungumzie namna ya kusafirisha chuma pamoja na makaa ya mawe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya tatu tunaboresha viwanja vya ndege kuanzia Njombe ambayo tupo kwenye usanifu wa kina lakini Mtwara pamoja na Lindi ambayo tunajenga pia kingine kipya. Kama nilivyosema hata katika bajeti hii tumetenga takribani milioni 702 yote hiyo ni kuelekea kuhakikisha kwamba tunafanya jambo hilo linakamilika mapema iwezekanavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hatua nyingine ambayo tunaifanya tunapojenga Reli ya SGR kutoka Dar es Salaam - Mwanza mpaka Kigoma takribani kilometa 2,102 hiyo ni kuonesha utayari wa Serikali katika kujenga Reli ya SGR Kusini. Kwa sababu unaanza hatua ya kwanza unamaliza hatua ya pili halafu unakwenda hatua zingine ambazo zinafuatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza tayari tumejenga 2,102 reli kwa maana kama nchi na inakuwa ni nchi ya tano. Kwa hiyo, tukijenga na kilometa 1,000 na Mtwara Corridor 1,000 tutakuwa na 3,000 kama na mia tatu au na mia nne. Hivyo, tutakuwa ni nchi ya tatu duniani kwa kujenga reli ndefu zaidi na kwa nchi ya kwanza kwa nchi zinazoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, faida zake kama alivyouliza Mheshimiwa Mbunge. Tuna faida nyingi ambazo tunazipata tukifanikiwa kujenga Reli ya Kusini kama nilivyosema Reli ya Kusini inafungamanishwa pamoja na Liganga na Mchuchuma ambayo Liganga na Mchumchuma tuna madini ya Vanadian, takribani pengine asilimia 0.4 kila mzigo unaopata pale ndani. Tuna vanadian na titanian ambayo inatengenezea engine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili inatusaidia kwenda kupata umeme megawatt 600 ambayo takribani 250 inakwenda kuyeyusha chuma na 350 inakwenda kuingia kwenye Gridi ya Taifa, nchi yetu ina changamoto ya umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi reli hii itatusaidia sasa kuchukua malighafi zile zote kwa maana ya Mchuchuma yale makaa ya mawe kusafirisha, kuyatoa pale yale yalipo kuyapeleka duniani yanapohitajika kwa wingi zaidi sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo taifa letu litapata fedha nyingi zaidi. Kama haitoshi pia itatuwezesha kufungamanisha nchi yetu kwenye viwanda, takribani milioni 2.9 ya chuma tutazalisha kwa mwaka wakati sisi mahitaji yetu tunakalibia milioni moja. Hivyo, basi niendelee kumuomba Mheshimiwa Mbunge, nafahamu yeye ni mkulima na angependa kujua faida kubwa ambazo zinapatikana kusafirisha mazao mbalimbali kwenye ukanda wa Kusini kupeleka nchi jirani na nchi za mbali kupitia reli hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niendelee kumuomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira wakati Serikali inakamilisha mchakato huu na hatimaye tutaenda kuanza ujenzi huo.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved