Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Sylivia Francis Sigula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. SYLVIA F. SIGULA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka vizimba Ziwa Tanganyika?
Supplementary Question 1
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, tunaishukuru Serikali kwa kutenga hiyo pesa kwa ajili ya kuwakopesha wavuvi, lakini bado wavuvi wetu hawana elimu ya mikopo. Je, Serikali ipo tayari kwenda kutoa elimu ya mikopo kabla haijatoa mikopo hiyo ili wavuvi wafahamu vigezo na masharti ili waweze kupatiwa hivyo vizimba? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; mwaka jana hapa tulizuia, Wabunge walitusaidia kuzuia kufungwa kwa Ziwa Tanganyika. Leo kuna sintofahamu kwa wavuvi wa ukanda wa Ziwa Tanganyika; Kigoma, Rukwa na Katavi. Wananchi na wavuvi wana taharuki kwamba ziwa linakwenda kufungwa. Je, ni ipi kauli ya Serikali ya kuwaondoa hofu wananchi wa ukanda wa Ziwa Tanganyika? (Makofi)
Name
Alexander Pastory Mnyeti
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Misungwi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nianze na hili la kwanza la kutoa elimu kwa wavuvi. Ni kweli elimu ni muhimu sana, lakini nimkumbushe Mheshimiwa Mbunge, miezi sita iliyopita mimi na Mheshimiwa Waziri na wataalamu wa Wizara ya Mifugo, tulifanya zoezi la kuzunguka katika maeneo yote ya pembezoni mwa Ziwa Tanganyika, lengo likiwa ni pamoja kuhamasisha wavuvi wetu kuwapa elimu juu ya namna gani wanaweza wakakopa vizimba na boti.
Mheshimiwa Spika, baada ya hapo tuliacha wataalamu wetu kwenye maeneo ya vijiji vyote vya wafugaji wakaendelea kutoa elimu inayohusiana na mikopo na namna ya uendeshaji wa vizimba. Namwomba Mheshimiwa Mbunge, kama kuna eneo ambalo anafikiri bado hawajapata elimu ya kutosha, Wizara ya Mifugo kupitia Serikali tupo tayari kuendelea kutoa elimu hiyo ya mikopo na namna ya kuendesha vizimba hivyo na boti pia. Kwa hiyo, naomba katika hilo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tupo tayari kushirikiana naye katika kutoa elimu.
Mheshimiwa Spika, hili la pili, kuhusiana na kufunga Ziwa Tanganyika, kwanza ni kweli lazima tukubaliane mazao ya samaki katika Ziwa Tanganyika yanapotea na namna pekee ya kuyalinda ni pamoja na kuzuia shughuli za uvuvi katika maziwa yetu. Sasa tukiruhusu wavuvi waendelee kuvua na hali inazidi kuwa mbaya, samaki wanazidi kupotea, kwa kweli hatutakuwa tunaitendea haki Sekta hii ya Uvuvi. Kwa hiyo, tukafikiri kwamba pengine ni lazima tusimamishe shughuli za uvuvi katika Ziwa Tanganyika ili kuruhusu mazalia ya Samaki yaweze kuchukua nafasi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge, awe balozi mzuri katika hili. Hili lina lengo jema kwa sababu hata baada ya kufungua watakaonufaika katika zoezi hili ni hao hao wavuvi wanaoishi katika maeneo hayo, ahsante.
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, hiyo sehemu ya pili ya kufunga Ziwa labda kama mmekubaliana na nchi jirani. Kama hawafungi, sina hakika kama kuna mpaka wa samaki kwenda upande mwingine, wao wakaendelea wakati ninyi huku mmefunga. Yaani wavuvi wetu huku wawe wanalinda samaki kwa ajili ya wale wengine, ama mmekubaliana na nchi jirani kwamba wote uvuvi utasimama kwa muda halafu uvuvi utaanza baadaye? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, Ziwa Tanganyika kama tunavyofahamu, linamilikiwa na nchi tatu: Zambia, Kongo na Tanzania. Hii ya kufunga, tarehe 15 Mei ni Mkataba wa Kimataifa dhidi ya nchi hizi zinazozunguka Ziwa Tanganyika kwamba ifikapo tarehe 15 mwezi Mei, lazima ziwa lote lifungwe katika nchi zote zinazozunguka katika ziwa hili.
Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba, sisi Tanzania pamoja na kwamba mkataba huu tulisaini, tulikuwa hatujawahi kuutekeleza, lakini wenzetu wamekuwa wakifunga ziwa na sisi tukasema, basi kwa mwaka huu tuanze kutekeleza mkataba huu ambao tumeshausaini siku nyingi na hatujawahi kuutekeleza. Kwa hiyo, kwa mwaka huu tunaanza kuutekeleza kuanzia tarehe 15 Mei na kuendelea kwa muda wa miezi mitatu, ahsante.
Name
Joseph Anania Tadayo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwanga
Primary Question
MHE. SYLVIA F. SIGULA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka vizimba Ziwa Tanganyika?
Supplementary Question 2
MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Je, ni lini Serikali italeta mradi huo wa ufugaji wa samaki kwa vizimba katika Jimbo langu la Mwanga katika Bwawa la Nyumba ya Mungu na Ziwa Jipe? (Makofi)
Name
Sylivia Francis Sigula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika jibu la msingi kwamba vizimba vinaambatana kwanza na hatua mbalimbali; hatua ya kwanza ni kufanya uchunguzi kama eneo hilo linaruhusu kuweka vizimba halafu baadaye ndiyo inakuja hatua hiyo ya pili.
Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Mbunge kwamba tutatuma timu ya wataalamu kwenda kufanya uchunguzi katika Bwawa la Nyumba ya Mungu na baada ya uchunguzi huo tutakuja na majibu kama je, eneo hilo linafaa kwa ajili ya vizimba ama la, ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved