Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Esther Nicholus Matiko
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza: - Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya Utegi hadi Kilongwe?
Supplementary Question 1
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, barabara za kiulinzi zilizopo mipakani ni muhimu sana kwa ulinzi na usalama wa Taifa letu lakini kwa bajeti ambayo imewasilishwa jana kwa mwaka wa fedha 2024/2025, hakuna hata senti tano ambayo imetengewa barabara hizi kwa nchi nzima. Je, ni lini Barabara ya Kiulinzi inayoanzia Kirongwe Wilayani Rorya Mpaka Nyanungu Wilayani Tarime itaenda kujengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kipande kilichopo kwenye mradi wa ujenzi wa Barabara wa kuanzia Tarime mpaka Mugumu, kwa maana ya Tarime Mjini mpaka Mogabiri kimeharibiwa sana na mvua ambazo zinaendelea kunyesha. Ninataka kujua Serikali inachukua mkakati gani wa kuhakikisha kwamba inaenda kuziba yale mashimo na mahandaki ambayo yamejijenga kwenye hicho kipande cha lami ili kuweza kurudisha usafiri na usafirishaji kwenye Jimbo la Tarime Mjini? (Makofi)
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante, ni kweli Barabara ya Ulinzi ya Kirongwe – Sirari ninajua inaenda mpaka Kegonga inaendelea kufanyiwa ukarabati kuhakikisha kwamba inapitika. Katika kipindi hiki tunachokifanya katika barabara hii ni kuhakikisha kwamba inapitika kwa kiwango cha changarawe na inapitika muda wote, wakati Serikali tunatafuta fedha kuzijenga hizi barabara ambayo ni moja ya kipaumbele cha Wizara na Serikali kuhakiksha kwamba Barabara za Ulinzi zinatekelezwa.
Mheshimiwa Spika, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, zipo Barabara za Ulinzi ambazo zinaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami na siyo kwamba Barabara zote Tanzania za Ulinzi hazijengwi. Zipo ambazo zipo kwenye mpango. Maana yake amesema Barabara zote za Ulinzi; Hapana, siyo kweli. Zipo ambazo zinaendelea kujengwa na zingine zitatangazwa katika bajeti hii.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kipande kilichoharibika cha kutoka Tarime kwenda Mogabiri, kipande hiki ni cha kiwango cha lami ambayo ni ya zamani. Ninamshakikishia Mheshimiwa Mbunge, katika mkandarasi ambaye sasa anajenga kambi eneo la Serengeti pale Mugumu, ambaye atajenga, ndiye atakayejenga pia kipande hicho cha lami. Ataifumua na kuijenga upya. Kwa hiyo, tutakachofanya ni kuangalia uwezekano.
Mheshimiwa Spika, hatutaijenga kwa kuziba, bali tunaifumua yote na kuijenga yote. Kwa sasa Meneja wa Mkoa wa Mara ahakikishe kwamba yale mashimo ambayo yapo anayaziba kwa muda ili yasije yakaleta changamoto kwa watumiaji, wakati tunasubiri kuijenga hiyo barabara yote ambayo tulishaitangaza, ahsante. (Makofi).
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved