Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Ghati Zephania Chomete
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. GHATI Z. CHOMETE aliuliza:- Je, kuna mpango gani wa kuhakikisha dawa zinapatikana na kukidhi mahitaji katika Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali za Mkoa wa Mara?
Supplementary Question 1
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kumekuwa na tatizo la MSD kupeleka madawa kwenye hospitali, vituo vya afya yanayokaribia kwisha muda wake. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha tatizo hili au jambo hili linamalizika kabisa ili lisilete madhara kwa wananchi wetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Kituo cha Afya cha Muriba katika Jimbo la Tarime Vijijini kinahudumia wananchi wa Kata tano ambao idadi yao ni 73,000 na zaidi, lakini idadi ya dawa zinazopelekwa ni za kuhudumia wananchi wa Kata moja yaani wananchi 14,000. Je, ni kwa nini Serikali isipeleke dawa kulingana na idadi ya watu wanaohudumiwa pale? Ahsante. (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishakubaliana Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Wizara ya Afya kuhusiana na dawa zinazopelekwa kwenye vituo vyetu kuwa na muda mrefu kabla hazijafikia expiring date yake. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tangu Mwaka wa Fedha 2021/2022, tayari kwa kiasi kikubwa sana dawa zinazopelekwa kwenye vituo vyetu angalau zina miezi 12 kabla ya ku-expire na tutaendelea kuhakikisha kwamba suala hili linasimamiwa hivyo ili wananchi wetu wapate dawa salama pia ziweze kutumika badala ya kuharibika zikiwa vituoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, wakati tunapeleka dawa kwenye vituo vya afya, hatuangalii kituo cha afya kiko katika Kata ipi kwa maana kwamba hatuweki mipaka kwamba wananchi wa kata ile tu ndiyo watapata huduma, tunaangalia catchment population ya wananchi wote hata kama ni kata tano, sita zinapata huduma katika kituo kile basi tunahakikisha tunapeleka fedha kwa ajili ya dawa zinazotosha wananchi wote ambao wanapata huduma ile. Kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tutakiangalia kituo hicho cha afya ili tuweze kukiongezea pia bajeti ili kihudumie vizuri wananchi wa kata za Jirani. Ahsante.
Name
Cecilia Daniel Paresso
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. GHATI Z. CHOMETE aliuliza:- Je, kuna mpango gani wa kuhakikisha dawa zinapatikana na kukidhi mahitaji katika Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali za Mkoa wa Mara?
Supplementary Question 2
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Wilaya ya Karatu tumepata Hospitali mpya ya Wilaya lakini bado kuna upungufu wa vifaa na rasilimali watu. Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha hospitali hiyo inapata mahitaji hayo ili kuwepo na ufanisi katika utoaji wa huduma?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali imejenga Hospitali mpya ya Halmashauri ya Karatu na Serikali inatambua kwamba kweli kuna upungufu wa watumishi na vifaatiba. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwanza tumeshapeleka fedha zaidi ya shilingi milioni 800 katika Halmashauri ya Karatu kwa ajili ya kununua vifaatiba na vituo vingine vya afya na zahanati pia tutaendelea kupeleka fedha hiyo katika mwaka wa fedha huu na mwaka ujao wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na watumishi tayari Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa kibali cha ajira ya watumishi zaidi ya 46,000. Watumishi wa Sekta ya Afya ni miongoni mwa watumishi watakaoajiriwa, tutahakikisha tunatoa kipaumbele kwa Hospitali ya Halmashauri ya Karatu ili itoe huduma bora zaidi kwa wananchi. Ahsante. (Makofi)
Name
Asha Abdullah Juma
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. GHATI Z. CHOMETE aliuliza:- Je, kuna mpango gani wa kuhakikisha dawa zinapatikana na kukidhi mahitaji katika Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali za Mkoa wa Mara?
Supplementary Question 3
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Je, Serikali ni lini itawasaidia wastaafu ambao wameambiwa bima zao zimesitishwa ambapo na wao wanaendelea kuumwa hawapati dawa huko kwenye sehemu zao?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni haki ya wastaafu kuendelea kupata huduma za afya kupitia bima. Naomba tulichukue jambo hili, tuweze kufuatilia ni wastaafu gani ambao wamepata changamoto hiyo. Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya tutalifanyia kazi ili wazee hawa wapate haki yao ya matibabu. Ahsante sana. (Makofi)
Name
Boniphace Mwita Getere
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Primary Question
MHE. GHATI Z. CHOMETE aliuliza:- Je, kuna mpango gani wa kuhakikisha dawa zinapatikana na kukidhi mahitaji katika Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali za Mkoa wa Mara?
Supplementary Question 4
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya Hunyari, Kituo cha afya Mgeta na Kituo cha Afya Ikizu mara nyingi sana vinakosa dawa na mahitaji maalum kwenye maeneo yao. Je, ni lini Serikali itapeleka dawa kwenye vituo hivyo? Ahsante. (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA(MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Vituo vya Afya vya Mgeta, Hunyari na kituo kingine ambacho amekitaja ni miongoni mwa vituo ambavyo tayari Serikali ilishaviweka kwenye mpango wa kuhakikisha kwamba vinapata dawa zote za msingi, dawa zote muhimu kwa 100%. Naomba nitumie nafasi hii kumwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kuhakikisha anakaa na Mganga Mkuu wa Halmashauri na Mganga Mkuu wa Mkoa kufanya tathmini ya upatikanaji wa dawa na kuona dawa ambazo zinapungua ili waweze kuzinunua haraka iwezekanavyo na Ofisi ya Rais, TAMISEMI tutafuatilia hilo. Ahsante. (Makofi)