Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Catherine Valentine Magige

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. CATHERINE V. MAGIGE aliuliza:- Mgogoro wa mipaka kati ya Hifadhi ya Serengeti na Vijiji vya Wilaya ya Ngorongoro ni wa muda mrefu na sasa umekuwa sugu na kusababisha kero kwa wananchi wa maeneo hayo:- Je, ni lini Serikali itaainisha mipaka ya maeneo hayo ili kumaliza mgogoro huu?

Supplementary Question 1

MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nimeona katika jibu la msingi la Naibu Waziri amesema viongozi wa vijiji vya Ngorongoro hawakutoa ushirikiano. Nataka kufahamu, kama viongozi hao hawakutoa ushirikiano ina maana Serikali ndiyo imekata tamaa? Kwa sababu wananchi wale wamekuwa wakipata shida sana, nyumba zao zimekuwa zikichomwa moto na mifugo yao imekuwa ikiuliwa. Nataka jibu la Serikali kuhusiana na kumaliza mgogoro huu wa Ngorongoro. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa migogoro mingi imekuwa ikichangiwa na wafanyakazi wa wanyamapori. Je, Serikali inawachuja vipi maafisa wake wale wasiokuwa na maadili?

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la kwanza kama Serikali imekata tamaa au laa, jibu la moja kwa moja ni kwamba, Serikali haijakata tamaa na wala Serikali haiwezi kukata tamaa katika kushughulikia changamoto ambazo zinawahusu wananchi wake. Kwa nyongeza tu ni kwamba, kwenye jibu langu la msingi nimetaja wilaya ambazo zinahusika na mgogoro ukizihesabu ni wilaya saba.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika wilaya sita mgogoro huu ulishughulikiwa baada ya kupata ushirikiano mzuri kutoka kwa wananchi na Serikali zao za Wilaya na Wizara ya Maliasili na Utalii. Changamoto zilizojitokeza kwenye vijiji hivi vya Wilaya ya Ngorongoro ni kama hivyo nilivyozieleza lakini kama nilivyotangulia kusema hapo awali tumeuorodhesha mgogoro huu ambao unahusu vijiji hivi vya Wilaya ya Ngorongoro kuwa miongoni mwa migogoro ya hifadhi ambayo haijashughulikiwa kikamilifu na nimesema Serikali inaenda kumaliza changamoto hizo katika zoezi linaloenda kufanyika hivi karibuni kimkakati zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili linalohusiana na wafanyakazi wa wanyamapori, nashukuru ameweza kuweka vizuri kabisa kwamba ni baadhi ya wafanyakazi. Jambo la kwanza kabisa wako wafanyakazi walio wengi wa wanyamapori wanafanya kazi zao kwa uadilifu mkubwa na kwa kuzingatia maadili, miiko, kanuni na taratibu na miongozo ya kazi zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wale wafanyakazi wachache ambao wanatumia vibaya nafasi zao, kwa kutumia mwanya wa kutekeleza sheria kwa kuvunja sheria na kufanya vitu ambavyo ni kwa kinyume kabisa na kanuni na taratibu hao wanafanya hivyo wakiwa wanavunja sheria. Kwa hiyo, sasa tunajipanga zaidi kwenda kuwashughulikia mmoja mmoja na kwa makundi ili waweze kukomesha kabisa tabia hiyo na wananchi waweze kutii sheria kwa kuongozwa na kanuni na taratibu na sheria zenyewe badala ya matumizi mabaya ya sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nitumie tu fursa hii pia kutoa wito kwa askari wote wa wanyamapori kwa ujumla wao kwamba wale ambao hawahusiki na vitendo hivi vibaya watumie nafasi zao kuwashauri wenzao lakini wale ambao wana tabia hii wakumbuke tu kwamba katika Serikali ya Awamu ya Tano mambo ya kufanya kazi kwa mazoea, kwamba ulikuwa unafanya namna fulani ulivyozoea tangu huko nyuma sasa imepitwa na wakati na sasa tumefungua ukurasa mpya kabisa wa kutaka kwenda kufanya vitu kwa mujibu wa kanuni na taratibu. Wajiepushe na taratibu za kujificha nyuma ya pazia la utekelezaji wa sheria kuonea wananchi kwa kuwachomea nyumba moto, kuwapiga na vitendo vingine vyote visivyofaa.

Name

Desderius John Mipata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Primary Question

MHE. CATHERINE V. MAGIGE aliuliza:- Mgogoro wa mipaka kati ya Hifadhi ya Serengeti na Vijiji vya Wilaya ya Ngorongoro ni wa muda mrefu na sasa umekuwa sugu na kusababisha kero kwa wananchi wa maeneo hayo:- Je, ni lini Serikali itaainisha mipaka ya maeneo hayo ili kumaliza mgogoro huu?

Supplementary Question 2

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kuniona. Katika Jimbo la Nkasi Kusini kuna Mbuga ya Wanyama inaitwa Rwamfi Game Reserve. Pamekuwepo na migogoro baina ya mipaka yake na Vijiji vya Ng’undwe, Mlambo, King’ombe Kasapa na vinginevyo. Katika michango mingi nimekuwa nikiuliza maswali lakini pia katika mchango wa Wizara hii niliweza kuorodhesha vijiji hivi kwamba vina mgogoro. Je, Waziri anafahamu kwamba mgogoro upo na ni miongoni mwa orodha iliyokwishamfikia kwa ajili ya kusuluhisha migogoro hiyo?

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme tu kwa ujumla kwamba katika migogoro ya ardhi ambayo Serikali imekwishaorodhesha, yote kwa ujumla ni migogoro takribani 289. Miongoni mwao ambayo inahusiana na masuala ya uhifadhi ni migogoro 35, ukifanya hesabu ya haraka pale ni kama asilimia kumi na mbili na nusu ya migogoro yote ya ardhi nchi nzima inahusu uhifadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mgogoro alioutaja kwenye eneo lile jirani kabisa na Katavi kule ni miongoni mwa migogoro ambayo imeorodheshwa kwenye orodha ya migogoro ya hifadhi ambayo tunakwenda kuishughulikia. Naomba nimshauri Mheshimiwa Mbunge baada ya kipindi hiki tuonane ili kwanza nimthibitishie kwamba migogoro hiyo ni miongoni mwa ile iliyoorodheshwa halafu asubiri hatua ambazo Serikali inachukua kushughulikia migogoro yote inayohusiana na masuala ya uhifadhi.

Name

Dunstan Luka Kitandula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkinga

Primary Question

MHE. CATHERINE V. MAGIGE aliuliza:- Mgogoro wa mipaka kati ya Hifadhi ya Serengeti na Vijiji vya Wilaya ya Ngorongoro ni wa muda mrefu na sasa umekuwa sugu na kusababisha kero kwa wananchi wa maeneo hayo:- Je, ni lini Serikali itaainisha mipaka ya maeneo hayo ili kumaliza mgogoro huu?

Supplementary Question 3

MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Hali ya migogoro iliyoko Serengeti na vijiji vya Ngorongoro inafanana na hali iliyopo katika Wilaya yangu ya Mkinga eneo la Kimuni katika mpaka wetu na Kenya na Pori Tengefu la Umba na Mbuga ya Mkomazi. Wananchi kwa muda mrefu wameomba mgogoro huu ili utatuliwe eneo lile litangazwe kuwa WMA lakini kwa muda mrefu hatujapata majibu, nini suluhisho la jambo hili na Waziri anatuambia nini?

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge wote ambao wanaishi kwenye maeneo yanayopakana na hifadhi kila mmoja kwa wakati wake tuweze kupata nafasi ya kuwasiliana ili tuweze kuangalia maeneo yake ambayo anaona yana mgogoro ni kweli yameorodheshwa kwenye orodha ninayoizungumzia ambayo imetayarishwa na Serikali. Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kujibu swali mahsusi la Mheshimiwa Dunstan Kitandula kuhusu eneo la Kimuni, Umba, Mkomazi na hasa kuhusiana na suala la maombi ambayo wameyaleta Serikalini kwa ajili ya kuundwa kwa WMA. Ni kweli WMA inaundwa kwa makubaliano baina ya wananchi wa eneo linalohusika na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii. Sasa nimpe tu comfort Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa suala hili ni mahsusi itakuwa ni vigumu kukumbuka maombi haya kama yameshatufikia tayari na yako kwenye status gani kwa sasa, nimuombe baada ya kikao hiki mchana tuweze kuwasiliana kwa sababu wakati huo mimi nitakuwa nimewasiliana na ngazi zinazohusika ili kuweza kupata uhakika zaidi ya majibu ya status au hatua gani imefikiwa kuhusiana na maombi ya WMA kwenye maeneo anayoyazungumzia.