Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Maulid Said Abdallah Mtulia
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kinondoni
Primary Question
MHE. MAULID S. MTULIA Aliuliza:- Taifa lina tatizo kubwa la ukosefu wa ajira rasmi kwa vijana. Vijana wa Jimbo la Kinondoni wameamua kujiajiri katika sanaa mbalimbali kama vile maigizo, maonesho ya mitindo na michezo mbalimbali:- (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaongezea vijana hawa vifaa, mitaji na menejimenti ili kuongeza tija katika kazi zao; (b) Je, Serikali imefikia wapi katika suala la hatimiliki ili Wasanii, Wanamichezo na Wanamitindo wetu waweze kupata haki zao.
Supplementary Question 1
MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu hivi sasa imekuwa soko holela la kazi za wasanii ambazo zinaingizwa kiujanja ujanja
bila kufuata taratibu wala Serikali yetu kupata kodi kwa mujibu wa sheria, pia wasanii wengi wana malalamiko makubwa kwamba kazi zao zinazotumiwa na makampuni ya simu hawalipwi ipasavyo. Vilevile, wasanii wana
manung’uniko mengi kwamba kazi zao za sanaa wanapokwenda kuziuza wanadhulumiwa na wanapewa kwa bei chee. Je, ni lini sasa Serikali itaamua kuleta mabadiliko ya sheria hizi ambazo Naibu Waziri amezitaja, Sheria Na. 7 ya Mwaka 1999, Sheria Na. 4 ya Mwaka 1976 na Sheria Na. 23 ya Mwaka 1984. Sheria hizi zote zinaonekana zina miaka mingi haziendi sawa na mabadiliko ya kasi yanayokwenda katika sanaa yetu Tanzania. (Makofi) Swali la pili; je, Mheshimiwa Naibu Waziri, yuko tayari kuambatana nami kwenda kukaa na wasanii ili tuwasikilize matatizo yao na tuweze kushirikiana nao ili kuwapatia ufumbuzi na kuhakikisha kazi zao zinaleta tija kama ilivyokuwa kwa wasanii wa nchi nyingine?
Name
Anastazia James Wambura
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kama alivyosema ni kweli
kwamba sheria zetu hizi zinazohusiana na usimamizi wa masuala ya sanaa na wasanii kwa ujumla zimepitwa na
wakati, kwa sasa tunachokifanya ni kuandaa sera kwanza kwa sababu tulikuwa hatuna Sera ya Sanaa, tulikuwa na Sheria ya Filamu lakini hatukuwa na Sera. Kwa hiyo, kwa sasa tunaandaa Sera ya Filamu na vilevile tunaandaa Sera ya Maendeleo ya Sanaa.
Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilisha sera hizi ambapo Sera ya Filamu tunatarajia kufikia mwishoni mwa mwezi wa Sita tuwe tumekamilisha kuandaa rasimu yake na baada ya kukamilisha sasa tutahuisha hizi sheria ili kusudi ziweze kuendana na wakati.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili; kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru na niseme kwamba tuna kila
sababu ya kumshukuru Mheshimiwa Rais na kumpongeza kwa kuanzisha Idara ya Sanaa katika Wizara yetu. Nia hasa ni kuhakikisha kwamba tunaongeza kasi ya maendeleo ya tasnia ya sanaa.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kuambatana naye kwenda katika Jimbo lake, nimekubaliana na hili. Hata hivyo
napenda kumjulisha kwamba Wizara yetu imeanzisha utaratibu kupitia utaratibu wa wadau tuzungumze. Kila
Jumanne tunaongea na wadau wa sekta zetu nne; Sekta ya Habari, Sekta ya Sanaa, Sekta ya Utamaduni pamoja na Sekta ya Michezo. Kwa hiyo, huwa tunaongea na wadau ili kupata changamoto na kupanga ni jinsi gani tuweze kutatua changamoto hizi.
Mheshimiwa Spika, hivyo nichukue nafasi hii kuwaalika wasanii wote pale ambapo tutakuwa tukizungumzia masuala yao siku ya Jumanne fulani kwa mwezi basi waweze kuhudhuria pale Dar es Salaam na hapa Dodoma. Maalum kwa Jimbo lake la Kinondoni, Wizara yangu iko tayari na binafsi niko tayari kuambatana naye ili tuweze kusikiliza matatizo ya wasanii. Mheshimiwa Spika, ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved