Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Primary Question

MHE. DAVID E. SILINDE aliuliza:- Wakati wa Kampeni za Urais mwaka 2015 wananchi wa Momba walipewa ahadi ya kutatuliwa kero ya ushuru wa mazao na mifugo kwenye vizuizi na minada:- (a) Je, mpaka sasa Serikali imefikia hatua gani katika kushughulikia kero hii? (b) Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya mwenendo mbovu wa ukusanyaji wa ushuru huo?

Supplementary Question 1

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, ningependa kuuliza maswali mado mawili.
Moja ya kero inayowakuta wafugaji wanapokuwa minadani, inatokea mahali mtu amekwenda kuuza bahati mbaya akiwa pale mnadani hajauza mfugo wake, na anapotoka pale anadaiwa ushuru wakati hajapata hiyo fedha. Sasa nilitaka nifahamu kauli ya Serikali juu ya wale wote ambao wanashindwa kuuza mazao ama mifugo yao katika maeneo hayo?
Swali la pili, je, ni kiwango gani ambacho mtu anapaswa kulipa, kwa sababu kuna watu wanatoka mashambani labda ana mahindi wanakwenda nyumbani kwao kuyatunza. Sasa wakikutana na kizuizi, mtu ana gunia mbili, gunia tatu anaambiwa lazima alipe ushuru hata kwenye yale mahindi ya kutumia.
Je, ipi ni kauli ya Serikali juu ya hili jambo? Ahsante.

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI (TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika mazoea ya kawaida watu wengine wanapeleka mazao yao sokoni, lakini kwa bahati mbaya wakifika pale wanakosa kuyauza. Ina maana na concept ya ushuru wa mazao, maana inataka mtu akishauza, yule mnunuzi sasa maana yake anatakiwa alipia ule ushuru. Lakini kama hajauza ukimwambia kwamba yule mkulima sasa aweze kutoa ushuru maana yake unambana mkulima. Na kauli ya Mheshimiwa Rais alipokuwa katika kampeni alizungumza wazi kwanza lengo lake ni kutoa huu usumbufu wa ushuru mdogo mdogo ambao unamkabili mwananchi wa kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa zaidi nawahimiza Watendaji wetu hasa katika Halmashauri, jinsi gani wabainishe kwamba katika maeneo yao kuna watu hawa wa kawaida ambao wanaenda kuuza. Kuna mfanya biashara mkubwa ambaye anakuja kuchukuwa mazao pale site, akishachukua lazima alipie ushuru. Lakini yule mtu anayefanya kazi ya kuchuuza kwa ajili ya maisha yake tu hili ni jambo ambalo ni suala zima kuwaelekeza watendaji wetu katika Halmashauri zetu watafanya vipi kuondoa kero hii kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ni kwa kiwango gani, nadhani suala la pili sikulipata vizuri lakini kikubwa zaidi ni nini. Ni kwamba mifugo yote inayopelekwa pale eneo la mnada, ndiyo maana nimesema sijalipata vizuri swali la pili, tuangalie kwamba kwa sababu sheria ndiyo inaelekeza kati asilimia tatu mpaka asilimia tano, sasa mtu anapoenda kuuza mfano ana ng’ombe wake mmoja, ng’ombe wake wawili, ndiyo nimesema hapa utaratibu mkubwa unaotakiwa ni katika Halmashauri husika. Kwa sababu tunajua Halmashauri nyingine zinategemea asilimia karibuni 70 ya mapato yake katika ushuru wa mazao.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jinsi gani kama Baraza la Madiwani pamoja na Watendaji wao watafanya kuangalia mazingira ya kijiografia katika eneo husika ili kuwasaidia wananchi hali kadhalika kuongeza uchumi katika Halmashauri zao.

Name

Suleiman Ahmed Saddiq

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mvomero

Primary Question

MHE. DAVID E. SILINDE aliuliza:- Wakati wa Kampeni za Urais mwaka 2015 wananchi wa Momba walipewa ahadi ya kutatuliwa kero ya ushuru wa mazao na mifugo kwenye vizuizi na minada:- (a) Je, mpaka sasa Serikali imefikia hatua gani katika kushughulikia kero hii? (b) Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya mwenendo mbovu wa ukusanyaji wa ushuru huo?

Supplementary Question 2

MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi, naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa katika Halmashauri zetu, hususani Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kumekuwepo na tatizo kubwa sana la ushuru huu na unaleta matatizo makubwa na kwa kuwa kuna ahadi ya Rais kwamba hizi shughuli ndogondogo zitaangaliwa upya, je, Serikali sasa iko tayari kuziagiaza Halmashauri zote ziangalie upya maeneo ambayo kuna usumbufu mkubwa na ushuru huu, ili marekebisho yafanywe haraka na wananchi wasipate bugudha ikiwemo Wilaya ya Mvomore?

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu yake ya ufasaha, na mimpongeze Mheshimiwa Murad kwa ufuatiliaji wake kwa masuala yanayohusu Jimbo lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba kama ambavyo nilisema wakati nachangia, tunakaa na wenzetu wa TAMISEMI pamoja na Wizara zingine ambazo zinahusiana na sekta ambazo zinahusu mambo ya makato makato na tulishasema tunayafanyia kazi mambo ya makato yote ambayo yanamgusa Mkulima na wafanyabiashara wadogowadogo. Lakini kwa leo nitamke tu kwamba kwa yale makato ambayo hayako kisheria, kwa makato ambayo yanawagusa wakulima ambayo hayako kisheria kuanzia leo hii wale wanaohusika waondoke na tamko hili kwamba wayaache, yale ambayo yako kisheria tunaenda kufuata utaratibu na kuangalia kama yote yabaki ama yabaki kiasi ili kuweza kuhakikisha kwamba tunawapa unafuu wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini yale hayako kisheria na yale ambayo hayahusiani moja kwa moja na uendelezaji wa zao husika hayo yakome moja kwa moja kufuatana na kwamba yamekuwa yakiwapa mzigo wakulima bila kuleta tija katika kuongeza uzalishaji wa zao husika. Na tutachambua moja baada ya lingine na yale ambayo yanaafikiwa kwa kupitia makubaliano ya wadau wahusika, wasikubaliane wao na kuanza kuyatumia mpaka wapate ridhaa ya Wizara kwamba kuna mambo haya wamekubaliana na sisi tuweze kupima umuhimu wa kuwepo makato hayo katika uendelezaji wa zao husika. (Makofi)