Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Edwin Enosy Swalle
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupembe
Primary Question
MHE. EDWIN E. SWALE aliuliza:- Je Serikali ina Mkakati gani wa kuboresha maslahi ya watumishi wa umma nchini?
Supplementary Question 1
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza niishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita kwa kujali maslahi ya watumishi nchini. Kwa kweli watumishi wana matumaini makubwa na Serikali hii, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; Serikali imekuwa na mpango wa kujenga nyumba za watumishi maeneo mbalimbali na wapo watumishi ambao huwa wanapata hizi nyumba na wengine wanapanga nyumba zao kwa hela zao wenyewe. Naomba kujua Serikali ina mpango gani wa kuwa na fedha maalum za kuwapatia watumishi ambao hawana nyumba za Serikali? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; mwaka 2020 Serikali ilitoa maelekezo kwamba halmashauri ambazo zilikuwa kwenye miji au nje ya maeneo yao wahamie kwenye maeneo yao. Halmashauri ya Njombe DC ni sehemu ya hizo halmashauri ambazo walihama kutoka Njombe Mjini kwenda Mtwango na baadaye kwenda Kidegembye, lakini mpaka leo watumishi hao ambao walihama kwenye maeneo hayo hawajalipwa fedha za uhamisho kwenye hayo maeneo. Je, ni lini watumishi wangu wa Halmashauri ya Njombe DC watalipwa fedha zao za uhamisho? (Makofi)
Name
Ridhiwani Jakaya Kikwete
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chalinze
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Swalle ambaye kwa hakika anafanya kazi kubwa ya kufuatilia maslahi ya watumishi na sisi kama Serikali tunaendelea kumpongeza Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la watumishi ambao wanakwenda kwenye vituo vya kazi wanakosa nyumba na kwamba wanaangaliwaje katika masuala mazima ya kuwa-motivate. Serikali kwanza imeendelea kuhakikisha kwamba watumishi wote wa umma hasa wale ambao wanakwenda katika maeneo ambayo yana changamoto kama ambazo amezieleza Mheshimiwa Mbunge, tumeendelea kuwaangalia katika maslahi yao kupitia taratibu mbalimbali zikiwemo zile taratibu za Mamlaka ya Serikali za Mitaa ambayo wamekuwa wanatoa token kwa ajili ya kuwasaidia watumishi hawa waweze kukaa katika mazingira ambayo watafanya kazi bila kujilaumu kwamba kwa nini wamekwenda kufanya kazi kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, yapo baadhi ya maeneo, Serikali kupitia mapato ya ndani imekuwa inatoa pesa kuwanunulia vifaa ikiwemo magodoro na vitanda. Pia, halmashauri nyingine zile ambazo zina uwezo mkubwa wamekuwa wanatoa pesa kuwasaidia hata kuwapangia nyumba watumishi hao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka nimhakikishie Mheshimiwa Swalle kwamba katika utaratibu huu kwangu mimi kama Mheshimiwa Waziri mhusika wa Watumishi, nataka nielekeze halmashauri zetu zote kuendelea kutenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya kuhakikisha watumishi wetu wanaendelea kuwa motivated kwa maana ya kutengenezewa mazingira mazuri ya kuendelea kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya swali la pili kwa watumishi ambao wamehamishwa mara mbili, wale watumishi wa Halmashauri ya Njombe DC. Nataka kulihakikishia Bunge lako pamoja na Mheshimiwa Mbunge Swalle kwamba Serikali haina nia ya kuwadhulumu watumishi hao. Serikali itaendelea kuweka kipaumbele kimojawapo ikiwemo kulipa au kutenga pesa kwa ajili ya kuwalipa madeni haya ambayo yameendelea yakitokea katika maeneo hayo hususan katika Halmashauri yako ya Njombe DC. (Makofi)
Name
Ally Mohamed Kassinge
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilwa Kusini
Primary Question
MHE. EDWIN E. SWALE aliuliza:- Je Serikali ina Mkakati gani wa kuboresha maslahi ya watumishi wa umma nchini?
Supplementary Question 2
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ukweli kwamba Watumishi wa Umma Kada ya Ualimu ndiyo kada pekee ambayo hainufaiki na aina yoyote ya allowance. Hawana extra duty allowance, hawana sitting allowance, hawana acting allowance na aina nyingine ya allowance. Kwa dhamira hiyo njema ya Serikali; je, Serikali ipo tayari sasa kufikiria kukaa ili kutoa teaching allowance kwa walimu? Nashukuru. (Makofi)
Name
Ridhiwani Jakaya Kikwete
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chalinze
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mawazo mazuri yanayotolewa na Mheshimiwa Mbunge kwetu sisi Serikali ni kupokea, kuchukua na kwenda kuangalia kwa sababu unapozungumzia allowance yoyote ile jambo kubwa au kigezo kikubwa ni uwezo wa kipato wa kibajeti ndani ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sisi tutaendelea kuangalia haya mawazo mazuri yaliyotolewa na Mheshimiwa Mbunge. Kama uwezo wa kuweka allowance hizi utakuwepo tutaendelea kuangalia. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na hasa kundi kubwa analolisemea la walimu, Serikali imeendelea kuwaangalia walimu katika maslahi mengi sana yakiwemo maslahi ya kuhakikisha walimu wanaendelea kupunguziwa mzigo wa masomo kwa kuongeza namba kubwa ya walimu ambapo katika mwaka huu wa bajeti watakuja kueleza hapa wenzetu jinsi ambavyo Serikali inaendelea kuongeza namba ya walimu. Pia, kuendelea kuwawekea mazingira mazuri ya kuwapa motisha nzuri ili waendelee kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka kulihakikishia Bunge lako na Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inalitambua hilo. Tutalichukua na tutaendelea kufanyia kazi kwa uwezo wa kibajeti.
Name
Issa Jumanne Mtemvu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibamba
Primary Question
MHE. EDWIN E. SWALE aliuliza:- Je Serikali ina Mkakati gani wa kuboresha maslahi ya watumishi wa umma nchini?
Supplementary Question 3
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na changamoto kubwa sana ya mpango wa kurithishana madaraka Serikalini au wanaita succession plan. Hii inasababishwa na kutokustaafu kwa watu wengi, lakini kutokuajiri kada nyingi kwa muda mrefu. Je, ni upi mpango wa Serikali kusimamia hii succession plan au mpango huu kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma? Ahsante.
Name
Ridhiwani Jakaya Kikwete
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chalinze
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako kwamba Serikali inao mpango wa succession plan katika kada zote. Kwa sababu katika utaratibu wa kupitisha muundo ili muundo wako uweze kukubalika katika Ofisi ya Katibu Mkuu Utumishi, moja ya kitu kikubwa ambacho lazima ukiweke ndani ni succession plan na hili Mheshimiwa Mbunge na Bunge linaweza likathibitisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na maombi mengi sana yanayoletwa kwa Katibu Mkuu tukiombwa kuongezea baadhi ya kada fulani au watu fulani muda wa nyongeza kabla hawajastaafu na Katibu Mkuu amekuwa anasisitiza sana. Hili jambo liende kwa Wizara na Taasisi zote ikiwemo wenzetu wa Serikali za Mitaa kwamba, kabla haujaleta muundo kwa Katibu Mkuu Utumishi, ni vyema uhakikishe kwamba ndani yake upo mpango wa kurithishana madaraka kama ambavyo inaelekezwa katika taratibu. (Makofi)
Name
Janejelly Ntate James
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. EDWIN E. SWALE aliuliza:- Je Serikali ina Mkakati gani wa kuboresha maslahi ya watumishi wa umma nchini?
Supplementary Question 4
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwapongeze Serikali kwa juhudi wanazofanya kuboresha maslahi ya watumishi, lakini swali langu ni moja. Katika majibu ya Waziri amesema sasa wamerudisha watumishi kupandishwa vyeo baada ya miaka mitatu. Je, watafanyaje kwa hawa ambao walishaumia kwa miaka minne na imewapotezea tayari gap la kupata promotion nyingine? Ahsante.
Name
Ridhiwani Jakaya Kikwete
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chalinze
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali zuri lililoulizwa na Mheshimiwa Janejelly ni kwamba kila inapokuja sheria yoyote utaratibu ni kwamba sheria hairudi nyuma inakwenda mbele, hili jambo nataka Bunge lako lifahamu. Serikali katika kuhakikisha kwamba huu msawazo, niite msawazo katika lugha nzuri; msawazo wa kimamlaka wa Watendaji wa Serikali unakuwepo, imeendelea kuangalia ili wasije watu wengine wakaachwa nyuma. Ndiyo maana Serikali ikaja na wazo la kuwa na kitu kinachoitwa vyeo vya mserereko ili kusaidia kufanya hiyo ambayo kwa lugha ya Kingereza tunaita adjustments ili kila mmoja akae katika cheo anachostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka nilihakikishie Bunge lako na Mheshimiwa Mbunge kwamba hilo wazo lililotolewa na Mheshimiwa Mbunge ni moja ya wazo ambalo tunalichukua na tumekwishaanza kulifanyia kazi. Nataka nimhakikishie na nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba hakuna mfanyakazi atakayeachwa katika kupandishwa vyeo.