Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Jackson Gedion Kiswaga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalenga
Primary Question
MHE. JACKSON G. KISWAGA aliuliza:- Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya katika Kata ya Maguliwa ambapo Wananchi wameshakamilisha ujenzi wa Boma?
Supplementary Question 1
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza naishukuru sana Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa zinazofanyika katika Jimbo la Kalenga. Hivi karibuni tumepokea ambulance mbili na vituo vitatu vya afya vimekamilika, kwa sehemu, katika kipindi cha miaka minne. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Katika Kituo cha Maguliwa wananchi wamejenga wodi mbili na imekamilika kwa nguvu za wananchi hasa ambayo nimeuliza. Je, Serikali ina mpango gani ije kumalizia angalau tupate wodi ya wanaume na wanawake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Katika Kituo cha Afya cha Kibena, tunaishukuru Serikali imejenga jengo la wagonjwa wa nje, lakini kuna majengo mengine pale ambayo tayari wananchi wameyajenga miaka mingi kidogo. Je, Serikali haioni haja ya kutuunga mkono, ili tumalizie hayo majengo? Nakushukuru sana.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Jackson Kiswaga kwa kazi kubwa anayofanya ya kuwasemea wananchi wa Jimbo la Kalenga. Namhakikishia kwamba, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa tutaendelea kumpa ushirikiano na ninapokea pongezi ambazo amempa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa hakika Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana katika sekta ya afya, amepeleka magari ya wagonjwa katika halmashauri zote 184 na zipo halmashauri ambazo zimepokea gari la wagonjwa zaidi ya moja na magari ya usimamizi. Zoezi hili linaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kuhusiana na ukamilishaji wa wodi mbili ambazo wananchi wamechangia na ziko hatua ya linta, Serikali tayari imeshafanya tathmini na tumeona kwamba, tunahitaji shilingi milioni 60 kukamilisha zile wodi. Nakuhakikishia kwamba, tunatafuta fedha, tutapeleka kwa ajili ya kukamilisha wodi hizo mbili ili wananchi wa Maguliwa wapate huduma bora za afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, kuhusiana na Kituo cha Afya cha Kibena ambacho majengo yamejengwa hayajakamilika, naomba nitumie nafasi hii kumwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa waanze kutenga fedha za mapato ya ndani kwa awamu ili kuendeleza ujenzi wa majengo hayo wakati Serikali Kuu ikitafuta fedha kwa ajili ya kuunga mkono juhudi hizo za wananchi, ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved