Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Sixtus Raphael Mapunda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbinga Mjini
Primary Question
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA aliuliza:- Hospitali ya Wilaya ya Mbinga inatoa huduma kwa Halmashauri Nne yaani Mbinga Mjini, Mbinga Vijijini, Nyasa na baadhi ya Kata za Songea Vijijini, hali inayopelekea Hospitali hiyo kuwa na upungufu wa vitendeakazi, wodi na vyumba vya kulaza wagonjwa pamoja na ukosefu wa Madaktari Bingwa:- Je, ni lini Serikali itaboresha Hospitali hiyo ili iweze kutoa huduma inayotarajiwa?
Supplementary Question 1
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri hasa eneo la kutoa milioni 50 kwa ajili ya wodi ya watoto, nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza ni lini Serikali itaboresha wodi ya akinamama wajawazito pamoja na sehemu ya kujifungulia hasa ukizingatia hali ya sasa pale hospitalini, akinamama wanakaa katika mazingira magumu na wanalala watatu watatu? (Makofi)
Swali la pili la nyongeza; kama nilivyoeleza kwenye swali la msingi, Hospitali ya Wilaya ya Mbinga inahudumia Halmashauri nne, yaani Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, Mbinga Vijijini, Mbinga Mjini na sehemu ya Halmashauri ya Songea Vijijini. Gari ambalo limetolewa na waterreed liko kwa ajili ya kitengo cha UKIMWI na linawasaidia wale wagonjwa wa UKIMWI tu, maeneo kama ya Mpepai kwenye zahanati na vituo vya afya Kihungu, Kilimani, Kigonsera, Mkumbi ambao hao wakipata mazingira magumu katika maeneo yao wanahitaji kuletwa katika hospitali ya Wilaya. Ni lini Serikali itatuletea gari la wagonjwa kwa sababu hilo lililosemwa hapa haliko kwa ajili ya kuwasafirisha wagonjwa wa hali ya kawaida, ni wale tu kwenye kitengo cha UKIMWI?
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MTAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kujali afya za akinamama na watoto katika eneo hilo, nikiri wazi kwamba kwa umahiri wako nadhani tutafika vizuri. Naomba nimhakikishie katika suala la wodi ya akinamama na watoto kipaumbele cha Serikali hivi sasa ni kuimarisha afya za jamii hasa akinamama na watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kumbukumbu yangu siyo muda mrefu tulikuwa na mkutano mkubwa sana hapa wa Madaktari wa Mikoa na Wilaya na bahati nzuri mkutano ule alikuwepo Makamu wa Rais wetu kama mgeni rasmi, mambo makubwa sana yameahidiwa pale. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mchakato wa bajeti wa mwaka huu unaokuja tutaangalia jinsi gani tutashirikiana nao kuhakikisha kwamba tunaweka kipaumbele katika wodi ya wazazi katika hospitali yetu ya Mbinga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika suala la gari la wagonjwa, ni kweli nafahamu katika hospitali mbalimbali siyo ya kwake peke yake isipokuwa hospitali nyingi sana changamoto za gari za wagonjwa zimekuwa ni kubwa. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Ofisi yangu itashirikiana naye kutafuta uwezekano wa aina yoyote japokuwa siwezi kuwaahidi hapa sasa, kwa sababu najua jambo kubwa sana linalotukwamisha ni ukomo wa bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango mkakati mpana ambao tunauandaa hivi sasa naomba tujadiliane kwa karibu zaidi jinsi gani tutafanya, lengo kubwa ni kuwasaidia wale watu ambao catchment area yake ni kubwa zaidi, tutafanya vipi kama Serikali, tukishirikiana na Mbunge na wadau mbalimbali kuwawezesha wananchi wa eneo hili kufika sehemu za referral ambazo zimekusudiwa katika eneo lake. Ahsante sana
Name
Catherine Valentine Magige
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA aliuliza:- Hospitali ya Wilaya ya Mbinga inatoa huduma kwa Halmashauri Nne yaani Mbinga Mjini, Mbinga Vijijini, Nyasa na baadhi ya Kata za Songea Vijijini, hali inayopelekea Hospitali hiyo kuwa na upungufu wa vitendeakazi, wodi na vyumba vya kulaza wagonjwa pamoja na ukosefu wa Madaktari Bingwa:- Je, ni lini Serikali itaboresha Hospitali hiyo ili iweze kutoa huduma inayotarajiwa?
Supplementary Question 2
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza.
Kwa kuwa wananchi wa Kata ya Kitumbeini na Namanga, Wilayani Longido, Mkoa wa Arusha wamekuwa hawapati huduma ya afya, hakuna vituo vya afya imefikia hata wanavuka mipaka kwenda nchi jirani ya Kenya kwa ajili ya kupata matibabu. Je, Serikali ina mpango gani kuwasaidia wananchi hawa waondokane na tatizo hili ukizingatia Wilaya ya Longido haina hata hospitali ya Wilaya.
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MTAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nyakati mbalimbali nilikuwa nikirejea kwamba ni kweli katika vituo vya afya tunavyohitajika kuvipata sasa hivi bado tuna upungufu mkubwa sana.
Katika mpango mkakati wetu sasa hivi tumejielekeza kwamba at least kila Halmashauri tuweze kuwa na hospitali ya Wilaya na katika hili naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, nakumbuka jambo hili muda mrefu sana linapigiwa kelele na kweli haipendezi, katika eneo hili wananchi wanakosa huduma mpaka wanakwenda nchi za jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali, lakini kama Halmashauri ya eneo hilo, nitaomba katika mchakato wa bajeti ya mwaka huu unaokuja kwa sababu tumeweka kipaumbele na kila Halmashauri tuna mpango mpana ambao tutakuja kuu-present baadaye hapa, at least tuwe na kituo cha afya katika kila Wilaya kwanza, kituo cha afya kimoja kimoja kwanza na umaliziaji wa magofu. Nadhani Wilaya ya Longido tutaipa kipaumbele hasa katika Kata ambayo ameikusudia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie, Serikali haitawatupa na iko tayari kushirikiana na wananchi wa Longido na kushirikiana na Mbunge ambaye yuko mahiri kutetea eneo hilo.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved