Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Abubakar Damian Asenga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilombero
Primary Question
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: - Je, lini Serikali itamaliza mgao wa umeme unaokatika kila Jumanne na Alhamisi katika Jimbo la Kilombero?
Supplementary Question 1
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa maswali mawili ya nyongeza. Nataka kukiri mbele yako, kwamba lazima tuuseme ukweli kwamba umeme umepungua kukatika na tangu Waziri wa Nishati na Naibu Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Biteko afike Kilombero atoe tamko lile kwamba tuna mgodi wa kuzalisha umeme, umeme usikatike, umeme haujakatika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikiri mbele yako, ukiona umekatika ujue basi yule anayeshika switch amezoea tu kukatakata lakini haukatiki umeme sasa hivi. Tunaishukuru Serikali ya Chama cha Mapinduzi, tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Zaidi ya mara mbili nimeuliza maswali mawili madogo ya nyongeza katika Bunge lako kuhusu bei. Kwangu kunaitwa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, lakini nina vijiji 48. Katika vijiji hivyo 48, kuna maeneo ya vijiji Kata ya Katindiuka na Kata ya Kidatu wanatozwa bei ya mjini kwa sababu ya hilo jina la Halmashauri ya Mji wa Ifakara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, tuliomba Kata ya Katindiuka na Kata ya Kidatu katika hivyo vijiji ambavyo wanatozwa bei ya mjini, warudushiwe bei ya zamani. Je, ni lini Serikali itarudisha bei hiyo? Hilo swali la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, niliiomba Serikali vijiji vyangu 15, nikaleta na orodha kwamba viunganishiwe umeme. Je, ni lini vitaanza kuunganishiwa umeme? Ahsante.
Name
Judith Salvio Kapinga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Asenga amekuwa akifuatilia sana maendeleo na hususan masuala ya umeme katika jimbo lake. Nakiri kwamba ni kweli hizi kata mbili za Kidatu na Katindiuka amekuwa akizifuatilia kwa karibu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ambayo yanapaswa kufanyiwa marejesho kwa Tanzania nzima ni mengi sana. Mwaka 2023 wakati Mheshimiwa Rais anafanya ziara Mtwara, alituelekeza Aizara kwamba tupitie maeneo haya upya ili tuone yale ambayo yanatakiwa kulipa shilingi 27,000 na yale ambayo yanatakiwa kulipa shilingi 320,960. Zoezi hili tumeshalifanyia kazi, tumeshaainisha maeneo 1,500 na kwenye jimbo la Mheshimiwa Mbunge, tumeainisha maeneo 10, lakini nakiri, maeneo ya Kidatu na Katindiuka, bado tunaendelea kuyachakata ili kuona na yenyewe kama yanaweza kuingia katika list ya yale maeneo 10 na yenyewe tuweze kuyaweka katika mchakato wa kupunguza bei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi na Waheshimiwa Wabunge wote, yale maelekezo ya Mheshimiwa Rais tumeanza kuyafanyia kazi. Tumeshaainisha maeneo 1,500 na tunaendelea kufanya hivyo ili baadaye tutafute mafungu kwa ajili ya kubadilisha kutoka shilingi 320,960 hadi shilingi 27,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la pili la vitongoji 15, tunamaliza, tupo katika hatua za mwisho za zoezi la zabuni ili kuweza kumpata mkandarasi kwa ajili ya kuanza kufanya kazi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kabla ya mwezi huu kwisha, tutakuwa tumepata mkandarasi kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa kupeleka umeme katika vitongoji hivi 15, ahsante.
Name
Grace Victor Tendega
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: - Je, lini Serikali itamaliza mgao wa umeme unaokatika kila Jumanne na Alhamisi katika Jimbo la Kilombero?
Supplementary Question 2
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kumekuwa na changamoto kwenye miundombinu ya line za umeme hasa Mkoa wa Iringa na kusababisha kukatikakatika mara kwa mara na hii kuleta adha kwa wananchi wetu. Je, ni lini mtamaliza changamoto hizi ili wananchi waweze kupata umeme wa uhakika?
Name
Judith Salvio Kapinga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa swali la nyongeza la Mheshimiwa Grace Tendega. Suala la kukatikakatika kwa umeme ni kweli linaweza kuwa hivyo kutokana na changamoto ya miundombinu. Kwa kila mwaka wa fedha, tunatenga bajeti kwa ajili ya kurekebisha miundombinu ya umeme kwa ajili ya kupunguza na kumaliza kabisa changamoto ya kukatika katika kwa umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mkoa wa Iringa kwa kiasi kikubwa, tumekuwa tukifanya matengenezo makubwa kwa ajili ya kupunguza kukatikakatika kwa umeme. Mheshimiwa Mbunge ni shahidi, suala la kukatikakatika kwa umeme kwa upande wa Iringa, limepungua kwa kiasi kukubwa sana. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Mkoa wa Iringa, tunaendelea kufanyia marekebisho kwenye miundombinu yetu ya umeme ili kuweza kuiondoa kabisa changamoto hii ya kukatika katika kwa umeme.
Name
Dr. Christine Gabriel Ishengoma
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: - Je, lini Serikali itamaliza mgao wa umeme unaokatika kila Jumanne na Alhamisi katika Jimbo la Kilombero?
Supplementary Question 3
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kukatikakatika kwa umeme katika Jimbo la Kilombero ni sawasawa na kukatikakatika kwa umeme katika Manispaa ya Morogoro. Je, ni lini umeme utaacha kukatikakatika katika Manispaa ya Morogoro?
Name
Judith Salvio Kapinga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Manispaa ya Morogoro, tumekuwa tukiboresha miundombinu na hata pale katika Kituo cha Kupooza Umeme cha Morogoro, tumefanya extension ya kuongeza transformer nyingine kwa ajili ya kuimarisha nguvu ya umeme na kuimarisha upatikanaji wa umeme katika Manispaa ya Morogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kiasi kikubwa katika Manispaa ya Morogoro, kutokana na kuongeza miundombinu hii, tumeweza kupunguza tatizo la kukatikakatika kwa umeme. Kama nilivyosema hapo awali, kukatikakatika kwa umeme ni changamoto ya miundombinu, na kadiri ambavyo tunaendelea kutenga bajeti, tunaendelea kufanya kazi changamoto hii ili mwisho wa siku tuondoe kabisa changamoto hii katika Manispaa ya Morogoro.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved