Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Joseph Michael Mkundi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ukerewe
Primary Question
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:- Je, nini husababisha kuchelewa kubadilishiwa Muundo wa Utumishi kwa Walimu mara baada ya kujiendeleza kitaaluma?
Supplementary Question 1
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini pamoja na majibu hayo kuna ukweli kwamba kuna baadhi ya matatizo kwa watumishi wetu yanasababishwa na uzembe au kukosa weledi kwa baadhi ya Maafisa Utumishi. Kwa mfano, kuna walimu walioajiriwa mwaka 2018 mwezi Aprili, wamepandishwa madaraja mwaka 2021/2022, lakini mwaka huo huo kuna baadhi ya walimu wamepandishwa madaraja mwaka 2023/2024.
Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta kwamba walimu wameajiriwa mwaka mmoja lakini wanatofautiana sana kimuundo na kimaslahi. Je, Serikali haioni kwamba inawakatisha tamaa walimu hawa na kwa hiyo ina wajibu wa kuchukua hatua kufanya marekebisho hayo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kuna walimu walioajiriwa kabla ya mwaka 2018, lakini wana sifa zilezile sawa na wale walioajiriwa mwaka 2018 kuendelea na wamepandishwa madaraja, wale walioajiriwa kabla hawajapandishwa madaraja. Serikali inasemaje katika kuwarekebishia muundo walimu hawa walioajiriwa kabla ya mwaka huu? Ninashukuru. (Makofi)
Name
Deus Clement Sangu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwela
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Joseph Mkundi kwa namna ambavyo anawasemea walimu wa Tanzania, lakini kipekee walimu wake katika Jimbo la Ukerewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu maswali yake yote mawili kwa pamoja, kwanza ninaomba nimwondoe shaka, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, haina nia na wala kwa wakati wowote haitawakatisha tamaa walimu wa Tanzania kwa sababu wanafanya kazi kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jitihada kubwa imefanyika, kwa Mwaka huu wa Fedha 2024/2025, Serikali imetenga bajeti ya shilingi bilioni 252.7 kwa ajili ya kutatua changamoto hizo ikiwemo kuwabadilishia miundo wale waliocheleweshewa na wale ambao walistahili kupandishwa vyeo ambapo Maafisa Utumishi hawakuleta taarifa Ofisi ya Rais Utumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kupitia Bunge hili, nichukue nafasi hii kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kuwaelekeza waajiri kwa maana ya Wakurugenzi, wakishirikiana na TSC, kuhakikisha walimu wote waliosahaulika kwenye suala la miundo na promotion, walete taarifa hizo Ofisi ya Rais Utumishi ili tuweze kutatua changamoto hii. Ninashukuru. (Makofi)
Name
Sophia Hebron Mwakagenda
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:- Je, nini husababisha kuchelewa kubadilishiwa Muundo wa Utumishi kwa Walimu mara baada ya kujiendeleza kitaaluma?
Supplementary Question 2
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kutokana na jibu lake la msingi Mheshimiwa Waziri anasema, walimu wanaenda kujiendeleza bila mwajiri kujua ndiyo maana inakuwa ngumu kwa Serikali kuweza kuwapandisha. Hamwoni kama mnawakatisha tamaa kwa kuwa Serikali haina fedha ya kuwasomesha au kuwaendeleza walimu hao?
Name
Deus Clement Sangu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwela
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Nitoe ufafanuzi, kwenye hili, walimu ninaowaongelea ni wale ambao hawakuomba ruhusa wakajiendeleza bila mwajiri kufahamu, lakini hata hivyo baada ya kujiendeleza Serikali inatambua jitihada kwa kuwa tunaamini mwalimu anapojiendeleza anakuwa na tija katika kazi yake. Kwa hiyo ninaomba nimwondoe shaka Mheshimiwa Sophia kwamba hata hawa baada ya kutambulika, tayari Serikali kama nilivyosema imeandaa bajeti nao watapewa kipaumbele, hakuna mwalimu atakayesahaulika.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved