Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Zuberi Mohamedi Kuchauka
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Liwale
Primary Question
MHE. ZUBERI M.KUCHAUKA (K.n.y. MHE. VEDASTO E. NGOMBALE) aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuitangaza Wilaya ya Kilwa kuwa ni moja ya maeneo makubwa ya Kiutalii katika Kanda ya Kusini kwa kuzingatia historia yake, maajabu mbalimbali yaliyopo, fukwe, mapango, malikale, mbuga, mabwawa na utamaduni wake?
Supplementary Question 1
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mheshimiwa Waziri anasema kwamba mpango mkakati mmojawapo ni kutangaza kuingiza hiyo tovuti na filamu. Hapa swali lilikuwa linataka kujua mkakati thabiti wenye dhamira ya kweli kwa sababu hapo wanaposema, hata barabara ya kufika kwenye hivyo vivutio hakuna. Sasa huu mkakati, hata hao watu unaoingiza kwenye filamu, watafikaje kule Kilwa ambapo kwenye hivi vivutio hamna barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri kwamba Pwani ya Afrika Mashariki ni mahali ambapo kwanza walikuwa na currency yao, yaani walikuwa na pesa yao; ni Kilwa, lakini haya yote watu hawayajui.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kwa mfano, ukiangalia Vita ya Majimaji; asili ya vita hii ni Kilwa, lakini makumbusho ya Vita ya Majimaji yako Songea. Sasa Wananchi wa Kilwa walitaka waone, Serikali inafanya taratibu gani kuirudisha Vita ya Majimaji Kilwa na kuitangaza Kilwa kama sehemu ya Utalii? Hilo ni swali la kwanza.(Kicheko)
Name
Eng. Ramo Matala Makani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Mheshimiwa Kuchauka nafikiri wewe na mimi kwa pamoja tunafahamu kwamba historia ya kwamba Kilwa haifikiki au haipitiki ilikuwa labda zamani; lakini kwa sasa hivi ninavyofahamu na nafikiri Wabunge wengi wanafahamu, kama unazungumzia barabara ya kufika mpaka Kilwa; ni ya lami, kwa maana vivutio vya Mjini Kilwa, yale magofu pamoja na maeneo mengine ya utalii wa kiutamaduni pamoja na utamaduni wa kihistoria.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama anazungumzia Mbuga ya Selous, kufika ndani ya Hifadhi ya Selous, ni kweli kuna namna na haja ya kuboresha miundombinu ya kufika ndani ya Selous na kuzunguka ndani ya Selous yenyewe kwa maana ya barabara; lakini iko miundombinu ambayo ni maeneo ya malazi au facilities za malazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, upande mmoja ni jukumu la Serikali, kwa mfano kama barabara, lakini upande mwingine ni jukumu la taasisi binafsi ambazo sasa Mheshimiwa Mbunge usaidie Serikali mnapokaa kwenye Mabaraza kule ya Halmashauri kuweza kuona namna ambavyo mnaweza mkashirikiana na Serikali kuweza kuhamisha wawekezaji wakaweza kuweka vivutio ndani ya Selous.
Mheshimiwa Naibu Spika, pengine nimtaarifu tu Mheshimiwa Kuchauka kwamba mkakati anaoutaka mahususi sasa kwa ajili ya Kilwa yenyewe; sasa hivi tunakamilisha hadidu za rejea kwa ajili ya mkakati mahususi kabisa kwa ajili ya Kilwa. Siyo Kilwa peke yake, kwa ajili ya southern circuit. Huu ni utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Miaka Mitano ambao tunaposema kutekeleza Mpango wa Miaka Mitano, maana yake tunazungumzia diversification kwamba kutanua wigo wa vivutio vya utalii nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kupitia mkakati huo, tuna uhakika kwamba tunakwenda kuboresha mazingira ambayo yataboresha utalii ndani ya Selous lakini pia vivutio ambavyo viko Kilwa Mjini hasa vya utamaduni na kihistoria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la Vita ya Majimaji, hilo suala bado linajadiliwa. Wako upande mmoja katika Kambi nyingine wanasema ni muhimu zaidi kuzingatia kwamba historia ya Majimaji ina mizizi zaidi Kilwa, wengine wanasema ina mizizi zaidi Songea. Sasa nafikiri unatingisha kichwa kwa sababu hayo ni maoni yako, lakini nafikiri suala hili linajadilika, lakini hali ilivyo kwa sasa hivi, mazingira yaliyoko sasa hivi yanazingatiwa kwa mujibu wa historia hiyo hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri utakumbuka siku za nyuma tulikaa hapa tukawa tunazungumzia kuhusu suala la historia kwamba wengine wanasema historia inabidi ziandikwe upya, lakini hatuna sababu ya kuandika upya, lakini tutaweza kuweka utaratibu ulio makini kuweza kuweka suala hilo likakaa sawa.
Name
Edwin Mgante Sannda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kondoa Mjini
Primary Question
MHE. ZUBERI M.KUCHAUKA (K.n.y. MHE. VEDASTO E. NGOMBALE) aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuitangaza Wilaya ya Kilwa kuwa ni moja ya maeneo makubwa ya Kiutalii katika Kanda ya Kusini kwa kuzingatia historia yake, maajabu mbalimbali yaliyopo, fukwe, mapango, malikale, mbuga, mabwawa na utamaduni wake?
Supplementary Question 2
MHE. EDWIN M. SANNDA: Nakushukuru sana Mheshimiwa Naibu Spika, kwa fursa. Wilaya ya Kondoa hususan pale Kata ya Kolo na nyinginezo, ipo michoro ya mapangoni ambayo ni vivutio vikubwa sana vya kihistoria kwa ajili ya utalii, lakini vimekuwa havitangazwi sana. Je, Serikali ina mpango gani wa kuvitangaza ili kizazi cha sasa na cha baadaye kitambue hii fursa na kuweza kuitumia ili hatimaye pia kipato kiongezeke?
Name
Eng. Ramo Matala Makani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, michoro ya kwenye mapango ya Kondoa ni mojawapo kati ya maeneo ya utalii wa kiutamaduni na utalii wa kihistoria ambao tayari unafahamika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ambayo imebaki sasa hivi ni ya kuweza kuboresha matangazo kwa maana ya utangazaji wa utalii; na nimesema katika majibu yangu ya maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Kuchauka, kwamba tunachokifanya sasa hivi ni utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao unasisitiza juu ya diversification of tourist attractions, kwamba tunataka kuendelea kuboresha na kutanua wigo wa vivutio vya utalii ili tuondokane na vivutio vya utalii vinavyohusiana na wanyamapori peke yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, chini ya mpango huu, chini ya utekelezaji wa Mpango wa Miaka Mitano, tunakwenda kutangaza zaidi vivutio ambavyo ni vipya; vimekuwepo lakini vimekuwa havitiliwi mkazo, lakini sasa tunakwenda kuvitilia mkazo kwa maana ya kwamba tutaboresha zaidi matangazo kwa ajili ya vivutio vya aina hiyo.
Name
Anthony Calist Komu
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Moshi Vijijini
Primary Question
MHE. ZUBERI M.KUCHAUKA (K.n.y. MHE. VEDASTO E. NGOMBALE) aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuitangaza Wilaya ya Kilwa kuwa ni moja ya maeneo makubwa ya Kiutalii katika Kanda ya Kusini kwa kuzingatia historia yake, maajabu mbalimbali yaliyopo, fukwe, mapango, malikale, mbuga, mabwawa na utamaduni wake?
Supplementary Question 3
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kule Moshi Vijijini kuna vyanzo vingi vya kitalii ambazo havijatangazwa vizuri. Kwa mfano, kule Kata ya Uru Mashariki kuna maanguko ya maji ya ajabu sana yanaitwa Mnambeni na hivi karibuni katika Kata ya Mbokomu, kumevumbuliwa mti ambao unasemekana ni mrefu kuliko miti yote katika Bara la Afrika. Sasa nataka kufahamu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, ni lini Serikali itachukua hatua za makusudi kuweza kuvitambua hivi vyanzo na kuvitangaza inavyostahili ili tuweze kuvitumia kikamilifu?
Name
Eng. Ramo Matala Makani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu hii ni tajiri sana ya vivutio vya utalii. Kama nafasi ingekuwepo, karibu kila Mbunge hapa angeweza kusimama na kueleza kwamba katika Halmashauri yake kuna kivutio hiki na kile; sasa suala la kuboresha utangazaji siyo suala la Serikali peke yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Serikali inaendelea na utaratibu wa kuweza kuboresha matangaza ambayo sasa hivi tunafanya, nitoe wito sasa kwa Mbunge moja moja lakini kupitia Halmashauri zinazohusika kuanza kuvibainisha vivutio vilivyopo kwenye maeneo yao ili viweze kwenda mbele ya wataalam wa Idara ya Utalii katika Wizara ya Maliasili na Utalii tuweze kuviorodhesha kwa pamoja, halafu tukubaliane kama vinakidhi viwango vya Kimataifa kama vivutio, tuweze kuvifanyia grading, halafu baada ya pale tuendelee na utaratibu wa kutangaza tukitambua kwamba ni jukumu letu sote.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2016 mwananchi mmoja wa Kenya alitamka maneno kwenye mkutano mmoja wa Kimataifa kwenye nchi mojawapo nje kule, kwa kurusha tu clip ndogo tu lakini ikatingisha dunia, lakini pia na sisi Watanzania tukaanza kusema kwa nini wanataka kuteka vivutio vyetu? Ule haukuwa mpango wa Serikali, ni mtu mmoja tu alifanya vile.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wananchi wa Tanzania nasi kwanza tushiriki katika utalii wa ndani ili tuvifahamu vivutio vyetu na sifa zake halafu baada ya pale nasi tuweze kushiriki kama Watanzania kutangaza vivutio vyetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaweza kushirikiana na wenzetu walioko nchi za nje kwa utaratibu wa diaspora ili tuweze kufanya nchi yetu ikapata kutangazwa sawa sawa kwa maana ya vivutio vya utalii. (Makofi)
Name
Rev. Peter Simon Msigwa
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Iringa Mjini
Primary Question
MHE. ZUBERI M.KUCHAUKA (K.n.y. MHE. VEDASTO E. NGOMBALE) aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuitangaza Wilaya ya Kilwa kuwa ni moja ya maeneo makubwa ya Kiutalii katika Kanda ya Kusini kwa kuzingatia historia yake, maajabu mbalimbali yaliyopo, fukwe, mapango, malikale, mbuga, mabwawa na utamaduni wake?
Supplementary Question 4
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na swali la msingi ambalo niliuliza kuhusu vivutio, Mji wetu wa Iringa ni Mji mkongwe ambao una historia kubwa ya Mtemi wetu Mkwawa jinsi alivyopambana na Mjerumani. Ni juhudi zipi za makusudi ambazo zinafanywa na maliasili kuhakikisha kwamba mji huu wa Iringa na historia kubwa ya Mtemi Mkwawa inaendelea kujulikana katika dunia nzima na Tanzania kwa ujumla?
Name
Prof. Jumanne Abdallah Maghembe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwanga
Answer
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni hatua nyingi zinafanywa kuboresha utalii katika eneo zima la Kusini mwa Tanzania, lakini hususan Mji wa Iringa na viunga vyake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tumefungua makumbusho ya historia ya Iringa na utemi wake kule. Pili, Serikali inapanua Uwanja wa Nduli kama ulivyoona kwenye bajeti. Vile vile Serikali imepanga kujenga barabara kutoka kwenye geti la Ruaha kuja Ruaha Mjini. Shughuli hii tumeishughulikia sana na Mheshimiwa Lukuvi katika kuitekeleza pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2016 tumeanza kwa mara ya kwanza kuwa na Maonesho ya Utalii Kusini mwa Tanzania na yalikuwa Iringa na mwaka huu maonesho hayo ni makubwa zaidi. Waheshimiwa Wabunge, nawakaribisha mje kushiriki katika maonesho hayo. Ahsante.
Name
Martin Alexander Mtonda Msuha
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbinga Vijijini
Primary Question
MHE. ZUBERI M.KUCHAUKA (K.n.y. MHE. VEDASTO E. NGOMBALE) aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuitangaza Wilaya ya Kilwa kuwa ni moja ya maeneo makubwa ya Kiutalii katika Kanda ya Kusini kwa kuzingatia historia yake, maajabu mbalimbali yaliyopo, fukwe, mapango, malikale, mbuga, mabwawa na utamaduni wake?
Supplementary Question 5
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kule Wilayani Mbinga yako mawe mawili makubwa ya ajabu ambayo yanafahamika kwa jina la Mawe ya Mbuji; mawe haya yanasadikika kuwa ni jiwe la kike na la kiume; lakini pia katika mawe hayo viko viumbe hai vyenye kimo kifupi sana vinavyofanana na binadamu, viumbe hivi huwa vinajitokeza hasa msimu wa michezo ya utamaduni. Je, ni lini Serikali itafanya utafiti ili kubaini ni viumbe vya aina gani hivyo ambavyo vinaishi katika mawe hayo na hatimaye kutangaza eneo hilo kama eneo la utalii? (Makofi)
Name
Eng. Ramo Matala Makani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kwenye maswali ya nyongeza yaliyotangulia, nimesema nchi hii ni tajiri sana ya vivutio vya utalii, jambo ambalo hatujalikamilisha bado na tunaendelea kulifanya ni kuwa na orodha ya vivutio hivyo vilivyohakikiwa kwa sababu siyo kila kitu ambacho mtu mmoja anaweza kukiona kwamba kinatosheleza kuwa kivutio cha utalii, kinakuwa hivyo; ni mpaka wataalam wanaohusika waseme kwamba sasa hiki kinakidhi viwango vya Kimataifa vya kuwa kivutio cha utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maliasili na Utalii, tayari imeshawasiliana na Halmashari zote nchini ili kuweza kuviorodhesha vivutio hivyo, vifike Wizarani, tuvifanyie uchambuzi halafu tuweze kuviweka katika makundi (grading) halafu tuweze kuweka mkakati wa pamoja wa namna gani ya kutangaza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema jukumu la kutangaza lisiwe jukumu la Serikali peke yake; kama mnavyofahamu na mnavyoona, dunia ya sasa ni kama kijiji; na kila mmoja akitumia wajibu wake wa kutumia mifumo ya mawasiliano ya kisasa, tunaweza kutangaza nchi yetu kwa namna ambayo ni ya mafanikio zaidi.
Name
Dr. Dalaly Peter Kafumu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Igunga
Primary Question
MHE. ZUBERI M.KUCHAUKA (K.n.y. MHE. VEDASTO E. NGOMBALE) aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuitangaza Wilaya ya Kilwa kuwa ni moja ya maeneo makubwa ya Kiutalii katika Kanda ya Kusini kwa kuzingatia historia yake, maajabu mbalimbali yaliyopo, fukwe, mapango, malikale, mbuga, mabwawa na utamaduni wake?
Supplementary Question 6
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa nchi yetu ina maeneo mengi ya masalia ya Wafalme pamoja na majengo; kwa mfano, Mtemi Shomali Mwanansali wa Igurubi, kuna majengo ya Mtemi Humbi Ziyota Mwanantinginya pale Ziba. Kwa nini Serikali sasa isiyatambue maeneo haya yote yenye majengo na masalia ya Watemi nchini kote na kuyatangaza? Najua wenzetu kutoka Ulaya watakuja kuyaangalia. Ahsante sana.(Makofi)
Name
Eng. Ramo Matala Makani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ambayo yalikuwa makazi au hata ni makazi hata sasa ya viongozi wetu wa kimila; Watemi, Mamwinyi na wengineo, kweli ni maeneo ambayo licha ya kwamba ni ya kihistoria, yana vivutio kwa sababu kimsingi yana record ambayo inaweza kutupa hata mafundisho kwa ajili ya siku za usoni. Kama ambavyo tunajua historia na faida zake, kwamba unaangalia tulikotoka, hapa tuliko na huko mbele tuendako, inaweza kuwa ni mchango mkubwa sana kwa upande wa maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaweza tukajiuliza, hivi ni kwa kiasi gani sisi wenyewe kwanza tunatembelea maeneo hayo? Ni kwa kiasi gani sisi wenyewe tunayapenda maeneo hayo na tunayatunza kabla hatujafikiria hata kuyatangaza kwa ajili ya watalii kutoka nje? Sasa wito nilioutoa kabla na napenda kuurudia tena hapa, tuanze sisi wenyewe kwanza kwenye Halmashauri zetu kuanza kuthamini maeneo hayo, kuyaweka vizuri katika ubora wake, halafu baada ya pale, kuwasiliana na Wizara ya Maliasili na Utalii na kuweza kuona namna gani tunaweza kuviboresha na kuvitangaza vivutio hivyo ndani na nje.
Name
Sixtus Raphael Mapunda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbinga Mjini
Primary Question
MHE. ZUBERI M.KUCHAUKA (K.n.y. MHE. VEDASTO E. NGOMBALE) aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuitangaza Wilaya ya Kilwa kuwa ni moja ya maeneo makubwa ya Kiutalii katika Kanda ya Kusini kwa kuzingatia historia yake, maajabu mbalimbali yaliyopo, fukwe, mapango, malikale, mbuga, mabwawa na utamaduni wake?
Supplementary Question 7
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana nami kupata fursa hii ya mwisho ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa mazingira ya kusini katika maana ya Ruaha, Rufiji mpaka Kilwa yanafanana kabisa na Hifadhi ya Msitu wa Liparamba unaounganisha upande wa Nyasa, Mbinga Mjini na upande wa Msumbiji. Ni lini Hifadhi ya Liparamba itapata hadhi inayostahili ili iwe kivutio cha utalii kwa center ya Kusini, hususan tunaunganisha nchi mbili za Msumbiji na nchi ya Malawi? (Makofi)
Name
Eng. Ramo Matala Makani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli kwamba Hifadhi ya Liparamba iliyopo mkoani Ruvuma ni mojawapo kati ya maeneo ya hifadhi ya wanyamapori machache sana kwa Mkoa wa Ruvuma, lakini tajiri kwa wanyamapori na ambayo inastahili kabisa kuwa kwenye viwango vya Kimataifa vya kuwa mojawapo ya maeneo yenye vivutio vya utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli pia kwamba katika siku za nyuma, mkazo wa kuweka mipango na mikakati ya kuweza kuboresha utalii katika hifadhi hiyo, hapo nyuma hakukuwa na mipango madhubuti kwa sababu hatukuwa na utaratibu wa kuweza kuboresha utalii upande wa kusini mwa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema hapo awali kwamba katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, tumezungumzia juu ya ku-diversify au kuweka utaratibu wa kuwa na mtawanyiko wa vivutio kwa maana ya vivutio vyenyewe; aina za vivutio, pia mahali vivutio vilipo hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, chini ya mpango huo, tutakwenda kuboresha utalii kusini na Hifadhi ya Liparamba ni mojawapo kati ya hifadhi ambazo zinaenda kuwekwa katika kipaumbele ili kuhakikisha kwamba sasa watalii hawaendi tu Arusha, Moshi, Kilimanjaro na maeneo ya Kaskazini, pia waweze kwenda Mbeya, Songea, Mtwara na maeneo mengine ya Kusini.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Mbunge atupe nafasi tuweze kukamilisha mipango iliyopo kwa ajili ya kutekeleza sehemu ya mpango wa miaka mitano ili tuweze kuona sasa tunaboresha utalii upande wa kusini.