Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Juma Selemani Nkamia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Primary Question

MHE. JUMA S. NKAMIA aliuliza:- Je, Serikali itakamilisha lini ukarabati wa Mradi wa Maji wa Ntomoko ili kuwaondolea wananchi adha ya ukosefu wa maji kwenye vijiji vya Sambwa, Kirikima, Churuku, Jangalo, Jinjo, Hamai, Songolo na Madaha?

Supplementary Question 1

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niishukuru sana Serikali ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuleta hizi fedha haraka na kujua umuhimu wa wananchi wa Chemba na Kondoa kutokana na tatizo hili la maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ningeomba hizi shilingi milioni 600 anazosema Mheshimiwa Waziri, ziliingia akaunti ya DAWASCO Dodoma toka Januari mwaka jana, mpaka leo hiyo fedha haijaingia katika Halmashauri ya Kondoa. Je, yuko tayari sasa, kusukuma ili fedha hii iingie kati ya leo na kesho?
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ucheleweshwaji wa miradi mingi ya maji umechangiwa sana na flow ya fedha kutoka Hazina kwenda kwenye Halmashauri. Je, Wizara sasa iko tayari kupeleka fedha hizi haraka ili miradi mingi nchini iweze kukamilika hasa hii ya maji ambayo wakandarasi wengi wameanza kutishia sasa kwenda Mahakamani?

Name

Eng. Isack Aloyce Kamwelwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Katavi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata taarifa kwamba hizo fedha zimekwama Mamlaka ya Maji Dodoma (DUWASA). Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba nitafuatilia kuhakikisha fedha hizo zinapelekwa Kondoa, lakini ndiyo umekuwa utaratibu kwamba fedha zikitolewa kwanza zinaanzia DUWASA, baadaye ndiyo zinakwenda huko kwenye kazi.
Hoja ya pili ya Mheshimiwa Mbunge, sasa hivi tunaingia katika awamu ya pili ya programu ya maji. Miradi mingi haikukamilika kwa sababu ya matatizo ya kifedha, lakini sasa tunaanza programu ya pili na hii programu ya pili tayari tunaanza kupata pesa na Serikali itatenga fedha ili kuhakikisha miradi yote iliyokuwa inaendelea inakamilika na miradi ambayo ilikuwa haijaanza inaanza. Pia tunatarajia kuwa na miradi mipya kulingana na upatikanaji wa fedha ili kuhakikisha tunapunguza hili tatizo la maji.