Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Pudenciana Wilfred Kikwembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kavuu

Primary Question

MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE aliuliza:- Serikali imekuwa na dhana ya ugatuaji madaraka kwa wananchi ili kuharakisha maendeleo, hususan katika sekta za afya na elimu:- Je, Serikali inasema nini kuhusu mfumo huo kutokuwa na tija endelevu katika sekta hizo?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipatia nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa, napenda nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, suala hili ni la kikatiba kwa maana ya kwamba linahusisha Serikali ya wananchi kwa maana ya Serikali za Vijiji. Kwa kuwa wananchi wamekuwa wakichangia takribani 20% ya maendeleo katika maeneo yao ya vijiji. Je, Serikali sasa inafikiria nini kupeleka pesa za maendeleo kwa wakati ili wananchi hawa waweze kujua sasa ile miradi ni mali yao? (Makofi)

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli dhana hii inapeleka fursa kwa wananchi na ni kweli tumeshuhudia wananchi katika maeneo mbalimbali wakishiriki vyema katika kutekeleza dhana hii kwa kujitolea katika miradi mbalimbali ya maendeleo. Hata hivyo, naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba Serikali kwa kipindi cha sasa na nina maana itakapofika mwezi wa Sita mtaona jinsi gani imepeleka nguvu kubwa sana katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano katika sekta ya afya mwaka huu peke yake fedha tulizopeleka katika mifuko mbalimbali ikiwepo Basket Fund ni zaidi ya shilingi bilioni 79 na sasa hivi tumeshapeleka fedha za quarter ya nne ambapo tunaenda kukamilisha shilingi bilioni 106, hii ni sekta ya afya peke yake. Tumefanya hivyo pia katika sekta ya elimu na maeneo mbalimbali na juzi juzi hapa tumenunua vifaa vya maabara katika maabara zote zaidi ya 1,000 ambapo vyote vilikuwa vinagharimu shilingi bilioni 16.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kuna fedha nyingine za LDGD ambazo zimeenda moja kwa moja ambazo hazina ukakasi katika kuzitoa kwake. Serikali imepeleka hela za kutosha na ni mara ya kwanza baada ya miaka minne iliyopita tulikuwa hatufanyi hivyo. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kuweka nguvu kubwa ya kutosha, lengo kubwa ikiwa ni kuwawezesha wananchi kutekeleza miradi yao.

Name

Pauline Philipo Gekul

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Babati Mjini

Primary Question

MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE aliuliza:- Serikali imekuwa na dhana ya ugatuaji madaraka kwa wananchi ili kuharakisha maendeleo, hususan katika sekta za afya na elimu:- Je, Serikali inasema nini kuhusu mfumo huo kutokuwa na tija endelevu katika sekta hizo?

Supplementary Question 2

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Mpango wa Afya ya Msingi (MMAM) muda wake ilikuwa uishe mwaka huu 2017 lakini fedha hizo haziji kwa muda mrefu, takribani kama miaka mitatu nyuma fedha haziji. Ni kwa nini mpango huu wa MMAM ambao ulikuwa unasaidia kujenga zahanati zetu umekwama na anawaambiaje Watanzania kwa sababu maboma/zahanati nyingi bado hazikajamilishwa?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema hapa sio suala la maboma ya afya peke yake hata maboma ya nyumba za Walimu halikadhalika madarasa. Kipindi fulani hapa takribani miaka mitatu, minne fedha hizi zilikuwa haziendi. Ndiyo maana nimesema kupitia Mfuko ule wa LDGD ambapo kwa sasa mwaka huu kwa mara ya kwanza, namshukuru Mheshimiwa Waziri wangu alilisimamia kwa karibu sana, ndiyo maana hivi sasa Wabunge kama tumepitia katika Kamati zetu za Fedha katika Halmashauri zetu tunaona kuna fedha nyingi zimekuja ambazo zimesaidia kwa kiwango kimoja au kingine kuweza kuhakikisha maboma mengi sana yameweza kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshuhudia hili kwani nilipopita maeneo mbalimbali nilikuwa nikipata taarifa mbalimbali kutoka kwa Wakurugenzi jinsi gani fedha hizi sasa wameweza kuzielekeza katika kuhakikisha zile nguvu za wananchi ambazo wamezitoa hazipotei kwa kukamilisha viporo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, naomba tushirikiane kwa pamoja. Lengo kubwa ni kutekeleza mpango wa D-by-D kama alivyosema Mheshimiwa Dkt. Kikwembe, tufanye hili kwa ajili ya mustakabali mzuri kwa kuunganisha nguvu za wananchi katika kuhakikisha Taifa hili linaenda mbele.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nataka tu kumfahamisha Mheshimiwa Gekul kwamba tayari tumeshaanza kuufanyia mapitio Mpango wa Afya ya Msingi (MMAM). Kwa hiyo, tunategemea kabla ya mwisho wa mwaka tutakuwa tumetoa mpango wa pili ambao utatueleza kama, je, ni lazima tuwe na zahanati kila kijiji wakati sasa hivi barabara zinapitika? Je, ni lazima tuwe na kituo cha afya kila kata? Kwa hiyo, hayo maeneo yote tutayaangalia kwa upana wake. Lengo letu ni kuhakikisha tunasogeza huduma bora kwa wananchi. Ahsante sana.(Makofi)

Name

Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Primary Question

MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE aliuliza:- Serikali imekuwa na dhana ya ugatuaji madaraka kwa wananchi ili kuharakisha maendeleo, hususan katika sekta za afya na elimu:- Je, Serikali inasema nini kuhusu mfumo huo kutokuwa na tija endelevu katika sekta hizo?

Supplementary Question 3

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na jitihada za Serikali kupeleka fedha za maendeleo, ugatuaji lazima uende sambamba na upelekaji wa resources hususan fedha za OC. Fedha za OC zimekuwa haziendi kwa kiwango kinachokusudiwa matokeo yake imekuwa inaathiri mipango inayopangwa na Halmashauri kwa kutekelezwa kutokana na makusanyo ya ndani. Matokeo yake fedha za makusanyo ya ndani sasa zinatumika kuendeshea ofisi badala ya kuelekezwa kwenye shughuli za maendeleo kama inavyoelekeza ile 50%, ikiwepo 5% ya vijana na wanawake. Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha kwamba inapeleka fedha za OC ipasavyo ili kusudi makusanyo ya ndani yasiathiri utekelezaji wa shughuli za maendeleo, kama ambavyo zimepangwa na Halmashauri zetu? (Makofi)

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli na nakumbuka kwamba tulipokuwa katika kikao chetu cha ALAT kule Musoma, concern kubwa ilikuwa siyo fedha za OC peke yake hata pesa za maendeleo. Waheshimiwa Wenyeviti wa Halmashauri na Wakurugenzi wali-raise jambo hili katika ofisi yetu na ndiyo maana katika kipindi cha katikati baada ya harakati hizi kufanyika mmeona tumepeleka fedha nyingi sana za maendeleo na pesa za OC.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama ambavyo Mheshimiwa Waziri wangu siku zote amekuwa akisema definition ya OC maana yake ni Own Source plus zile fedha nyingine zinazotoka Serikali Kuu. Kwa hiyo, sisi Serikali tutajitahidi kwa kadiri iwezekanavyo OC iweze kwenda, lakini niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge katika maeneo yetu vilevile tuhakikishe makusanyo ya ndani haya yanaimarika kwa kiwango kikubwa kwa sababu tumeshuhudia hivi sasa kuna Halmashauri zingine zimefanya vizuri lakini nyingine zinasuasua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili ni jambo letu sisi sote. Upande wa Serikali tutajitahidi kufanya kila liwezekanalo kuziwezesha Halmashauri zetu ziweze kufanya kazi vizuri kwa sababu bila ya hivyo maana yake utekelezaji wa Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi utakuwa una matatizo. Kwa hiyo, naomba niwahakikishie kwamba Serikali itafanya kila liwezekanalo, tutakusanya mapato lakini tutayapeleka katika Halmashauri zetu ili miradi iweze kutekelezeka vizuri.