Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
George Malima Lubeleje
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpwapwa
Primary Question
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:- Kila mwaka Bunge limekuwa likipitisha Bajeti ya Serikali kuhusu Wizara, Mikoa na Wilaya lakini kumekuwa na ucheleweshwaji wa fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo hususan katika Mikoa na Wilaya na kupelekea miradi mingi kutokamilika. Je, ni sababu gani za msingi zinazofanya Serikali kuchelewa kuleta fedha za Miradi ya Maendeleo katika Mikoa na Wilaya?
Supplementary Question 1
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha, nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa kuna miradi imeshaanza kutekelezwa, kwa mfano, Wilaya ya Mpwapwa tulikuwa na matarajio ya kujenga barabara za lami, Mpwapwa Mjini kilometa 10; na kwa kuwa fedha iliyoletwa ni kidogo sana na ni karibu Majimbo yote kuna viporo; je, fedha iliyobaki Serikali italeta fedha zote kwa Wilaya zote? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa fedha zinazotengwa kwa ajili ya kujenga Vituo vya Afya Mima na Mbori ni kidogo sana na ndiyo maana havijakamilika sasa zaidi ya miaka kumi; je, Serikali itaongeza fedha ili tukamilishe vituo hivyo?
Name
Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kondoa
Answer
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Lubeleje kwa jitihada zake za kufuatilia maendeleo ndani ya Mpwapwa na ndani ya Wilaya nzima ya Mpwapwa, wananchi wako wanakutegemea sana kaka yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ni kupelekwa fedha zote. Kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, upelekaji wa fedha hutegemea mapato ya Serikali na hivyo fedha hizi zinapopatikana, lengo la Serikali ni kuhakikisha bajeti yetu inatekelezeka kwa asilimia 100. Kwa hiyo, fedha hizi tutakapokuwa tumezipata fedha zote zitapelekwa na miradi yote tuliyopanga itatekelezwa kama ambavyo tulipitisha bajeti yetu.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili la Vituo vya Afya kuongeza bajeti, ni imani yangu Wizara ya Afya watakapoleta bajeti yao hapa tutaiona na tumelizingatia hilo, vituo vyote vya afya ambavyo vimejengwa miaka mingi havijakamilika tumevizingatia katika bajeti yetu ya mwaka huu 2017/2018.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved