Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Soud Mohammed Jumah
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Donge
Primary Question
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH K.n.y. MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani kunusuru vipando visivyohimili maji ya bahari katika Bonde la Tibirinzi Chakechake Pemba?
Supplementary Question 1
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza kwa niaba ya Mheshimiwa Maryam Mwinyi. Swali la kwanza; kwa kuwa uharibifu wa misitu ya mikoko umepelekea maji ya bahari kupanda juu na kuingia katika mashamba ya kilimo ya wananchi Kisiwani Pemba na kupelekea uzalishaji wa mazao kuwa hafifu. Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza ujenzi wa Tuta la Sipwese ili kupunguza maji ya bahari yasiingie katika mashamba ya wananchi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, Mheshimiwa Naibu Waziri, upo tayari kufanya ziara kuona uharibifu wa mikoko na athari zake ili kuharakisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuhami na kurejesha misitu ya mikoko Kisiwani Pemba? Ahsante sana.
Name
Khamis Hamza Khamis
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, kwanza ninataka kumwambia Mheshimiwa Mbunge kwamba Sipwese pale tuna miradi miwili. Tuna miradi miwili, lakini yote ni ya ujenzi wa hayo matuta. Mmoja tayari umeshakamilika kwa asilimia zote na umeanza kuleta manufaa kwa wananchi, lakini mwingine hivi sasa upo kwenye 80% ambayo jumla ya shilingi bilioni 1.1 zilitumika kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo.
Mheshimiwa Spika, nimwambie tu Mheshimiwa kwamba tarehe 24 Septemba, 2024, mimi na Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Kijaji, tulifanya ziara katika eneo hilo la Sipwese na tulitoa maelekezo kwa mkandarasi ili ukuta ule uweze kumalizika kwa haraka. Tulikubaliana baada ya miezi miwili kwa maana kwamba mwezi Desemba ukuta ule utakuwa umeshakamilika. Nimwambie tu Mheshimiwa, awe na subira, tayari mkandarasi yupo site na ujenzi unaendelea.
Mheshimiwa Spika, linguine, nimwambie tupo tayari kwenda Pemba kuona hali ilivyo na kuona namna ambavyo tunaweza kuziomba fedha kwa haraka ziweze kutatua changamoto hiyo kwa sababu tumepanga sasa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kila mwezi tutakuwa tuna siku tatu za kwenda kufanya ziara Zanzibar ikiwemo Unguja na Pemba kwa ajili ya kuona miradi lakini kuona changamoto kubwa ya athari ya mabadiliko ya tabianchi. Kwa hiyo tuko tayari kwenda Pemba.
Name
Simai Hassan Sadiki
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nungwi
Primary Question
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH K.n.y. MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani kunusuru vipando visivyohimili maji ya bahari katika Bonde la Tibirinzi Chakechake Pemba?
Supplementary Question 2
MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Spika, je, ile dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar juu ya ujenzi wa ukuta maeneo ya fukwe za bahari kule Nungwi imefikia wapi? Ahsante sana.
Name
Khamis Hamza Khamis
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, dhamira ya Serikali zote mbili Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuendelea kutatua changamoto ikiwemo changamoto inayotatiza katika eneo la Kijiji cha Nungwi kama ambavyo Mheshimiwa Simai ameiona. Ninamwambia Mheshimiwa aendelee kuwa na subira, tunatafuta fedha, zitakapopatikana, basi Nungwi tunakwenda kufanya jambo kubwa la ujenzi wa ukuta kwa ajili ya kuzuia maji ya bahari yasiingie kwenye mitaa. Ninakushukuru.
Name
Hamida Mohamedi Abdallah
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Lindi Mjini
Primary Question
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH K.n.y. MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani kunusuru vipando visivyohimili maji ya bahari katika Bonde la Tibirinzi Chakechake Pemba?
Supplementary Question 3
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ninaomba kuuliza swali, Mheshimiwa Naibu Waziri nilishamwomba kuja Lindi kuangalia bahari namna ilivyokula nchi kavu. Sasa, ni lini atakuja Lindi kuangalia ili kutafuta suluhu na kuokoa nchi kavu kwa namna ambavyo inaliwa? Ahsante sana.
Name
Khamis Hamza Khamis
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, niko tayari kwenda Lindi na ninamwahidi sasa tena kwa mara ya mwisho Mheshimiwa Hamida kwamba baada ya Bunge hili, tutakwenda Lindi kwenda kuona changamoto na kuona namna ambavyo tunakwenda kushughulikia changamoto ya maji ya bahari pale Lindi. Kwa hiyo baada ya Bunge hili tutakwenda Lindi. (Makofi)
SPIKA: Ukiwa unamaanisha Jumamosi ijayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, haina maana hiyo, lakini tukimaliza Bunge hili basi tutapanga siku twende Lindi.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved