Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Primary Question

MHE. JORAM I. HONGOLI aliuliza:- Waathirika wa UKIMWI katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe wamekuwa wakipoteza maisha haraka zaidi kutokana na kutembea umbali mrefu kwenda kupata huduma za matibabu. Je, ni lini Serikali itaongeza bajeti ya ujenzi, vifaa tiba na dawa katika kila kijiji na vituo vya afya kwa kila kata?

Supplementary Question 1

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa dawa za kurefusha maisha kwa waathirika hawa wa UKIMWI zimekuwa zikitolewa kwenye vituo vya afya na kwenye zahanati chache. Kwa nini sasa Serikali isitoe huduma hizi kwenye zahanati zote ili kuwapunguzia wananchi hawa ambao wameathirika kutembea umbali mrefu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, waathirika hawa
au hawa watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI wanaoishi vijijini sehemu kubwa ndiyo waathirika pia kwa maana ya umaskini. Kwa nini sasa Serikali isiweke utaratibu wa kuwakopesha waathirika hawa kwenye vikundi mikopo midogo midogo ili waweze kupata fedha waweze kufanya shughuli ndogo ndogo kama vile kilimo, kufuga na bustani ili kuwainua kiuchumi au kuweza kupata fedha za kuweza kujikimu kwa maana ya kuwasaidia kuishi vizuri kwa kupata mahitaji madogo madogo? Ahsante sana.

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, concern ya Mheshimiwa Mbunge ni kwamba ikiwezekana hizi dawa zitolewa katika zahanati zote, naomba niseme sasa hivi tumeanzisha zile center maalum na tutambue kwanza zoezi hili lilipoanza tulikuwa tunafanya katika Hospitali za Wilaya lakini tuka-scale up hii programu sasa imeenda katika vituo vya afya mpaka zahanati.
Kwa hiyo, tunachukua hoja hii ya msingi lengo kubwa ikiwa ni jinsi gani tutafanya tuwasaidie wananchi wetu waweze kupata huduma kwa karibu.
Kwa hiyo, tutashirikiana na wenzetu Wizara ya Afya, kuangalia tufanyeje mambo yetu ya kisera ili wananchi wetu wa Tanzania ambao wameathirika na janga la UKIMWI waweze kupata tiba kwa maeneo ya karibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili amesema kwamba hawa waathirika wengi wao ni maskini, ni kweli na ndiyo maana ukiangalia mipango ya Serikali hivi sasa hata ule mpango wa TASAF, lengo kubwa ni zile kaya maskini ambazo upatikanaji wa fedha inakuwa ni tatizo tunaziingiza katika mpango wa TASAF ziweze kupata fedha kuweza kujikimu katika maisha yao.
Hata hivyo, nizielekeze Halmashauri zote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa vile tunakuwa na mpango maalum wa kuziwezesha familia zetu hasa za wanawake na vijana ambapo asilimia tano ni kwa vijana na asilimia tano ni kwa wanawake, tuangalie kama tuna watu ambao wameathirika basi familia hizi tuzipe kipaumbele katika suala zima la mikopo ili waweze kushiriki katika suala la uchumi ili kujikomboa na umaskini.

Name

Masoud Abdalla Salim

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtambile

Primary Question

MHE. JORAM I. HONGOLI aliuliza:- Waathirika wa UKIMWI katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe wamekuwa wakipoteza maisha haraka zaidi kutokana na kutembea umbali mrefu kwenda kupata huduma za matibabu. Je, ni lini Serikali itaongeza bajeti ya ujenzi, vifaa tiba na dawa katika kila kijiji na vituo vya afya kwa kila kata?

Supplementary Question 2

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Katika swali la msingi muuliza swali Mheshimiwa Joram Hongoli alisema kwamba wamekuwa wakipoteza maisha kule Njombe kutokana na kutembea umbali mrefu bila kupata matibabu.
Pia kule Njombe na maeneo mengine ya karibu kuna tatizo au tabia ya kurithiana wajane na wagane pale ambapo mmoja amefariki bila kupimwa vizuri afya zao. Wengine wamekwenda mbali zaidi, kumekuwa na tabia ya kwenda katika mapango jambo ambalo linaongeza matatizo ya VVU na UKIMWI na viongozi ndani ya Halmashauri wamekuwa wakilifahamu suala hili.
Je, Serikali ina mkakati gani wa ziada ili kuhakikisha kwamba tabia ya kurithiana wajane na wagane na matambiko katika mapango unakomeshwa katika maeneo hayo?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala analozungumzia Mheshimiwa Masoud ni kweli ni jambo halisia na lipo. Miongoni mwa sababu kubwa zinazosababisha hili janga la UKIMWI liweze kuongezeka ni ile tabia ya kwamba mtu amefariki halafu mtu mwingine anamrithi, lakini kuna visababishi mbalimbali. Jukumu letu kubwa hapa sisi kama Serikali ni kutoa elimu kwa wananchi ni vitu gani ambavyo vinasababisha ongezeko la UKIMWI katika maisha yetu. Katika suala hili zima la kurithiana, Serikali imekuwa ikitoa elimu mara kwa mara kwamba utaratibu ule wa zamani wa kimila kwamba mtu amefariki bila kujua afya zao zikoje basi shemeji au mtu mwingine anamrithi si utaratibu mwema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaelekeza maeneo mbalimbali hasa katika Halmashauri zetu kwa sababu Serikali za Mitaa ziko kwenye maeneo yote kuendelea kutoa elimu hii. Ni vyema wananchi wote sasa wajue kwamba programu ya upimaji wa afya zetu ni jambo la msingi kwa sababu sio wagane peke yake hata katika hali ya kawaida katika suala zima la ndoa ajenda ya kupima afya zetu ni jambo la msingi ili kuzilinda familia zetu na watoto watakaozaliwa.

Name

Edward Franz Mwalongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Njombe Mjini

Primary Question

MHE. JORAM I. HONGOLI aliuliza:- Waathirika wa UKIMWI katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe wamekuwa wakipoteza maisha haraka zaidi kutokana na kutembea umbali mrefu kwenda kupata huduma za matibabu. Je, ni lini Serikali itaongeza bajeti ya ujenzi, vifaa tiba na dawa katika kila kijiji na vituo vya afya kwa kila kata?

Supplementary Question 3

MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Kibena katika Jimbo la Njombe Mjini ndiyo inayotumika kama Hospitali ya Mkoa wa Njombe lakini haina kipimo cha x-ray.
Je, Serikali ipo tayari kutuwezesha wananchi wa Jimbo la Njombe Mjini mashine ya x-ray ili iweze kusaidia wananchi wote wa Mkoa wa Njombe?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme kwamba amehamisha goli, goli limehama kutoka katika swali la msingi, hii ni kwa sababu Mheshimiwa Mbunge anaguswa na wananchi wa Njombe. Ni kweli pale hakuna x-ray na tulivyofika pale ilibainika kweli changamoto kubwa pale ni x-ray. Hata hivyo, tulitoa maelekezo kwa Halmashauri katika mipango yao ya bajeti kuhakikisha wanapata x-ray, aidha, kwa kupata mikopo kutoka NHIF au kutumia mikakati yoyote kupata funds.
Napenda nimtaarifu Mbunge kwamba suala hili tumelichukua na tutakaa pamoja naye kuangalia tufanye nini ili tuwaokoe wananchi wa pale Njombe wanaohudumiwa na Hospitali ya Kibena kupata x-ray kwa sababu mtu akiumia inakuwa shida. Tunatambua eneo hilo imepita barabara kubwa ya magari yanayotoka Songea, kwa hiyo, ajali zikitokea pale lazima waweze kupimwa na vipimo hivyo vya x-ray. Kwa hiyo, nitaomba tukae pamoja kuona ni jinsi gani tutakuwa na mpango mkakati, Halmashauri na Serikali tubadilishane mawazo ya jinsi ya kupata x-ray katika Hospitali ya Njombe.

Name

Eng. James Fransis Mbatia

Sex

Male

Party

NCCR-Mageuzi

Constituent

Vunjo

Primary Question

MHE. JORAM I. HONGOLI aliuliza:- Waathirika wa UKIMWI katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe wamekuwa wakipoteza maisha haraka zaidi kutokana na kutembea umbali mrefu kwenda kupata huduma za matibabu. Je, ni lini Serikali itaongeza bajeti ya ujenzi, vifaa tiba na dawa katika kila kijiji na vituo vya afya kwa kila kata?

Supplementary Question 4

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya ya Kilema inahudumia zahanati zaidi ya 13; lakini zahanati hizo zina upungufu mkubwa wa vifaa tiba pamoja na watumishi ambapo zahanati ya Miwaleni imefungwa kabisa kwa kukosa watumishi. Ni nini tamko la Serikali kuhusu watumishi hawa kwenye zahanati zote 13?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka Mheshimiwa Mbatia ali-raise concern hii nadhani wiki iliyopita kuhusu hospitali hii. Mimi nafahamu wazi hata katika zoezi letu hili la uhakiki wa watu walioghushi vyeti, katika sekta ya afya tutakuwa na changamoto kubwa sana ya kukosa wataalam. Ndiyo maana Mheshimiwa Rais juzi alitoa maelekezo kwamba tutakuwa na ajira takribani 52,000 lakini miongoni mwao watakuwa ni wa kada ya madaktari, wahudumu wa afya pamoja na wauguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimtoe shaka Mheshimiwa Mbunge kwamba katika ajira mpya tutaipa kipaumbele zahanati yake kwa sababu tunajua kuna vifaa vingi vimewekezwa ni lazima tupate wataalam wa kufanya ile. Kwa hiyo, tutalichukulia kwa umakini mkubwa ili kuwasaidia wananchi wa Vunjo waweze kupata huduma.

Name

Kangi Alphaxard Lugola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwibara

Primary Question

MHE. JORAM I. HONGOLI aliuliza:- Waathirika wa UKIMWI katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe wamekuwa wakipoteza maisha haraka zaidi kutokana na kutembea umbali mrefu kwenda kupata huduma za matibabu. Je, ni lini Serikali itaongeza bajeti ya ujenzi, vifaa tiba na dawa katika kila kijiji na vituo vya afya kwa kila kata?

Supplementary Question 5

MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa suala la umbali linalowakabili wagonjwa wa UKIMWI kule Njombe ndilo hilo hilo ambalo linawakabili akina mama wajawazito wa Jimbo la Mwibara. Kutoka katika Kituo cha Afya cha Kasiguti pamoja na Kisorya kwenda Hospitali ya Misheni ni takribani kilometa 40. Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari baada ya Bunge hili la bajeti kuambatana na mimi ili twenda kwenye Kituo cha Afya cha Kisorya na Kasuguti ajionee namna ambavyo wananchi wametumia nguvu zao kujenga wodi ili Serikali iweze kutusaidia kukabiliana na changamoto ya umbali mrefu inayowakumba akina mama wajawazito?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi pamoja na Waziri wangu Mheshimiwa Boniface Simbachawene tumekuwa na mkakati mkubwa sana wa kuyafikia maeneo mbalimbali. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya hapa tutaangalia tufanye utaratibu gani ili tuweze kufika katika maeneo yake, lakini siyo hapo peke yake tutafika mpaka Rorya pamoja na Tarime kule kwa sababu kuna changamoto mahsusi katika Mkoa wa Mara ambazo lazima twende tukazifanyie kazi.