Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Oscar Ishengoma Kikoyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Primary Question

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO aliuliza: - Je, lini Serikali itawasilisha Bungeni Muswada wa kutunga Sheria ya kuwalinda watumiaji huduma na bidhaa nchini?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali lililotangulia lilikuwa linahusu masuala ya watumiaji na mikopo. Sasa ni lini Serikali kutokana na umuhimu wa watumiaji itatenganisha masuala ya ushindani na masuala ya watumiaji ili tuweze kuwalinda watumiaji wa Tanzania?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Tanzania tunazalisha bidhaa. Ili kuuza ile bidhaa, watumiaji inabidi wanunue. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhamasisha watumiaji wa Tanzania wanunue na kutumia bidhaa na huduma zilizozalishwa hapa nchini? (Makofi)

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba sheria hii tuliyoitaja inasimamia ushindani wa haki pamoja na kuwalinda walaji. Uzoefu unaonesha kwamba nchi nyingi duniani zinatumia sheria hii moja ambayo inachukua maeneo mawili kwa maana ya ushindani wa haki katika soko, lakini pia kupitia humo kumlinda mlaji, kwa sababu tunapitia sheria hii, pale ambapo tunaona kuna haja ya kutenganisha kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameshauri, basi Serikali haitasita kufanya hivyo na tunachukua ushauri wake, lakini pia na wadau wengine ambao watatoa maoni wakati tunaihuisha au tunarekebisha Sheria hii Na. 8 ya Mwaka 2003.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, ni kweli sisi kama Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, tayari tuna mikakati mbalimbali. Moja ya kaulimbiu yetu katika kuhakikisha tunakuza Sekta ya Viwanda na Uzalishaji nchini ni, “Nunua Tanzania, Jenga Tanzania,” kwa maana ya nunua bidhaa zilizozalishwa Tanzania ili uweze kuijenga nchi yako Tanzania.

Mheshimiwa Spika, tunaendelea kufanya hivyo, lakini kwa kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zina ubora unaotakiwa ili ziweze kushindana na bidhaa zinazotoka nje, kwa sababu ili kuhakikisha Watanzania wanapenda bidhaa zao za ndani, lazima ziwe na ubora ule ambao unalingana na bidhaa nyingine kutoka nje ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaendelea kuhakikisha tunatangaza hilo, lakini kuhakikisha bidhaa zetu zinazalishwa katika ubora unaotakiwa, nakushukuru.