Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Jitu Vrajlal Soni
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Babati Vijijini
Primary Question
MHE. RIZIKI S. MNGWALI aliuliza:- Kumekuwa na tatizo sugu nchini kwa baadhi ya vituo vya afya na zahanati kuwa na watumishi wasio na sifa za utabibu:- Je, Serikali inatumia vigezo gani kuwapeleka watumishi wasio na sifa katika zahanati na vituo vya afya?
Supplementary Question 1
MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuiuliza Serikali, je, katika maeneo ambapo sisi kama wananchi na viongozi tumejitahidi, kwa mfano, Kituo cha Afya Magugu tumeweza kuwekeza vifaa mbalimbali ambavyo ngazi hiyo haina mpango au kwa mpango wa Serikali haipeleki wataalam wa aina hiyo, kwa mfano, tuna ultra-sound na vifaa vya macho. Je, Serikali itakuwa tayari mahali ambapo sisi wananchi tumewekeza vifaa mbalimbali ituletee wataalam wa ngazi hiyo? Kwa mfano, Kituo cha Afya Magugu watuletee Madaktari wa Upasuaji wa Macho na wa Ultra-sound kwa sababu vifaa vyote tunavyo na havitumiki. Inabidi tuombe wataalam kutoka mkoani wawe wanakuja mara moja kwa wiki kutusaidia. Je, Serikali itakuwa tayari kutusaidia wataalam hawa?
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Answer
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nikiri miongoni mwa Wabunge ambao wanafanya kazi kubwa ni Mheshimiwa Jitu Soni. Mwaka juzi nilikuwa ni shahidi Detros Group ya Arusha imesaidia vifaa vyote kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Magugu. Kwa hiyo, juhudi hii amefanya Mbunge akashirikiana na wadau wenzake kutoka Arusha lakini kusaidia Mkoa wa Manyara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikiri katika mgao wa mwaka huu zoezi kubwa tunalokwenda kufanya, juzi nilijibu swali hapa kwamba mwaka huu mkakati wa Serikali ni kuajiri watumishi wapya wa afya 10,780. Katika watumishi hao wapya ambao tunakwenda kuwaajiri, naomba nikuambie Mheshimiwa Jitu Soni; Kituo cha Afya cha Magugu kitapewa kipaumbele kwa sababu wananchi wa Manyara, Babati Vijijini mmefanya kazi kubwa, lengo letu akinamama wapate huduma bora pale. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nitoe tu majibu ya ziada kwamba Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jami ipo kwenye mchakato wa kutengeneza utaratibu wa kuwasainisha mikataba maalum watumishi wote ambao wataajiriwa kuanzia sasa kwa kipindi maalum, kama miaka mitatu ama miaka mitano ili wasiondoke kwenye maeneo ya pembezoni kama ilivyo kwenye Kituo cha Afya cha Magugu.
Name
Riziki Shahari Mngwali
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. RIZIKI S. MNGWALI aliuliza:- Kumekuwa na tatizo sugu nchini kwa baadhi ya vituo vya afya na zahanati kuwa na watumishi wasio na sifa za utabibu:- Je, Serikali inatumia vigezo gani kuwapeleka watumishi wasio na sifa katika zahanati na vituo vya afya?
Supplementary Question 2
MHE. RIZIKI S. MNGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na kwa niaba ya wananchi wa Mafia niulize maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa majibu ambayo hayatoshelezi sana, namuuliza Mheshimiwa Waziri kama ataichukulia kesi ya Mafia kuwa ni special case ambayo inahitaji kushughulikiwa kwa haraka? Hili liko katika zahanati ya Chemchem ambapo zahanati imepewa jukumu la kuwa kituo cha afya kwa maana ya kushughulikia vijiji zaidi ya kimoja lakini ina mhudumu wa afya badala ya tabibu ambaye anahudumia wananchi. Je, analichukulia jambo hili kuwa ni suala la dharura na kwa hiyo atupatie tabibu haraka iwezekanavyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ataichukulia pia kama ni special case Zahanati ya Chunguruma ambapo pamoja na kumuweka Mkunga mwenye sifa lakini ni mwanaume. Je, atatupelekea haraka Mkunga mwanamke katika Zahati ya Chunguruma ili wanawake wa Mafia wapewe huduma stahiki? Ahsante.
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Answer
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeisikia changamoto hii na umezungumzia Zahanati ya Chechem na Chunguruma. Kama nilivyosema pale awali, ni kweli, ukiangalia Mafia ina Hospitali ya Wilaya na tuna zahanati takriban 16. Changamoto yake ni kwamba zinazo-function vizuri ni zahanati tano. Kwa hiyo, tuna upungufu mkubwa zaidi katika zahanati zipatazo 11.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili nini cha kufanya sasa, ndiyo maana Wilaya ya Mafia sasa hivi imepewa kibali cha kuajiri watumishi wapatao 18 lakini katika hilo kipaumbele cha awali ni kuajiri Clinical Officers ili ku-cover maeneo yale ambayo tunaona kuna watu ambao hawastahili kufanya hizo kazi lakini kutokana na changamoto iliyopo wanafanya kazi ambazo ziko nje ya kada yao. Kwa hiyo, tunalifanyia kazi hilo suala hilo na tunaishukuru Ofisi ya Utumishi imeshatupatia kibali. Si muda mrefu sana baada ya ajira hiyo watumishi hao wataweza kufika katika zahanati hizo ili waweze kutoa huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika hili tumejielekeza, asubuhi tulikuwa tunawasiliana na RAS wetu wa Mkoa wa Pwani. Changamoto ya jiografia ya Mafia utakuta watumishi wengi sana wakipangwa wengine wanasuasua kufika. Tumeelekezana na RAS wa Mkoa wa Pwani kuhakikisha watumishi wote wanaotakiwa kufika Mafia hasa katika sekta ya afya waweze kufika ili wananchi wote wanaotakiwa kupata huduma waweze kupata huduma. Lengo letu kama Serikali ni kuhakikisha afya hasa ya mama na mtoto inalindwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya kwamba mhudumu mwanaume ndiye anayetoa hiyo service, tumelichukua hili. Nadhani ni angalizo kwa sisi watu wa Serikali japokuwa watu wa afya hasa Madaktari kazi zao wanafanya sehemu zote lakini tunatoa kipaumbele kwa akinamama. Inawezekana magonjwa mengine anapohudumiwa na baba inakuwa ni changamoto kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tulichukue hili na nimwelekeze RAS wetu wa Mkoa wa Pwani kuhakikisha kwa haraka anafanya juhudi iwezekanavyo kupeleka Madaktari au wahudumu wanawake katika zahanati hii ambayo inaonekana ina changamoto kubwa ili hata mtu akienda katika zahanati ile akiwa mwanamama aone kwamba sitara yake imesitirika. Nashukuru sana.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved