Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. Jasson Samson Rweikiza
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Vijijini
Primary Question
MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:- Bukoba Vijijini kuna Shule za Sekondari za Serikali na za Wananchi zipatazo 29 ambazo zinaishia Kidato cha nne na moja kati ya hizo ina Kidato cha tano na sita hali, inayosababisha wahitimu wengi wanaomaliza Kidato cha nne wakiwa na sifa za kuingia Kidato cha tano kukosa nafasi:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga madarasa na miundombinu inayofaa kwa Kidato cha tano na sita kwenye baadhi ya shule zilizopo ili kutatua tatizo hilo?
Supplementary Question 1
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Ni dhahiri kama Mheshimiwa Naibu Waziri alivyosema kuna shule 29 za sekondari ambazo ni nyingi kwa shule moja ya form five na six. Hiyo shule moja ya form five na six sasa hivi haipo tena, baada ya tetemeko la ardhi imeharibika kabisa na imefungwa. Sasa Serikali haioni kwamba umuhimu umeongezeka baada ya shule hii kuharibika kabisa kuharibiwa na tetemeko la ardhi, kwamba juhudi zifanywe za ziada kujenga shule ya form five na six?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa vile shule ya namna hii ni shule ya Kitaifa kwa nini jambo hili wanaachiwa halmashauri ndio washughulike nalo kutafuta fedha, kujenga wenyewe na isijengwe na Serikali Kuu?
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunajua kwamba, pale hali imekuwa ni mbaya na hasa katika ile shule ambayo imeporomoka zaidi, na hata hii Shule ya Lubale karibu nyumba mbili zimehaibika pamoja na baadhi ya madarasa. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali italiwekea hili kipaumbele. Na ndiyo maana katika Mfuko huu wa Maafa ya Mkoa wa Kagera maeneo ya elimu tumeyapa kipaumbele cha kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, ile shule iliyoharibika tutaijenga upya yote, lakini halikadhalika hii shule ya Lubale tutaweka nguvu kubwa sana kuhakikisha kwamba majengo yanarudi katika hali yake nzuri, ili vijana ambao wanasoma wapate elimu. Vile vile juhudi za Serikali kwenye janga hili ambalo limeupata Mkoa wa Kagera zitakuwa ni kupeleka nguvu za kutosha katika taasisi zote zilizopata uharibifu mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake linalohusu shule hizi kuwa ni shule za kitaifa na kwamba kwa nini inaachiwa Halmashauri? Ni kweli na ndiyo maana tumetoa maelekezo kwamba kila halmashauri ifanye hivyo kwa sababu wote tunaunga mkono nguvu moja nguvu ya Kitaifa na ndiyo maana hata mpango wa Serikali wa uwezeshaji wa shule mbalimbali mwaka huu ni kuhakikisha tunaboresha zile shule za Kitaifa, lakini pia kuongeza nguvu kwenye zile za wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo naomba nimpongeze sana ndugu yangu Mheshimiwa Rweikiza kwa juhudi kubwa anayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika kwa upekee niwapongeze wananchi wa Mkuranga, nimpongeze Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Mkuu wa Mkoa wa Pwani pamoja na Mbunge wa Mkuranga kwa kuwahamasisha vijana wapatao 53 watengenezaji wa matofali mapya karibu 45,000. Naomba niwasihi Wakuu wote wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, mambo haya ni mambo ya kuigwa tufanye hayo kwa ajili ya maslahi ya Taifa letu.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Jafo nilipenda niongezee kwenye eneo lifuatalo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kisera kila Kata inakuwa na shule ya sekondari ya kidato cha kwanza mpaka cha nne, lakini kwa kidato cha tano na cha sita, shule hizi zina umaalum wake na ni lazima ziwe na vigezo ambavyo vimeelezwa kwa mujibu wa sheria na si lazima kila eneo kuwa na shule yake ya kidato cha tano na cha sita, Kwa sababu hakuna mtoto aliyefaulu kwenda kidato cha tano ambaye atakosa nafasi kwa shule zetu tulizonazo nchini; kubwa hapa ni ubora wa shule hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme tu kwamba Mheshimiwa Rweikiza kama wao wana mpango wa kujenga shule ya kidato cha tano na cha sita waje tutawapa vigezo vinavyotakiwa ili tusirudi kwenye makosa yaliyopita ili tuweze kujenga shule zenye sifa zinazostahili kwa ajili ya kidato cha tano na cha sita, kwa sababu hata tulizoanza nazo nyingine bado zina changamoto nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge na wawakilishi wa maeneo yote kuhakikisha kwamba tunapotaka kuanzisha shule ya kidato cha tano na cha sita basi vigezo vyote vile vya msingi vizingatiwe ikiwepo kwanza uwepo wa umeme, uwepo wa maji maeneo husika, majengo yanayostahili lakini na mazingira yanayoweza ku-accommodate masomo ya watoto wa kidato cha tano na cha sita.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved