Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Masache Njelu Kasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Primary Question

MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza: - Je, lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya upanuzi wa Kituo cha Afya Mtanila ili kiendane na vituo vinavyojengwa sasa?

Supplementary Question 1

MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na tuna imani pesa hizo zitafika kwa wakati. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Chunya tuna kata za kimkakati: Kata ya Ifumbo, Kata ya Matwiga pamoja Mafyeko, ambazo zimeanza kujenga vituo vya afya kwa nguvu za wananchi na ni muda mrefu. Je, ni lini sasa Serikali itatoa fedha za kutosha kukamilisha vituo hivi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Wilaya ya Chunya tuna changamoto kubwa sana ya watumishi hasa kwenye upande wa Idara ya Afya. Je, ni lini sasa Serikali itatupatia watumishi wa kutosha hasa madaktari ili kuweza kukabiliana na changamoto za uhaba wa watumishi? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, hivi vituo vya afya ambavyo Mheshimiwa Mbunge amevitaja, cha Kata ya Matwiga, Mafyeko na kata nyingine, ni vituo ambavyo kimsingi hata tulipofanya ziara kule na Mheshimiwa Waziri Mkuu, alivisema na Ofisi ya Rais, TAMISEMI tulishavichukua. Pia Mheshimiwa Waziri Mkuu alielekeza Mkurugenzi aanze kutenga fedha. Napongeza kwamba ameanza utekelezaji huo. Nimhakikishie tu kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunatambua na tutatenga fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa vituo hivyo vya afya.

Mheshimiwa Spika, pili kuhusiana na upungufu wa watumishi, ni kweli Halmashauri ya Chunya ni moja ya halmashauri ambazo zina upungufu mkubwa wa watumishi wa sekta ya afya. Niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge wote kwamba tumeainisha kwa vipaumbele halmashauri zenye upungufu mkubwa zaidi wa watumishi. Kila kibali cha ajira kinapojitokeza watapewa watumishi wengi zaidi kuliko wa halmashauri zile ambazo zina nafuu ya upungufu wa watumishi. Kwa hiyo Halmashauri ya Chunya pia itapewa kipaumbele katika ajira zinazofuata. (Makofi)

Name

Emmanuel Peter Cherehani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Primary Question

MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza: - Je, lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya upanuzi wa Kituo cha Afya Mtanila ili kiendane na vituo vinavyojengwa sasa?

Supplementary Question 2

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, naomba kujua mkakati wa kuanza ujenzi wa Kituo cha Afya Ulowa, ahadi ambayo Mheshimiwa Waziri na wewe mlikuja kuwaahidi wananchi, ahsante.

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, Kata ya Ulowa ni kata yenye wananchi wengi sana katika Jimbo la Ushetu. Tulishafanya ziara pale na kwa kweli mahitaji ya wananchi pale ni kituo cha afya. Nikuhakikishie tu kwamba, tumeshakiingiza kwenye Mpango wa Vituo vya Afya vya Benki ya Dunia na tunaamini fedha ikitoka mapema iwezekanavyo tutakwenda kuanza ujenzi katika Kata ya Ulowa. (Makofi)