Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Jesca David Kishoa
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JESCA D. KISHOA aliuliza:- Je, makubaliano ya mkataba ujao kati ya SONGAS na Serikali yamefikia hatua gani ikiwa mkataba wa awali upo katika mwaka wa mwisho?
Supplementary Question 1
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, taarifa za CAG pamoja na Kamati za Kudumu za Bunge toka mwaka 2009 zimekuwa zikieleza mapungufu makubwa yaliyopo kwenye mkataba wa SONGAS, nataka kujua Serikali ilishachukua hatua gani kwa GNT (Government Negotiation Team) ya wakati huo ili ya sasa Government Negotiation Team isifanye makosa yale.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, chanzo cha Tanzania kupata alama ya chini kwenye tathmini ya EIT ya mwaka 2023 ni kutokana na mikataba kutowekwa wazi kinyume na sheria ya Tanzania Extractive Industry Transparency Act ya Mwaka 2015. Nataka kujua Serikali ni lini mtaleta mkataba huo Bungeni, sisi kama Wabunge tuujadili kabla ya kuusaini. Ahsante. (Makofi)
Name
Judith Salvio Kapinga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mawili ya nyongeza, kwanza kuhusiana na hii timu ya wataalamu. Mwaka jana mwezi Aprili timu ya wataalam iliundwa na walipewa jukumu la kuchambua mikataba yote ya Mradi wa SONGAS ikihusisha mikataba ya msingi (basic agreements) vilevile mikataba ya fedha (financial agreements).
Mheshimiwa Spika, ilivyofika mwezi Disemba tulianza majadiliano, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako hili Tukufu kwamba, timu hii ya wataalamu ambayo imewekwa kwa ajili ya majadiliano ya nyongeza ya mkataba wa mauziano ya umeme kati ya TANESCO na SONGAS na mikataba mingine ambayo inahusiana. Ni timu ya wataalamu wenye weledi mkubwa sana na imehusisha maeneo yote ya msingi, lengo kuu ni kuhakikisha hatufanyi makosa yoyote tunapoenda kwenye mikataba ya namna hii.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la pili la mikataba kuwa wazi, kwa sababu sasa hivi hatujafahamu kama tutaendelea na mkataba huu ama hatutaendelea na mkataba huo, inaniwia vigumu kusema ni lini tutaleta mkataba huo Bungeni lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, section 16 ya Sheria ya Extractive Industry ni kweli inataka uwazi kwenye mikataba na leseni za sekta ya uziduwaji na sisi kama Serikali tunahakikisha mara zote tunaenda kwa mujibu na matakwa ya sheria hizo. Kwa hiyo nimhakikishie kama tutafikia hatua hiyo basi tutawajibika kulingana na sheria. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved